Wednesday 13 November 2013

Tisa mbaroni wakidaiwa kumjeruhi Dk Mvungi


Na Raymond Kaminyoge,Mwananchi

Posted  Jumanne,Novemba12  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Polisi wanadai wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kutokana na ushirikiano wa wananchi



Dar es Salaam.Polisi imekamata watu tisa wanaotuhumiwa kumvamia, kumjeruhi kisha kumwibia Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.
Dk Mvungi alijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga kichwani Novemba 3, mwaka huu nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kulazwa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Milpark, Johannesbarg, Afrika Kusini.
Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova walifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Kova alisema miongoni mwa watuhumiwa hao, wawili ni madereva wa bodaboda na mmoja ni fundi ujenzi ambaye aliwahi kujenga nyumba ya Dk Mvungi.
Alisema baada ya kukamatwa, mmoja alikutwa na simu iliyoibiwa nyumbani kwa Dk Mvungi wakati wa tukio hilo.
“Baada ya kubanwa zaidi, walikwenda kuonyesha mapanga matano na kigoda ambavyo vilitumika kujeruhi siku ya tukio,” alisema Kova.
Alisema asilimia 80 ya watuhumiwa hao wamekamatwa kwa ushirikiano wa familia ya Dk Mvungi na wananchi.
Kamanda Kova alisema watu hao watafikishwa mahakamani wakati wowote, baada ya kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Alisema upelelezi unaonyesha huo ni ujambazi wa kawaida wenye kuhitaji fedha na mali na kwamba, hauna uhusiano wowote na masuala ya siasa.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi aliwapongeza polisi kwa kufanikishwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Dk Nchimbi alisema upelelezi unaendelea kuwatafuta wengine na kompyuta mpakato (Laptop), ambayo haijapatikana.
“Tunaendelea kuwasaka waliobaki ili waweze kushtakiwa kwa makosa waliyoyafanya, ninashukuru polisi kwa weledi wao hadi kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao,” alisema Dk Nchimbi.
Mkutano huo ulifanyika ofisini kwa waziri badala ya kufanyika kwa Kamanda Kova, ambako mikutano ya ufafanuzi wa masuala ya uhalifu hufanyika.

SOMA ZAIDI: Mwananchi