July 22, 2013
Katika
siku za karibuni baada ya kuzinduliwa kwa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ya
Tanzania, pamekuwepo na mjadala mkubwa kuhusu Muundo wa Muungano.
Shauku kubwa imekuwa juu ya Muundo wa Serikali tatu. Waandishi,
wachambuzi, wanasiasa na wasomi wametumia muda
mwingi kutoa maoni yao juu ya muundo. Ukisoma kwa makini na kufuatilia
mjadala huo,unapata hisia kuwa Muundo wa Muungano unachukuliwa kama
mwarobaini wa matatizo ya muungano na umasikini wetu. Sehemu kubwa ya
mjadala huo imejikita kwenye maudhui ya Haki na Usawa.
Sijakutana na msukumo wa kutosha kujadili kuhusu Ustawi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na watu wake, jambo linalonipa maswali ikiwa
tuliungana ili tuwe SAWA, tugawane HAKI au TUSTAWI. Ikiwa tutaweza
kupata jibu la kwanini tuliungana, tutakuwa tumeshapata jawabu la Muundo
unaofaa na sio kinyume chake. Lengo la andiko hili, ni kuongeza sauti
kuwa lengo la Muungano wetu ni Ustawi, na kuwa, Muundo wa Serikali Mbili
ndio njia ya kufikia ustawi huo, na kwamba changamoto za muungano
(kero) sio suala la Muundo (structural) bali mfumo (systemic), na kuwa unaweza kufumua au kurekebisha mfumo bila kuathiri Muundo.
Mantiki ya Muundo wa Serikali Mbili
Muundo wa Muungano wa Tanzania wa Serikali mbili haukutokana na
nasibu bali mantiki na maridhiano yaliyotokana na tathmini za mazingira
yaliokuwapo wakati huo. Mjadala mkubwa tokea Muungano kuanza na hata
sasa umejikita kwenye idadi ya Serikali zinazofaa ambapo wako
wanaozungumzia Serikali Moja, Serikali Mbili na Serikali Tatu. Aidha,
mjadala huu kuhusu idadi ya Serikali haswa tatu na moja umekuwa
ukifanyika kana kwamba ni wazo jipya au ugunduzi. Upo ushahidi kuwa hoja
hii sio mpya na kuwa ilikuwa mezani wakati uamuzi wa Serikali mbili
unafikiwa. Ushahidi huu unajidhihirisha kwa maneno ya Mwl. Nyerere
ambaye ni mmoja wa Waasisi wa Muungano hapa chini:
“Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa nchi moja,
tungeweza kufuata mojawapo ya mifumo ya kawaida. Lakini tulishindwa
kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika.
Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni
kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali moja ungefanya ionekane
kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania uhuru na Umoja
wa Afrika, hatukutaka tudhaniwe hata kwa makosa kwamba tunaanzisha
ubeberu. Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali moja. Shirikisho la
Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar
ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya
Shirikisho; na Tanganyika ingefanya hivyo hivyo. Lakini ni dhahiri
kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali ya
shirikisho. Kwa hiyo, Tanganyika ingeendesha Serikali ya watu milioni 12
na pia ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu
milioni12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa
gharama ya Serikali yoyote kati ya hizi ingekuwa ndogo. Gharama ya
Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, hata bila ya gharama za mambo
yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na
Tanganyika. Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha
Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya
Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na Serikali
yake, itaonekana imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na
Serikali moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na
tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa bila kuibebesha Tanganyika mzigo
wa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana. Hivyo ndivyo
tulivyofanya, na hiyo ndio asili ya muundo wa Muungano wa serikali
mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali
halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi” Mwl. J.K. Nyerere, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania.
