Na Herieth Makwetta, Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba15 2013 saa 14:16 PM
Posted Ijumaa,Novemba15 2013 saa 14:16 PM
Kwa ufupi
- Dawa zinazoleta madhara si zile zinazotumika mara kwa mara, lakini kwa bahati mbaya wapo wanawake wanajigundua kwamba wamebeba ujauzito na hawa wanajikuta wakitumia dawa hizo ambazo mwishowe zinawaletea madhara katika ujauzito na hawezi kugundua mpaka atakapojifungua japokuwa wapo ambao mimba zao huharibika,” anasema Dk Masawe.
Hili ni tatizo kubwa na ambalo linazidi kujitokeza, lakini ambalo kama litaachwa liendelee lilivyo litaiangamiza jamii
Kujifungua mtoto asiyetimia viungo vyake vyote,
mwenye matatizo ya viungo au viungo visivyo vya kawaida hutokana na
vitendo au matukio hatarishi yaliyofanyika katika mwili wa mama, kuanzia
siku moja hadi miezi mitatu tangu mimba kutungwa.
Kitu chochote ambacho ni sumu, dawa, kemikali,
mionzi na mgawanyiko wa seli wakati wa uumbaji wa mtoto zimetajwa kuwa
sababu kuu za tatizo hilo.
Madaktari mbalimbali waliozungumza na gazeti hili
wametoa sababu mbalimbali huku wakisisitiza kuwa mpaka sasa dunia bado
haijapata sababu maalumu inayosababisha matukio kama hayo kutokea,
lakini zipo sababu zinazoaminika kuwa chanzo cha hayo.
Dk Cyriel Massawe Daktari Bingwa wa Magonjwa ya
Wanawake na Afya ya Uzazi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anasema
mwanamke mjamzito hashauriwi kunywa dawa ya aina yoyote ile kama
hajapata ushauri kutoka kwa daktari ni kutokana na baadhi ya dawa
kuainishwa kwamba huenda yanaweza kuchangia kuvuruga uumbaji siku za
mwanzo za ujauzito.
Anaongeza: “Hali hiyo husababisha seli kushindwa
kugawanyika vizuri kila moja kwenda kufanya kazi ile inayokusudiwa
katika uumbaji wa mtoto hapo ndipo tatizo huanza kutokea.”
Anatoa mfano kuwa kuwa tatizo kubwa linalowapata
watoto walioungana pia linaweza kusababishwa na kutogawanyika vizuri kwa
seli wakati wa utungwaji wa pacha.
“Mfano mzuri ni watoto walioungana, hawa ni wale
wa mfuko mmoja. Yai moja linapogawanyika mara mbili ni nadra kutokea
kosa, lakini katika uumbaji seli zikishindwa kugawanyika vizuri na
kufanya uumbaji uliotimifu hapo pacha wataungana matumbo, migongo,
vichwa na sehemu zingine za mwili au mmoja asitimie kama ilivyotokea
hivi karibuni,” anasema.
Anasema iwapo mama hakutumia vidonge au dawa za
aina yoyote basi yawezekana tatizo ni la kiasili na hali hii hutokea
katika hatua za mwanzo wa ujauzito na hata mwanamke akienda hospitali
huambiwa kwamba atajifungua watoto mapacha lakini hali huwa ndivyo
sivyo.
Anakiri kwamba kuna idadi kubwa ya wanawake ambao
hutumia dawa miezi ya mwanzo kabla ya kujigundua kwamba ameshika mimba
huathirika zaidi.
“Dawa zinazoleta madhara si zile zinazotumika mara
kwa mara, lakini kwa bahati mbaya wapo wanawake wanajigundua kwamba
wamebeba ujauzito na hawa wanajikuta wakitumia dawa hizo ambazo mwishowe
zinawaletea madhara katika ujauzito na hawezi kugundua mpaka
atakapojifungua japokuwa wapo ambao mimba zao huharibika,” anasema Dk
Masawe.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika
Hospitali ya Muhimbili, Dk Zaitun Bokhary anasema mama mjamzito hutakiwa
kutumia dawa za ‘folic acid’ kabla na baada ya ujauzito ili kuepuka
kujifungua mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa (Hydrocephalus) na
Mgongo wazi (spina bifida).
SOMA ZAIDI: Dawa--kemikalI
SOMA ZAIDI: Dawa--kemikalI