Na Habel Chidawali, Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 23:26 PM
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 23:26 PM
Kwa ufupi
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali
na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba
kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi
kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei
magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana ameangukia pua baada ya Bunge
kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya
Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa
habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Kadhalika Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana
na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika
kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari,
badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa
Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge
alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo
haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na
hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
“Sitegemei magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya
taifa. Walio wangu watanikataa na wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa
ajili ya taifa sitamwangukia mtu yeyote miguuni,” alisema Werema, kauli
ambayo iliwachefua wabunge.
Hata hivyo, jana baada ya Spika kuwahoji wabunge
na kukataa mapendekezo ya Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka
hivyo alisimama na kutaka Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu
hicho.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande
wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina
mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema Werema.
Hata hivyo, Spika alikataa na kusema: “Kama kuna
eneo ambalo tumefanyia utani Serikali ni katika eneo hili, naomba
Serikali mtuletee muswada bungeni siyo porojo za maneno.”
Katika marekebisho hayo, Serikali ilikuwa
ikipendekeza katika sheria hiyo mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa
waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya kuandika habari za
uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi kiasi kisichozidi Sh5 milioni.
Hata hivyo, wakati Bunge lilipoketi kama kamati
wabunge walikataa kupitisha marekebisho hayo ambayo yalikuwa sehemu ya
Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2013, wakisisitiza
kwamba Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria ya habari.
Moto wa wabunge
Moto wa wabunge hao uliwashwa na Mbunge wa Kigoma
Mjini, Peter Serukamba (CCM), ambaye alipendekeza sehemu ya nane ya
muswada iliyokuwa na vipengele vya 39, 40 na 41 iondolewe ili
kuishinikiza Serikali kupeleka bungeni sheria nzima inayohusu vyombo vya
habari.
Mbunge huyo alisema kuwa sehemu hiyo na vipengele
vyake kama vingepitishwa vingeifanya Serikali kuwa kimya na kushindwa
kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari kama ilivyoahidi
kwa muda mrefu.
“Mimi nimekuwa mbunge hapa huu mwaka wa nane, lakini kila siku
Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuleta muswada huo. Kila mara
tunaambiwa kuwa utaletwa, lakini hauletwi sasa mpango wa kuleta vitu
nusu-nusu haufai,” alisema Selukamba.
Mbunge huyo alilalamika kuwa baadhi ya viongozi
walishapendekeza kuwa watu wote wanaopigia kelele sheria hiyo waangaliwe
hati zao za kusafiria kwa madai kuwa zinatia shaka jambo alilosema kuwa
yuko tayari kufanya hivyo ilimradi ahakikishe anasimamia kweli.
Jenista Mhagama
Baada ya Serukamba kutoa hoja hiyo, wabunge wengi
walisimama kumuunga mkono ndipo akapewa nafasi ya kuchangia Mbunge wa
Peramiho, Jenista Mhagama ambaye pia alisisitiza kwamba lazima sheria ya
vyombo vya habari ifikishwe bungeni.
Mhagama alisema kutokana na kigugumizi cha
Serikali, tayari kuna gharama ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kutumwa India kwa ajili
kujifunza mambo mbalimbali yanayoendana na sheria hiyo, lakini bado hata
hivyo haijasaidia kitu.
Mhagama na Serukamba tangu wakati mjadala wa
sheria ulipoanza juzi walisisitiza kuunga mkono kuletwa kwa sheria ya
vyombo vya habari. Serukamba alisema akichangia muswada huo alihoji:
“Kuna nini hapa? Maana hii tabia ya kuchomoa vipande vipande na
kutuletea hapa haina tija.”
“Tukatae vipengele hivi, nawaomba wabunge wenzangu
mniunge mkono katika hili na ikiwa tutavikataa vipengele hivi Serikali
italeta sheria nzima hapa, mimi sina tatizo na adhabu hata ingekuwa mara
tatu, lakini tuleteeni sheria nzima, mnaogopa nini?” alihoji Serukamba.
Mhagama yeye alisema kwa muda mrefu wadau wa
vyombo vya habari wamelalamikia kuwapo kwa sheria hiyo itakayolinda
tasnia ya habari, lakini Serikali mara zote imekuwa ikipiga danadana.
