Saturday 2 November 2013

NEMC, TCRA mnakiona kiama cha simu za mikononi!

2nd November 2013
Simu za Mkonini
Simu  ya mkononi ilivumbuliwa  mwaka 1973 na timu ya wataalam wafanyakazi wa kampuni ya Motorola wakiongozwa na Dk. Martin Cooper.  Mtaalamu huyu aliitumia simu ya mkononi kwa mara ya kwanza Aprili 1973. Matumizi hayo yalifungua mlango wa bidhaa hizo sehemu mbalimbali duniani.

Miaka ya hivi karibuni matumizi ya simu hizo yamekuwa makubwa  hasa kwa mataifa yanayoendelea pamoja na Tanzania. Ongezeko la matumizi ya simu linamaanisha wingi wa taka zitokanazo na simu zinapomaliza muda wa  matumizi  hivyo kuchangia katika uchafuzi wa mazingira na kuleta changamoto  ya namna ya kutupa mabaki ya simu muda unapomalizika.

Kwa kuangalia ukubwa wa tatizo hili na athari za haraka zinazotishia bayoanuwai, Mhadhiri Mwandamizi wa Kemia na Mkuu wa Idara ya Kemia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Egid Mubofu, anachambua madhara ya simu na viambata vyake na kupendekeza mbinu za kukabiliana nazo ili kuepusha kitisho kikubwa kinachokuja.
Swali: Betri za simu za mikononi zinazotupwa kila mahali  ni nini athari zake?

Jibu: Simu hizi zinatupwa ovyo pasipo na utaratibu maalum. Ukiacha matatizo ya kimazingira yanatokanayo na simu yenyewe, pia betri zake zinatupwa bila mpangilio. Kwa wastani simu ya mkononi  kwa asilimia 45 imeundwa kwa  plastiki, asilimia  40 ni nyaya, asilimia nne ni  ute mkavu  na zilizobakia  11 ni madini ya metali mbalimbali.

Madini mengi katika simu hizi yana sumu kali mfano ni  risasi na mengine yasiyo na majina ya Kiswahili kama   brominated flame –retardants, beryllium, chromium  arsenic, antimony na cadmium.

Betrii ya simu imeundwa mahususi kuweza kubadilisha nguvu ya kikemikali iliyomo ndani yake na kuifanya iwe nguvu ya  umeme. Nguvu yake  hutegemea kikemikali iliyomo ndani yake ambayo ikiwa hasi (-) ndipo betri inaweza kufua umeme na pale inapofikia sifuri haina uwezo wa kufua umeme hivyo simu inazimika.

Katika hali hii kinachotumiwa ni  nguvu ya nje ya betri kuirudishia  uwezo wa kufua umeme kwa hiyo betri huchajiwa ili kuipa tena nguvu ya kuzalisha umeme huo, ndiyo maana zinachajiwa.

Namna ya kutupa betri ya simu ni changamoto kubwa kwani  zina metali nzito  kama  mercury, lead, cadmium na nickel na kwa hiyo utupaji holela unaharibu mazingira na kutishia usalama wa bayoanuia.

Mathalani kama  betri hizi zikichomwa  baadhi ya metali zinaweza kuingia kwenye hewa, nyingine zilizoko kwenye majivu  huzama  ardhini na  kwenye mazingira. Uharibifu huu wa mazingira unaweza kusababisha magonjwa mbalimbali yatokanayo na athari za metali hizi zinazokwenda moja kwa moja kwenye  mimea, wanyama na viumbe wengine.

Kimsingi suala hili la utupaji betri linatakiwa kutazamwa kwa upana na kwa makini ikiwezekana Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi Mazingira (Nemc), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na wadau wengine waweke taratibu za kudhibiti utupaji wa betri na simu zilizoisha muda wake ili kuondoa hatari ya  uchafu wa mazingira.

Kadhalika zitumike sheria za kimataifa kama vile The Basel Convention, ambayo Tanzania imeridhia ili  kudhibiti utupaji wa simu na viambata vyake.
Chanzo cha  maradhi:
Betri za zina metali ya risasi ‘lead’ ambayo ipo katika kundi hatarishi la kemikali zinazojikusanya kwenye seli za viumbe kidogo kidogo  hatmaye  kuleta madhara makubwa.
Kwa vile risasi iko kwenye orodha ya kemikali hatarishi persistent bioaccumulative toxins (PBTs) na inajulikana kuwa ni sumu mbaya sana kwa wanadamu, viumbe wengine na mazingira kwa ujumla.

Metali hii ina athari kubwa kwani inaweza kuharibu mfumo mzima wa kiikolojia na kwa  binadamu, baadhi ya athari zake  ni kwenye mfumo wa mishipa ya fahamu ambapo  inaharibu mishipa mkuu ya neva,  inaharibu kinga ya mwili, figo, inadumuza ukuaji wa ubongo kwa watoto na hivyo kupunguza uwezo wao wa kuelewa na akili kufanyakazi ipasavyo inaweza kusababisha saratani na madhara mengine mengi .
Sumu kujikusanya na kuishi  mwiilini:

Katika simu ya mkononi  vizuio vya moto ‘brominated flame retardants (BFRs)’ hupatikana katika plastiki ya jumba la simu ambayo Watanzania wengi hulifahamu kama  ‘hauzing’ ili kuzuia kuungua simu endapo itashika moto.

