Na Rashid Kejo,Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Jumatano,Novemba13 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Novemba13 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Azungumzia tathmini ya uongozi wake chini ya Serikali ya umoja wa kitaifa kwa miaka mitatu.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema
hakuna kiongozi yeyote wa Zanzibar mwenye mamlaka ya kuzungumzia msimamo
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusu masuala ya Katiba na
Muungano isipokuwa yeye na kwamba kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na
Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad ni zake binafsi au za
chama chake.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Zanzibar
jana juu ya tathmini ya uongozi wa Awamu ya Saba anayoiongoza, Dk Shein
alisema kuna changamoto kubwa za kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa
na kwamba jambo muhimu ni kuvumiliana.
Tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya, msimamo
wa Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, umekuwa ni kuundwa kwa
Serikali Tatu au ya Mkataba, ambao unapingana na ule wa CCM, wa kutaka
Serikali mbili kama ilivyo sasa.
Rasimu ya kwanza iliyotolewa na Tume ya
Marekebisho ya Sheria imependekeza kuwapo kwa Serikali Tatu, ya
Muungano, Tanganyika na Zanzibar.
“Serikali yangu haina msimamo wa jambo hilo. Kila
mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni yake, ninaweza kutoa msimamo kutokana
yaliofikiwa na uamuzi wa chama changu na kila mtu anaweza kufanya hivyo
na si kuisemea Zanzibar na wananachi wake.”
Alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa dhamira yake ya
kusimamia suala la mabadiliko ya Katiba na mchakato ulivyokwenda na sasa
taifa linaelekea kupata Bunge la Katiba kabla ya kufanyika kwa kura ya
maoni mwakani.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk
Shein alisema imefanikiwa kudumu kwa miaka mitatu sasa kutokana na
kuvumiliana na kufanya kazi kwa pamoja bila ya kutanguliza itikadi za
kisiasa. “Nchi nyingi zimejaribu hili zimeshindwa, lakini sisi
tumefanikiwa kwa sababu tunavumiliana. Hili linahitaji stahimili kubwa
vinginevyo tutagawana mbao na sitaki hili litokee kwenye uongozi wangu.”
Akizungumzia masuala ya Muungano, Dk Shein alisema
licha ya mchakato wa Katiba Mpya kuendelea, Serikali zote mbili
(Muungano na Zanzibar), zimeendelea kujadili masuala muhimu na
changamoto zilizopo na kusema siyo sahihi kubeza mgawo wa sasa wa mapato
ya Muungano ambao Zanzibar inapata asilimia 4.5.
“Jeshi la Wananchi na JKT (Jeshi la Kujenga Taifa)
wanatumia mabilioni mangapi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Elimu ya Juu
Sayansi na Teknolojia... Sisi (Zanzibar tunatoa ngapi?)”
Uchumi
Akizungumzia ukuaji wa uchumi katika kipindi cha
miaka mitatu ya uongozi wake, Dk Shein alisema kumekuwa na ongezeko
kubwa la ukusanyaji wa mapato akisema katika mwaka wa fedha wa 2010/11
Sh181.4 bilioni zilikusanywa na mwaka uliofuata wa 2011/12 makusanyo
yaliongezeka hadi kufikia Sh212 bilioni na mwaka wa fedha wa 2012/13
kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia Sh266. 2 bilioni.
Alisema uchumi wa Zanzibar umekuwa ukiongezeka
mwaka hadi mwaka. Alisema mwaka 2010 uchumi ulikua kwa asilimia 6.4,
mwaka 2011 asilimia 6.7, mwaka 2012 asilimia saba na mwaka huu
unatarajiwa kukua hadi kufikia asilimia 7.5.
SOMA ZAIDI HABARI HII: mwananchi
SOMA ZAIDI HABARI HII: mwananchi