Kwa ufupi
Kusema kweli Mandela ni mtu wa aina yake…
alipitia mazingira magumu yaliyoambatana na mateso makubwa, lakini
pamoja na yote hayo, alisimama na kuhubiri umoja uliofanikisha kujenga
taifa la Afrika Kusini hadi leo
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim amesema katika kipindi
cha miaka saba alichofanya kazi na Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
aligundua kuwa ni mtu muungwana na mwenye hisia kubwa kuhusu ubinadamu.
Dk Salim alisema jana katika mahojiano maalumu
kuwa katika siku za mwanzo hakujiamini kufanya kazi na kiongozi huyo
ambaye anatambuliwa kama nuru ya dunia.
Alisema alikutana kwa mara ya kwanza na Mandela
Mjini Addis Ababa, Ethiopia mwaka 1990 alipokuwa mtendaji mkuu wa OAU
ambapo Mandela alikatiza ziara yake ya Tanzania Mei, 1990 na kwenda
Ethiopia kwa siku moja na kurejea tena nchini kuendelea na ziara yake.
“Kwanza niseme kwamba pamoja na kuwa wakati ule wa
ubaguzi wa rangi sisi sote tulikuwa tukishiriki kuupinga, lakini moyoni
mwangu sikuamini kama Mandela atakuja kutoka na hatimaye kuiunganisha
Afrika Kusini.
“Sasa alipoachiliwa tu, nakumbuka alikuja Addis
Ababa na ndipo nilipoanza kufanya naye kazi,” alisema Dk Salim, ambaye
aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Dk Salim alisema wakati wote, Mandela alionyesha
kuwa ni mtu mwenye kuzingatia misingi ya haki za binadamu na kutoa sura
ya matumaini kwa wale waliozungumza naye. “Nimebahatika kufanya naye
kazi kwa karibu sana… nakumbuka hata tulipokutana Tunisia kwa ajili ya
mkutano wa Afrika, wakati wote Mandela alionyesha sura ya kujali utu na
ubinadamu.
“Kusema kweli Mandela ni mtu wa aina yake…
alipitia mazingira magumu yaliyoambatana na mateso makubwa, lakini
pamoja na yote hayo, alisimama na kuhubiri umoja uliofanikisha kujenga
taifa la Afrika Kusini hadi leo,” alisema.
Alisema kitendo cha Mandela kukaa madarakani kwa
muhula mmoja na kisha kupisha uongozi kwa mwanasiasa mwingine, ni
fundisho kwa wanasiasa wa Afrika wanaopenda kung’ang’ania madaraka.
“Hii peke yake inatosha kutoa fundisho kwa
viongozi wa Afrika kwamba urais siyo wa milele, unaweza kufanya kazi
katika muda wako na kisha kuwapisha wengine, hivyo ndivyo Mandela
anavyotufundisha,” alisema.
Akizungumzia uhusiano baina ya Tanzania na Afrika
Kusini, Dk Salim alisema msimamo ulioonyeshwa na Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere aliyepinga hadharani utawala wa ubaguzi wa rangi
uliiponza Tanzania katika duru za kimataifa.
Alisema pamoja na kuwa uamuzi wa Tanzania ulikuwa
wa busara, ulikumbana na wingu la upinzani kutoka kwa baadhi ya mataifa
ambayo yalikuwa yakitetea siasa za ubaguzi wa rangi kwa masilahi
binafsi.
“Tusisahau hata sisi Tanzania tulikumbana na
misukosuko kutokana na msimamo wetu wa kupinga ubaguzi wa rangi… lakini
jambo la kushukuru ni kwamba matunda ya msimamo wetu sasa
yamejidhihirisha,” alisema Dk Salim.