“Kwa nini Serikali inachelewa kuwasilisha muswada
wa sheria bungeni? Hebu sasa tukae na wadau tukubaliane mambo ya msingi,
tuwe na sheria ili kuinusuru tasnia ya habari, sheria itasaidia
kuwadhibiti makanjanja, wapo watu wanaoidhalilisha tasnia ya habari bila
sababu za msingi,” alisema.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa bungeni jana
ilisema Muswada wa Vyombo vya Habari uko tayari na kwamba wakati wowote
unaweza kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa kuwa sheria.
Wabunge wengine
Vipengele hivyo vilipingwa na wabunge wengi tangu
mwanzo, akianza Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) pamoja na Wabunge wa Viti Maalumu,
Ester Bulaya na Martha Mlata (CCM).
Tundu Lissu
Katika maoni ya Kambi ya Upinzani, Lissu alisema
mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Magazeti hayana msingi kwa
sababu; hakuna ushahidi wowote kwamba adhabu zilizoko katika vifungu vya
36(1) na 37(1)(b) zinazopendekezwa kuongezwa zimeshindwa kudhibiti
makosa ya uchochezi.
“Tangu sheria hiyo ilipotungwa miaka zaidi ya 37
iliyopita, hakuna mwandishi wa habari au mchapishaji wa gazeti lolote
ambaye amewahi kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ya makosa
hayo. Badala ya kuwapeleka wakosaji mahakamani, Serikali imejenga
utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi habari,” alisema
Lissu na kuongeza:
“Hii peke yake inathibitisha hoja kwamba sheria
ilitungwa kwa malengo ya kisiasa ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa
Serikali na watawala na si kuzuia makosa ya jinai”.
Bulaya
Bulaya kwa upande wake alisema, Serikali inafanya
makosa makubwa kwa kutaka kuwaadhibu waandishi wa habari, pasipo kujenga
msingi imara wa uandishi wenyewe kama taaluma katika nchi.
“Kwa nini Serikali inawaza adhabu kali tu?
Kuongeza faini kutoka Sh15,000 hadi Sh5 milioni, hapo kuna nini, lazima
tujiulize maana kwa kufanya hivi tunawaumiza waandishi wa habari ambao
wengi wao hawana uwezo wa kulipa hizo fedha,”alisema Bulaya na kuongeza:
“Sheria nzima ikiletwa hapa, tutakuwa na uwezo wa
kuangalia mambo mengi yakiwamo masilahi ya waandishi wa habari, lakini
pia kuwabana watu ambao hawataki kutoa habari ila wanasubiri waandikwe
ndipo wajitokeze kulalamika.”
Mlata
Naye Martha Mlata katika mchango wake alisema
wanasiasa ndio wamekuwa wakiwatumia waandishi wa habari na kwamba faini
iliyowekwa na Serikali ni mbaya kwani ni mzigo kwa waandishi wa habari.
“Na sisi wanasiasa tuache kuwatumia waandishi wa
habari na ninyi waandishi wa habari msikubali kutumiwa na wanasiasa,
tukitaka kuwatumia mkatae na mfanye kazi kwa kumwogopa Mungu kila mtu
kwa dini yake,” alisema Mlata.
Walioishabikia sheria
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, Pindi Chana na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba
(CCM) walishabikia kuwapo kwa adhabu kali kwa waandishi wa habari, kwa
maelezo kwamba wamekuwa wakitumiwa kuwachafua watu.
Chana alisema: “Katika malengo ya Serikali
ilipoleta marekebisho haya wametuambia kwamba malengo yake ni kuongeza
adhabu ili kulinda matumizi ya lugha ya matusi, makosa haya yanajumuisha
matumizi ya lugha za uchochezi zinazoweza kusababisha machafuko katika
jamii.
“Ni ukweli kila Mtanzania anafahamu kuwa magazeti
yetu kuna wakati yanatumika na kikundi fulani, kuwabeba kikundi fulani
au mtu fulani na kuangamiza mtu fulani au kikundi fulani.
Aliliomba Bunge litoe majibu pale magazeti
yanapomdhalilisha mtu kwa kuandika jambo ambalo halina ushahidi wa
kimahakama. “Nawauliza wahariri, pale magazeti yanapotumika kuchochea
ndivyo sivyo tufanyaje? Je, huo ndio uhuru wa habari?” alihoji.
Nchemba kwa upande wake alisema hakuna haja ya
kusubiri sheria mpya na
kwamba kusubiri kunaweza kutoa mwanya kwa vyombo vya habari kuitumbukiza nchi kwenye machafuko.
SOURCE: MWANANCHI
kwamba kusubiri kunaweza kutoa mwanya kwa vyombo vya habari kuitumbukiza nchi kwenye machafuko.
SOURCE: MWANANCHI