Nashawishika kuamini, hadi nitakapo shawishiwa vinginevyo kuwa
mantiki iliyopelekea Serikali mbili ingali ina mashiko hata sasa, na
kuwa kama mantiki haijabadilika, basi uhalali wa hoja yenyewe ya
Serikali mbili nao haujabadilika. Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka
2012, Idadi ya Watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni milioni
44,928,923, kati ya hao, Tanzania Bara ina idadi ya watu milioni
43,625,354 (tuchukulie wote walioko bara ni watanganyika) na idadi ya
watu Zanzibar ni milioni 1,303,569 (tuchukulie hakuna Wazanzibari
wanaoishi bara). Aidha, takwimu zinaendelea kueleza kuwa Tanzania bara
ina kaya milioni 9,109,150 na Zanzibar ina kaya 253,608. Idadi ya ujazo
wa Watu kwa Kilometa za Mraba (Population Density) kwa upande wa bara ni
wastani wa watu 49 kwa kilometa moja ya mraba na Zanzibar ni watu 530
kwa kilometa moja ya mraba. Aidha, eneo la ukubwa wa ardhi ya Tanganyika
na ardhi ya Zanzibar haujaongezeka tokea nchi hizi mbili zilipoungana
mwaka 1964.
Kwa takwimu hizi, tujiulize, je kuna mabadiliko ya msingi katika
idadi ya watu ambayo sasa hayatafanya Zanzibar kuonekana kumezwa na
utaifa wake kupotea ikiwa tutakuwa na muundo wa Serikali moja? Je, baada
ya miaka 49 ya Muungano, utaifa wa Mtanganyika umepotea na kupotea huko
kunamaanisha kumezwa na uzanzibari? Je, watanganyika leo wamezanzibarishwa au watanganyika na wanzanzibari wametanzanianishwa
zaidi? Na kama wametanzanianishwa zaidi, hii si ndio hatua katika
kuelekea lengo la Umoja wa Afrika? Je, kasi ya ukuaji wa idadi ya watu
Zanzibar (530 kwa kilometa ya mraba) wakati ukubwa wa eneo haujaongezeka
hakufanyi umuhimu wa Muungano kuwa mkubwa zaidi leo kuliko
1964? Mwandishi mmoja wa nchi za Magharibi aliwahi kusema, “Unaweza
kukataa kukubaliana na Mwl. Nyerere lakini ni vigumu kupinga mantiki
yake”.
Hoja ya Usawa
Wanaopinga Muundo wa Serikali Mbili wanaibua hoja ya kutokuwepo kwa
usawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kinachostaajabisha ni kuwa kila
upande unadai kuwa upande mmoja unafaidi zaidi ya mwingine. Wanaendelea
kutuaminisha kuwa hata matatizo ya Muungano (kero) yanatokana na
Serikali mbili. Wako wanaosema kuwa Tanzania Bara inanufaika zaidi
kushinda Zanzibar katika Muundo uliopo kwa kuwa inaneemeka na kuendesha
Serikali ya Muungano na hivyo kutumia rasilimali za Muungano kwenye
kuendeleza Tanganyika kwa mambo ambayo sio ya Muungano. Hali kadhalika,
wapo wanaosema kuwa Zanzibar inafaidi zaidi kwa kuwa ina Serikali yake,
inajiamulia mambo yake na pia inafaidi yale ya Muungano kama kugawana
misaada, kumiliki ardhi bara, kuongoza hata Wizara zisizo za muungano na
mengineyo. Ili kuweka hali ya kile kinachodhaniwa ni usawa,
inapendekezwa kuwa njia pekee ya kufikia usawa ni kuwepo kwa Serikali
tatu.
Asili ya maumbile ya Tanganyika na Zanzibar, idadi ya watu katika
nchi hizo mbili, na tofauti za ukubwa wa uchumi wa nchi hizo mbili hata
kabla ya kuungana haviakisi Usawa. Ukweli huu mchungu unatueleza kuwa
tunapojadili hoja ya Usawa hatuna budi kuzingatia suala la Haki. Usawa
peke yake hauwezi kutupatia jawabu. Tukiendeleza hoja ya usawa peke
yake, wako watakaoupa usawa maana ya nusu kwa nusu. Mantiki ya usawa
itatutaka tufike mahala serikali za Tanganyika na Zanzibar zichangie
gharama za kuendesha Serikali ya Muungano ya watu milioni 44,928,923
nusu kwa nusu, na idadi ya wafanyakazi kwenye taasisi za Muungano iwe
nusu kwa nusu. Hatua hii haitaleta msawazo na hakuna atakayefaidika
zaidi ya Muungano kudhoofika. Swali la kujiuliza, tuliungana ili
tugawane nusu kwa nusu? Hili ndilo lengo la Muungano?
