Kwa ufupi
- Leo ni miaka 23 tangu Mandela atoke gerezani, bado asilimia 80 ya ardhi ya Afrika Kusini na rasilimali nyingi zinamilikiwa na wazungu wachache.
Pamoja na ukweli kwamba Rais mstaafu wa Afrika
Kusini, Nelson Mandela (94) analiliwa na dunia nzima kutokana na
historia yake ya kupinga siasa za ubaguzi zilizoigubika nchi hiyo kwa
muda mrefu, bado ana deni kubwa kwa wananchi wake na Waafrika kwa ujumla.
Mandela aliyekaa gerezani kwa miaka 27 akitumikia
kifungo cha maisha, alitoka bila kutegemea baada ya aliyekuwa rais wa
nchi hiyo , Fredrick de Klerk kumfutia adhabu hiyo.
Atakumbukwa kwa ujasiri wake wa hali ya juu pamoja
na wapiganaji wengine kwa kuwatetea watu weusi waliokuwa chini ya
utawala wa makaburu.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Mandela kutoka
gerezani mwaka 1990, ilibidi akubali baadhi ya masharti ikiwa pamoja na
kutowabugudhi makaburu.
Ni kweli, alipata nafasi ya kuwa rais wa kwanza
mweusi wa nchi hiyo ambayo aliitumikia kwa miaka mitano na kustaafu. Ni
kweli kwamba sasa Waafrika nchini humo walipata ahueni na kuanza
kushiriki uongozi wa nchi hiyo, lakini bado hali za maisha yao bado ni
ngumu.
Leo ni miaka 23 tangu Mandela atoke gerezani, bado
asilimia 80 ya ardhi ya Afrika Kusini na rasilimali nyingi zinamilikiwa
na wazungu wachache.
Waafika wengi wanaishi pembezoni wakisongwa na umasikini wao. Wengi ni vibarua kwenye migodi, viwanda na mashamba ya Wazungu.
Mfano mzuri ni wakati ule ulipozuka mzozo kwenye mgodi wa Marikana unaomilikiwa na kampuni ya Lonmin katika eneo la Rustenburg mwaka 2012.
Mgogoro huo ulisababisha mauaji ya watu 44
waliopigwa risasi na polisi baada ya kufanya mgomo na maandamano wakidai
nyongeza za mishahara, mgomo ulioambukiza na migodi mingine nchini
humo.
Hata hivyo, Rais Jacob Zuma hakuchukua hatua kali
si tu kwa polisi walioua, bali hata kwa kampuni hiyo ili kuwaridhisha
wazalendo wale waliokuwa wakipigania maslahi yao.
Mtu pekee aliyeonekana kuwalilia wafanyakazi wa
migodini, alikuwa Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa vijana wa chama
hicho, Julius Malema.
Hata hivyo, juhudi zake hazikufua dafu kwani hivi sasa ameshafukuzwa uanachama wa ANC.
Tukirudi kwa Mandela, pengine baada ya kutoka gerezani angeshika
msimamo kama wa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe wa kuwanyang’anya ardhi
Wazungu ili awagawie Waafrika, leo tungeona Afrika Kusini nyingine
kabisa.
Lakini inaonyesha alikata tamaa na kulegeza msimamo wake, ili awe huru na Wazungu wasibughudiwe.
Ni kweli tunamlilia Mandela, lakini hakumaliza kazi ya kuwakomboa Waafrika Kusini.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI