Na Wandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatano,Novemba13 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Novemba13 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine
zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR-
Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo
Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika
Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka
Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark,
Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni
kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana
(saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.
Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo
akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo
chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba
walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.
“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya
kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji
Warioba na kuongeza:
“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini
pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana.
Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu
aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo
moyoni mwake”.
Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi
aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa
katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati
katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu
Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi
hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika
majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba),
yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. Kweli
tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria,
hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii.
Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.
Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine
zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR-
Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo
Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi
saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki.
Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu
familia,”alisema Mbatia.
Taarifa ya Tume
Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa
taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko
makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa
Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika
Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini
amefariki dunia.”
Taarifa iliyotolewa Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk
Mvungi alifariki dunia saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.
Iliendelea kusema taarifa hiyo kuwa taratibu za
kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini kuja nchini kwa
maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini baada
ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana walipovamiwa nyumbani kwake
Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu.
Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013
kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba
ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa
tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine
za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa
Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu sana, kwani ni
mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo na dira yake.
“Tumepata pigo kubwa sana kwani tumempoteza mtu
ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na aliyafahamu
vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri aliyebobea katika
constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi walimpenda
sana,”alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi ambaye alikuwa
naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu alipokwenda
kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani kwake (kwa
Mahalu).
“Wakati huo nilikuwa nikifundisha Ujerumani,
alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na alifikia nyumbani
kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa kazi, kweli
tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.
Chadema, CCM wamlilia
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba taifa
limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele katika
kudai Katiba Mpya.
“Tumepokea taarifa za kifo hiki kwa mshtuko
mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Dk Mvungi,
tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,” alisema Mbowe.
SOURCE: MWANANCHI
Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM), Mwigulu Nchemba alisema
amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kutoa pole kwa
Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya kazi muhimu ya
kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Alisema amekufa wakati mchango na mawazo yake
yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali iwasake wahalifu
hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema
ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho kimetokea wakati Dk Mvungi
akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu
aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu na kwamba hali
ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa kitaifa.“Tunahitaji kuangalia
kiini cha uhalifu hapa nchini, watu wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni
lazima tuchukue hatua,” alisema.
Mitandao ya kijamii
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake,
mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii Forum ilikuwa
ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.
Hussein Bashe kwenye ukurasa wake wa Facebook
aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More (hatunaye tena), taarifa
zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark, ndugu yetu Mvungi amefariki,
mnamo saa tisa na nusu.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya jukumu zito kwa ajili ya
taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu atalipia uhalifu huu, poleni
Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni NCCR-Mageuzi.”
Mtu mwingine aliyechangia suala hilo kwenye
mtandao wa Jamiiforum ni yule aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi
aliyeandika kuwa, RIP Dr. Mvungi... Mungu akulaze mahala pema peponi.
Japo umeondoka kivuli chako kitaishi... Naipa pole familia yako, maisha
yetu kwa sasa nchini ni kudra za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe...
wengine wamepona lakini wewe umeondoka.”