Hoja ya Haki
Muundo wa Serikali mbili pamoja na changamoto zake umezingatia utoaji
wa Haki. Kama alivyosema Mwalimu Nyerere, Muundo huo ulilenga kulinda
Haki ya Zanzibar ambayo kimaumbile, ilitishiwa ikiwa tungekuwa na Muundo
wa Serikali moja. Tanganyika haikuwa na hofu hiyo ya kumezwa wakati
ule na hata sasa. Ukweli wa hoja hii unajidhihirisha hata leo ambapo
hata baada ya miaka 49 ya Muungano chini ya Muundo wa Serikali mbili,
hofu ya Zanzibar kumezwa ingali ipo. Napata tabu kuamini kuwa hofu hii
itaisha kwa kuwa na Serikali tatu. Somo tunalopata hapa ni kuwa mantiki
ya Muundo wa Serikali mbili ilikuwa ni kutafuta urari kati ya USAWA na
HAKI kati ya nchi mbili huru zililokuwa zikiungana. Je, tunaona
uwezekano wa Muundo wa Serikali moja au tatu kutibu jeraha la hofu ya
ustawi wa Zanzibar?
Lengo la Muungano ni Ustawi
Pundamilia na Swala ni wanyama wa porini, wote hula majani na ni
VITOWEO vya wanyama wanaokula nyama, sifa zote hizo zinawapa usawa. Hata
hivyo, Pundamilia na Swala kwa maumbile yao wana utofauti, pundamilia
ni mkubwa kuliko Swala, na hivyo Pundamilia HUITAJI MAJANI MENGI KULA
ili ashibe tofauti na kiwango anachohitaji Swala. Lakini, Pundamilia na
Swala wana hofu moja, HOFU YA KULIWA na wanyama wanaokula nyama kama
Simba na Duma, hivyo ustawi wa kila mmoja, na ustawi wao kwa ujumla
unategemea kushirikiana. Pundamilia ana macho makali na huona mbali
lakini hana masikio makali, Swala ana masikio makali na husikia sana
lakini haoni mbali. Pundamilia na Swala huamua kuendeleza ustawi wao kwa
kula majani pamoja, bila kujali nani anakula majani kiasi kikubwa
kuliko mwingine, kwa kuwa ustawi wao dhidi ya hatari ya kuliwa na
wanyama wakali ni muhimu zaidi kuliko haki au usawa wa kila mmoja wao
ukisimama peke yake.
Tatizo kubwa tunalokabiliana nalo leo ni kuwa busara iliyopelekea
Muungano ni kubwa zaidi kuliko jumla ya baadhi ya busara ya wanasiasa na
wananchi tulionao leo. Nguvu kubwa imeelekezwa kujadili Muundo kuliko
lengo la kuungana. Muundo wa Muungano hauna budi utokane na lengo la
kuungana na sio kinyume chake. Muungano wetu ni muungano wa watu, kabla
ya kuungana watanganyika na wazanzibari walishachanganya damu na udongo,
miaka 49 baadae, muingiliano ni mkubwa kuliko ilivyokuwa mwaka 1964.
Hatukuungana ili tuandike Katiba, tuliungana kurasimisha muingiliano
wa damu uliokuwapo wa watu wa Tanganyika na Zanzibar. Hayo ma
‘print-out’ (Article of the Union) yanayotuzungusha kichwa leo sio lengo
la Muungano bali ni matokeo. Tuliunganisha nguvu zetu kwa lengo la
kulinda uhuru wa Tanganyika na mapinduzi ya Zanzibar dhidi ya wale wenye
jicho la husuda nasi katika mazingira ya vita baridi vya dunia.
Muungano wetu umeendelea kuwa wa kipekee na nchi pekee katika bara la
Afrika ambayo imetokana na Muungano hadi sasa. Miaka 49 baadae, tishio
la ustawi kwa nchi yetu katika mfumo wa utandawazi ni mkubwa na nchi
zote duniani zinatafuta kuungana kama njia ya kukabiliana na utandawazi.
