Na Hamida Shariff,Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Novemba8 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kutokana na kuitishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kupitiwa upya ikiwa ni utaratibu usiopingika .
Morogoro. Kesi yenye mashtaka
matatu inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
nchini,Sheikh Ponda Issa Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani
hapa,imeshindwa kusikilizwa baada ya jalada halisi la kesi hiyo
kuitishwa kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya
kulipitia upya.
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo mapema
asubuhi kwa kutumia usafiri wa basi maalumu la magereza na safari hii
kesi yake ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,Mary Moyo baada ya
hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo tangu awali, Richard Kabate
kuhamishiwa mkoani Dodoma.
Akitoa maelezo ya kesi hiyo,Hakimu Moyo alisema
jalada halisi la kesi hiyo liliitishwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam Oktoba 15, mwaka huu kwa ajili ya mapitio na kwamba Mahakama Kuu
inamamlaka ya kisheria ya kuitisha jalada lolote na kuongeza kuwa kesi
hiyo haitaweza kusikilizwa hadi jalada hilo litakaporudi.
Hakimu Moyo alisema kwa sasa kesi hiyo itakuwa
ikitajwa tu na suala la mshtakiwa kuletwa ama kutoletwa mahakamani liko
chini ya magereza kwani dhamana ya mshtakiwa huyo imefungwa,hivyo
ataendelea kuwapo magereza hadi Novemba 21,mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Mapema baada ya kufikishwa mahakamani hapo, Hakimu
Moyo alimuuliza Sheikh Ponda kama ana taarifa zozote kuhusu kutokufika
kwa mawakili wake watatu mahakamani hapo ambao ni Batholomew Tharimo,
Ignas Punge na Juma Nassor hata hivyo, Sheikh Ponda alidai kuwa hana
taarifa zozote kuhusu kutofika kwa mawakili wake.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na
Wakili wa Serikali, Sunday Hiela ulidai uko tayari kutoa ushahidi ambao
ungeanza na askari namba F4949 DC Kingazi wa Kituo Kikuu cha Polisi.
Hata hivyo, shahidi huyo hakuweza kutoa ushahidi wake kutokana na jalada
halisi la kesi hiyo kutokuwapo mahakamani hapo kwa sababu zilizotolewa
awali.
Pamoja na kutokufika kwa mawakili wote watatu pia idadi ya wafuasi wa Shekh Ponda ilionekana kuwa ndogo.
Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kutokutii
amri halali ya mahakama,kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini
na kushawishi watu,makosa hayo kwa pamoja anadaiwa kuyatenda Agosti 10,
mwaka huu.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI