Saturday 9 November 2013

Mapigano yautingisha mji wa Tripoli


Makundi ya wanamgambo yameshambuliana kwa saa kadhaa kwa kutumia mizinga ya kutungulia ndege na maguruneti katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, hapo Alhamisi (07.11.2013) na kuuwa mtu mmoja na kujeruhi wengine 12 .
Makundi wa wanamgambo wa Libya. Makundi wa wanamgambo wa Libya.
Kuzuka huko kwa mara ya pili kwa mapigano ya mitaani katika kipindi cha siku chache kunaonyesha jinsi serikali ilivyo kwenye kipindi kigumu kujaribu kuwadhibiti wanamgambo ambao walisaidia kumpinduwa aliyekuwa kiongozi wa Libya, hayati Muammar Gaddafi, miaka miwili iliopita lakini wameendelea kushikilia silaha zao kufuatia uasi wao ulioungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Duru za usalama zimeliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, kwamba kundi la wapiganaji lililokuwa na silaha nzito kutoka mji wa kati wa Misrata liliingia katika mji mkuu wa nchi hiyo wakati wa jioni kulipiza kisasi kwa mauaji ya mmoja wa wapiganaji wao katika mapigano mengine madogo yaliyotokea Tripoli hapo Jumanne.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo malori aina ya Toyota yakiwa na mizinga ya kutungulia ndege yaliwasili sehemu mbalimbali za Tripoli na kufyetuwa risasi wakati yakijaribu kukivamia kitongoji cha mashariki cha Surq al-Juma. Watu waliokuwa nje wakijipatia mlo wa jioni kwenye mikahawa walitimka kutafuta usalama wakati madereva waliyatelekeza magari yao.
Mapigano yazusha taharuki
Vikosi vya usalama vya Libya. 
Vikosi vya usalama vya Libya.
Kwa muijbu wa Reuters mapigano hayo ambayo ni makali kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miezi kadhaa katika mji mkuu wa nchi hiyo.yameuwa mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 12 lakini kituo cha televisheni cha al-Arabiya chenye makao yake Dubai kimesema watu wawili wameuwawa na 21 kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Radisson Blu, mojawapo ya hoteli nzuri kabisa za Tripoli, ilibidi kuwahamisha baadhi ya wageni wake waliokuwa na hofu baada ya madirisha katika eneo la mapokezi kuvunjwa kutokana na risasi zilizokwenda kombo.
Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan ana kibaruwa kigumu cha kuwadhibiti wanamgambo.  
Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan ana kibaruwa kigumu cha kuwadhibiti wanamgambo.
 
Makundi ya wanamgambo yanayopingana yalivurumisha maguruneti kwa kutumia maroketi kwa washambuliaji kutoka kwenye daraja moja. Milio mizito ya risasi pia ilisikika takriban katika vitongoji vengine vitatu vya mji mkuu huo karibu na wizara ya mambo ya nje, jengo la televisheni ya taifa na ofisi za ubalozi. Wapiganaji walionekana wakipakia mizinga ya kutungulia ndege kwenye malori karibu na wizara hiyo.

Mzozo huo ulianza hapo Jumanne wakati makundi hasimu ya wapiganaji yalipopambana kwa takriban saa nne. Watu watatu walijeruhiwa na mmoja ambaye ni kiongozi wa wanamgambo wa Misrata alifariki baadaye na kusababisha shambulio hilo la kulipiza kisasi wakati habari za kifo chake zilipoanza kuzagaa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Wanamgambo ni tatizo kwa serikali
 Makundi ya wapiganaji wakati wa uasi uliompinduwa Gaddafi 2011. Makundi ya wapiganaji wakati wa uasi uliompinduwa Gaddafi 2011.
Juu ya kwamba ofisi za ubalozi na wizara zimewahi kushambuliwa huko nyuma mjini Tripoli, kwa ujumla mji mkuu huo umenusurika na ghasia za matumizi ya nguvu yaliyoshuhudiwa katika mji wa mashariki wa Benghazi ambapo mauaji na miripuko ya mabomu hutokea takriban kila siku.
Serikali ya Libya inaiwia vigumu kuwadhibiti wapiganaji wa zamani na wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu katika nchi ambapo silaha zimezagaa ovyo.

Waziri Mkuu Ali Zeidan amekuwa akijaribu kuwajumuisha pamoja na silaha zao wanamgambo waliosaidia kumpinduwa Gaddafi wakati wa uasi katika jeshi na polisi ya taifa. Lakini kiutendaji wengi wa wanamgambo hao wanaendelea kuripoti kwa makamanda wao wenyewe au kwa makabila yao.

Migomo na maandamano ya wanamgambo wenye silaha na wapiganaji wa kikabila wenye kudai malipo au haki za kisiasa pia imesababisha kuzuwiwa kwa sehemu kubwa ya uzalishaji wa mafuta kwa miezi kadhaa kutoka katika nchi hiyo mwanachana wa nchi zinazosafirisha nje mafuta kwa wingi duniani, OPEC, na kuinyima serikali ya nchi hiyo chanzo chake kikuu cha mapato.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

SOURCE: D.W