Tishio la ustawi wa nchi yetu nje ya Muungano ni kubwa kwa Serikali ya
Tanganyika na Serikali ya Zanzibar kuliko tukiwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Umoja unaoonyeshwa na baadhi ya watanganyika na ule unaoonyeshwa na
baadhi ya wazanzibari katika kuunga mkono Serikali moja na tatu ni umoja
dhaifu, umoja unaojengwa na chuki. Ni rahisi sana kuunganisha watu kwa
chuki kuliko kuunganishwa na nia njema. Hata hivyo, chuki tangu kale na
hata sasa haijawahi kuwa msingi endelevu wa kuunganisha watu. Matatizo
ya Muungano wetu leo yanatokana na KUTOKUAMINIANA, HOFU na CHUKI za
viongozi, na KUTOKUFAHAMIANA katika ngazi ya wananchi.
Nilifika mara ya kwanza Zanzibar mwaka 1994 nilipomaliza Darasa la
Saba kwa kuwa Shule ya Msingi Forodhani ilikuwa na mahusiano na Shule
Dada ya Msingi (Nimesahau jina) huko Zanzibar, tukatembezwa makumbusho
ya Zanzibar na kuweza kuoanisha kile tulichojifunza kwenye historia
darasani na tulichokikuta Zanzibar. Kuanzia hapo nimekuwa na marafiki wa
kizanzibari na nimekuwa nikienda Zanzibar mara kwa mara kikazi na
kibinafsi. Kinyume chake, leo hii, mbara anaweza kusoma hadi akamaliza
Chuo Kikuu hajawahi sio tu kufika Zanzibar, bali kuwa na rafiki
Zanzibar, na vivyo hivyo kwa upande wa Zanzibar. Kutokufahamiana huleta
ombwe (vacuum) linalofidiwa na HISIA. Kwa maoni yangu matatizo ya
HISIA sio matatizo ya Muundo, na hayatatuliwi kwa KATIBA. Iwe Serikali
moja au tatu, mafanikio ya Muungano yatatokana na KUAMINIAMA,
KUHESHIMIANA na KUPENDANA.
Ni bahati mbaya kuwa wenye kuamini Serikali mbili, wamekuwa kimya
wakidhani mantiki ya Serikali mbili inajieleza yenyewe tu katika kile
kinachosemekana, “Chema chajiuza, Kibaya Chajitembeza”. Kwa kufanya
hivyo, wametoa mwanya kwa wanaoupinga mfumo huo kwa sababu wanazozijua
wao kuupaka matope na kupotosha mantiki yake. Mhe. Rais Ally Mohamed
Shein wa Zanzibar aliwahi kusema, “Mtemewa mate na wengi hurowa”.
Tumeacha Muundo uliopo pamoja na uzuri wake kutemewa mate kwa muda mrefu
mwishowe umerowa.
Nampongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa kuanzisha mfumo wa Serikali
Mbili za Muungano na SMZ kukutana na kuzungumza chini ya Uenyekiti wa
Makamu wa Rais. Tangu kuanzishwa kwa Mfumo huo, kero 13 zimeshajadiliwa,
hoja 6 tayari zimepatiwa ufunguzi, hoja nyingine 3 ziko katika hatua ya
mwisho kutatuliwa na hoja 4 zinaendelea kushughulikiwa. Toka mwaka 2012
hadi Aprili, 2013, vikao 9 vimekaa, vinne vikiwa vya Makatibu Wakuu na
viwili vya Mawaziri. Aghalabu, hatua kubwa kama hii kujulikana kwa
wananchi jambo ambalo linafanya watu kudhani kuwa Muundo ndio tatizo.
Umefika wakati wa Wananchi kuelimishwa kuhusu Muungano wetu, Muundo
wake, faida zake na gharama za kuubadilisha muundo au kuvunja Muungano
wenyewe. Kwa tulipofikia ni nadra sana jukumu hili kufanywa na wanasiasa
wa pande zote maana sehemu kubwa ya wanasiasa hao ndio kero ya
Muungano, kuliko kero zenyewe.
Na Mwandishi Wetu
Imenukuliwa kutoka :http://wewrite.or.tz/2013/07/mbadala-wa-muungano-kuelekea-katiba-mpya-fikra-za-nje-ya-boksi/