Na Peter Saramba na Mussa Juma, Mwananchi
(email the author)
Posted Jumatatu,Julai15 2013 saa 8:12 AM
Posted Jumatatu,Julai15 2013 saa 8:12 AM
Kwa ufupi
Yaibuka na ushindi wa kishindo katika kata zote nne za Arusha Mjini, wapiga kura wengi washindwa kujitokeza
Arusha. Chadema kimethibitisha
umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa
kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika
jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu
na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na
mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia
kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya
Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih
Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles
Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa
Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah
Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer
wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea wengine ambao ni John
Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima
(TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema
aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa
Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor
Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna
Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470
dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa
CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini
aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman
Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa
kura 2,761 na kumshinda Edna
Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa
kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa na kumi na moja na TLP
kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya
Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu
kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha
15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti
kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa
kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia
mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi
karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya
aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na
Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu
kukitetea kiti hicho.
Wachache wajitokeza
Uchaguzi ulikuwa na idadi ndogo ya wapigakura kulinganisha na chaguzi zilizopita.
Elerai inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya
wapigakura 23,885 waliojitokeza ni 3,824 tu ikifuatiwa na Kimandolu
yenye wapigakura 17,209 lakini waliopiga kura ni 3,967.
Kata ya Kaloleni ina wapigakura 12,674 hata hivyo,
waliopiga kura ni 2,292. Themi yenye wapigakura wachache kuliko zote
ikiwa na watu 6,387 lakini waliojitokeza kupiga kura ni 1,319 tu.
Licha ya idadi hiyo ndogo, baadhi ya wapigakura
waliojitokeza walishindwa kutimiza dhamira yao baada ya kugundulika
dosari kadhaa kwenye vitambulisho vyao na Daftari la Kudumu la
Wapigakura.
“NEC wamevuruga uchaguzi huu makusudi kwa kuchezea
Daftari la Wapigakura kwa nia ya kukibeba CCM. Haiwezekani waliopiga
kura Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 leo hii waambiwe majina yao hayamo kwenye daftari,” alilalamika mgombea udiwani Kata ya Kaloleni, Abbas Mkindi ‘Darweshi’.
Mkindi aliyewania kiti hicho kupitia CUF alitoa
mfano wa mtoto wake, Omar Othman mwenye kitambulisho cha mpigakura namba
32479962 alichokitumia mwaka 2010 kuzuiwa kupiga kura baada ya jina
lake kukosekana kwenye Daftari hilo. Wapiga kura wengine, Godchan Msella
mwenye kadi namba 32479396 na Richard Minja mwenye namba 32479311
alizuiwa kupiga kura baada ya kubainika kuwa namba iliyopo kwenye
Daftari ni tofauti na ya kadi yake.
Kutokana na kuwapo kwa mkanganyiko huo, Makamu
Mwenyekiti wa NEC, Hamid Mohamoud Hamid alilazimika kuwaita wataalamu wa
mfumo wa kompyuta (IT), katika Kituo cha Kupiga Kura cha Kaloleni
kusaidia, kazi ambayo ilifanywa na timu iliyoongozwa na Seif Mtero.
Malaba alikiri uwezekano wa kutokea tofauti za
tarakimu kwenye vitambulisho vya wapigakura na Daftari la Kudumu la
Wapigakura huku akishauri wasimamizi na mawakala wa vyama kutumia busara
kuruhusu wananchi wenye vitambulisho na maelezo sahihi kupiga kura.
“Tofauti ya tarakimu kwenye kadi ya mpigakura na
Daftari la Mpiga Kura ni kosa la NEC, hivyo siyo sahihi kuwahukumu
wapiga kura kwa kuwanyima haki yao ya kuchagua viongozi wawapendao,”
alisema Malaba.
Amani yatawala
Ukiacha dosari na idadi ndogo ya wapiga kura,
uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa tofauti na hofu
iliyokuwapo awali kwamba huenda vurugu zingeibuka kutokana na mvutano
uliopo kati ya vyama vya CCM na Chadema.
Hata hivyo, kulikuwa na kamatakamata na baadhi ya waliotiwa mbaroni ni wale waliokutwa na vitambulisho feki vya kupiga kura.
Katika eneo la Shule za Msingi Kimandolu na
Elerai, watu wawili walikamatwa kwa kukutwa na shahada feki za kura.
Kimandolu msichana aliyejitambulisha kwa jina la Mariamu alikamatwa
baada ya kwenda na kadi inayodaiwa kuwa feki.
Mpiga kura huyo alikamatwa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mtendaji wa Kata hiyo, Selemani Kikingo na kukabidhiwa kwa polisi.
Katika Kata ya Elerai, Zainabu Mohamed pia alikamatwa kwa tuhuma za kuwa na shahada yenye utata na baadaye kukabidhiwa polisi.
Katika maeneo hayo, pia vijana ambao waliokataa kuondoka karibu na vituo baada ya kupiga kura walikamatwa.
Msimamizi wa uchaguzi kwa upande wa CCM katika
Kata ya Kimandolu, Abraham Joseph alisema idadi kubwa ya waliojitokeza
ilikuwa ni ya vijana.
“Kituo hiki kina wapiga kura takribani 12,000
lakini kwa hali ilivyo sidhani kama wanaweza kufika hata wapigakura
4,000,” alisema Joseph.
Katika Kata ya Themi hali ilikuwa shwari. Makada
wa CCM, wakiongozwa na Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda walikuwa
wakizunguka katika vituo vyote vya kata hiyo.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari nao walikuwa wakizunguka
katika vituo.
chanzo: mwananchi.co,tz
chanzo: mwananchi.co,tz