Na Mwandishi wetu,Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Kibanda aliamua kutoa asilimia 10 ya fedha alizopewa kanisani wakati nusu ya fedha itakazobaki itakwenda kwa mke wa Mwangosi.
Mwanza.Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari
(2006), Absalom Kibanda aliangua kilio baada ya kutangazwa kuwa mshindi
wa tuzo ya Uandishi wa Habari Uliotukuka ya Daudi Mwangosi. Pia aliamua
kutoa sehemu ya fedha za zawadi kwa familia ya marehemu Daudi Mwangosi.
Pamoja na tuzo hiyo, Kibanda pia alipata zawadi ya
fedha taslimu ya kiasi cha Sh10 milioni kwenye shughuli hiyo
iliyoandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Tuzo hiyo ilianzishwa ikiwa ni heshima kwa
Mwandishi wa habari wa zamani wa Kituo cha Televisheni cha Channel 10,
Daudi Mwangosi, ambaye aliuawa Septemba 2, mwaka 2012 na askari polisi
waliokuwa wanatawanya wafuasi wa Chadema huko Mafinga mkoani Iringa.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hizo jana,
Kibanda alisema kitendo cha kukabidhiwa tuzo hiyo ni uthibitisho kuwa
aliteswa na kujeruhiwa kutokana na masuala ya kikazi na si vinginevyo.
“Nawashukuru majaji waliotambua na kunichagua
kupata tuzo hii ambayo ni ushahidi tosha kuwa tukio lililonipata pasipo
shaka linatokana na kazi yangu ya uandishi.
Uchunguzi wa jambo hili umekuwa kimya hadi leo na
badala yake maneno yamekuwa yakisambazwa kwenye balozi kwamba niliteswa
kwa mambo binafsi,” alisema Kibanda, baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Tido Mhando.
”Ifike wakati waandishi wote tufikirie kwa makini
kuwa viongozi wa siasa waliopo madarakani na wengine walishatoka, ndiyo
wamekuwa wakitutangaza kama wasaliti, wachochezi na kama maadui na ndiyo
maana wanapeleka miswada kandamizi bungeni wakati wamekuwa wakitutumia
katika mambo yao mengi, tujiulize kama tunajitendea haki,” alisisitiza.
Kibanda alisema pia kifo cha Mwangosi na kipigo
alichopata yeye na Said Kubenea kinapaswa kuwafanya waandishi kuchukulia
kama sababu kubwa ya kuwafanya wasonge mbele na kuendelea kutekeleza
majukumu yao huku wakiweka pembeni maumivu na mateso waliyoyashuhudia
kwa wenzao.
Kibanda aliamua kutoa asilimia 10 ya fedha alizopewa kanisani wakati nusu ya fedha itakazobaki itakwenda kwa mke wa Mwangosi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited, Tido Mhando, alisema kuwapo kwa
matukio ya kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania Mwanahalisi
pamoja na kujeruhiwa na kuuawa kwa waandishi, ni kielelezo cha kuminywa
kwa uhuru wa habari.
Alisema hata hivyo matukio haya hayapaswi kuwavunja moyo waandishi wa habari katika kutimiza wajibu wao.
Pia aliwataka kusimamia taaluma yao na maadili ya
kazi zao ikiwa ni pamoja na kuwajibika katika uandishi huku wakizingatia
weledi. Mhando aliwataka waandishi wa habari kutokubali kutumiwa na
wanasiasa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI