Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Jumanne,Novemba19 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Novemba19 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Yakiri pia kuwa, yaliyosemwa na Maalim Seif Sharif Hamad ni mtazamo wake binafsi kama kiongozi wa kisiasa.
Zanzibar. Chama cha Wananchi
(CUF), kimesema kinaunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein kuwa yeye ndiye msemaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na
yaliyosemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ni
mtazamo wake binafsi kama kiongozi wa kisiasa.
Msimamo huo umewekwa wazi na Naibu Katibu Mkuu wa
CUF Zanzibar, Hamad Masoud Hamad katika mahojiano maalumu na Mwananchi,
Mtendeni mjini Unguja jana.
Hatua hiyo ya Hamad imekuja siku chache baada ya
Rais wa Zanzibar, Dk Shein kuwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna
mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar isipokuwa yeye.
Hamad alisema, Makamu wa Kwanza wa Rais
anapozungumza na kutoa msimamo wake juu ya mambo ya muungano na siasa,
hufanya hivyo kama kiongozi wa CUF ndiyo maana hutumia jukwaa la kisiasa
kuzungumza na wafuasi pamoja na wanachama wake.
“Rais wa Zanzibar ndiye msemaji wa Serikali na
kiongozi mkuu, lakini Makamu wa Kwanza anapozungumza katika jukwaa na
wafuasi wake, hutoa msimamo wa chama chake kama kiongozi wa juu,”
alisema Hamad.
Maelezo hayo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,
yamekuja kufuatia tofauti ya kimtazamo na kimsimamo iliyojitokeza
kuhusu ni nani mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar.
Akizungumzia tathmini yake ya miaka mitatu ya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Hamad alisema kimsingi
imefanikiwa kudumisha amani na kuondoa mivutano ya kisiasa na malumbano
yaliyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar.
Hata hivyo, alisema muundo wa SUK unahitaji
kuangaliwa upya kwa ngazi ya watendaji na viongozi wa kisiasa ili kuleta
taswira ya umoja wa kitaifa.
Mawaziri na manaibu wake wanafanya kazi kwa
ushirikiano, lakini watendaji wakuu wa SUK bado wameshindwa kutekeleza
majukumu yao na kuendeleza baadhi ya vitendo vinavyowanyima haki
wananchi.
Alisema haikuwa mwafaka muundo SUK kuhusisha
mawaziri na manaibu wake bila ya kuangalia nafasi nyingine za watendaji
wakuu wa Serikali wakati wa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984.
Alisema pamoja na rais kuzungumzia mwelekeo wa kuimarika na kukua kwa
uchumi wa Zanzibar bado hali ya vipato kwa
wananchi wa kawaida ni duni kutokana na kuanguka kwa sekta ya viwanda na
kuzorota kwa uzalishaji wa ndani.
Hamad alisema sekta za uwekezaji, viwanda, mifugo na uvuvi lazima zipewe kipaumbele ili lengo la kuwapatia maisha bora wananchi lifanikiwe.
SOURCE: MWANANCHI
Hamad alisema sekta za uwekezaji, viwanda, mifugo na uvuvi lazima zipewe kipaumbele ili lengo la kuwapatia maisha bora wananchi lifanikiwe.
SOURCE: MWANANCHI