Aina mbalimbali ya BFRs zinazotumika ni  malighafi za ‘polymeric  zenye  madhara makubwa ya kiafya kwa binadamu  na mazingira. Tafiti zinaonyesha kuwa hizi BFRs, polymeric ni sumu zinazojikusanya kwenye mfumo wa viumbe hai na kukaa muda mrefu hivyo simu za mikononi kutupwa kwenye madampo kusogeza hatari hiyo kwa viumbe hai wanaoishi karibu .

Baadhi ya hizi kemikali kama vile Polybrominated diphenyl zinahusishwa na uwezekano wa kusababisha saratani, kuharibu maini, mfumo wa kinga, kusababisha tatizo la tezi la shingo na matatizo mengine ya mfumo wa mwili wa binadamu.
Mabaka/makovu kwenye mapafu:

Simu ya mkononi  pamoja na umuhimu wake imetengenezwa kwa sumu kali iliyo ndani  ya madini  ya beryllium . Sumu hii mara nyingi inakuwa katika hali mchanganyiko na metali ya shaba ‘beryllium-copper alloy’ ili kuongeza uimara na mnyumbuliko (flexibility).

Sumu hii inayotoka baada ya simu kutupwa ovyo na sumu hiyo kuruhusiwa kusambaa inasababisha matatizo  endapo mtu atakuwa karibu na vumbi la beryllium na hivyo kusababisha maradhi yaitwayo ‘beryllicosis’ ambayo inaweza kusababisha makovu ya kudumu kwenye mapafu na wakati mwingine kusababisha kifo.

Kwa ujumla madhara ya betri na simu za mikononi kwa mazingira ni makubwa  hata hivyo inategemea aina ya betri na kwamba itatumika muda gani kabla haijaisha matumizi yake.
Betri ambazo zinaweza kudumu muda mrefu na kuchajiwa zinaleta madhara madogo ukilinganisha na zinazodumu muda mfupi na zisizoweza kuchajiwa ambazo hutupwa ovyo kama ilivyo kwa nchi nyingi maskini..

Swali : Unazungumziaje  utupaji wa  simu zilizochakaa  na  viambata vyake , athari za kikemikali kwa mazingira? 
Jibu: Utupaji wa  simu zilizochakaa kwa hapa Tanzania siyo mzuri kwa maana zinatupwa ovyo kama taka nyingine hivyo zinaweza kusababisha madhara makubwa kama ifuatavyo.

Kemikali nyingi zilizomo kwenye simu za mkononi  hujikusanya kwenye mwili wanyama pamoja na binadamu pia. Kitaalamu kemikali hizi huitwa ‘persistent bioaccumulative toxins (PBTs)’.
Kwakuwa PBTs hujikusanya kwenye mafuta ndani ya miili ya watu na wanyama  usumu wake huongezeka taratibu kwa hivyo kuingiza mfumo mzima wa utegemezi ulaji ‘the food chain’ katika hatari kubwa. Hivyo kuna haja ya kuchukua hatua na kurekebisha athari zake kabla hazijawa kubwa kama ambavyo inafikiriwa.       

Swali: Mataifa yaliyoendelea yanatumia utaratibu gani katika kutupa betri hizi na simu zilizomaliza muda wake? Tutajie mifano kama ipo.

Jibu: Utupwaji wa simu katika nchi zilizoendelea limekuwa tatizo ijapokuwa mara nyingi zinasafirishwa kupelekwa katika mataifa maskini kama bidhaa za mitumba ili kuepukana na madhara yake japo wanafanya kwa ujanja.

Pamoja na hilo mataifa hayo yanahimiza matumizi ya betri zinazoweza kuchajiwa zaidi  ambazo zinazoweza kudumu kwa muda mrefu ili kupunguza  kasi ya kuharibu mazingira. Vilevile katika nchi zilizoendelea kama vile  mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU), betri na simu zote zenye kemikali ambazo zimo kwenye orodha ya ‘the Basel Convention’s Annex I’ zimezuiliwa kutumika tangu July 1, 2006.

Hivi sasa EU imeweka udhibiti wa matumizi ya kemikali hizi hatarishi.  Pia miongozo inatumiwa  namna ya kuachana  na matumizi ya betri zenye lead, cadmium, hexavalent chromium na simu zenye vizuio vya moto vyenye bromine,  (brominated flame-retardants)  kwenye vifaa vyote vya kielectroniki.
Swali: Unadhani kwa Tanzania nini kifanyike kudhibiti utupaji ovyo wa simu na betri zake?

Jibu: Wakati wa kutengeneza sheria (sina uhakika kama Bunge limetunga sheria hii) na miongozo ya namna ya kutupa taka zitokanazo na vifaa vya kielectroniki  na pia itumie sheria za kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kama vile ‘the Basel Convention’ ili kuelekeza namna ya kudhibiti utupaji ovyo wa simu za mkononi  na betri zake.
Ukiacha suala la sheria za namna ya kutupa, pia kuwepo udhibiti wa kutoagiza ama kuingiza nchini simu na vifaa vya kiieletronic vya mitumba kwa maana vinaharibika kwa muda mfupi na kuleta madhara mapema.
Yafaa serikali ifikirie kama kuanzisha sehemu maalum za kukusanya na kutupa simu na vifaa vingine vya kieletronic kwa utaratibu maalum ili kudhibiti uharibifu mkubwa mazingira  unaoweza kuletwa na utupaji holela uliopo sasa.

Tunaweza kuangalia uwezekano wa kufanya urejelezaji ‘recycling’ ya baadhi ya vifaa vinavyotumika kutengeneza simu. Pia serikali idhibiti uingizaji wa simu za bei duni pia ihakikishe kuwa bei za kulipia simu kwa makapuni yote hazitofautiani ili mtu asimiliki zaidi ya simu moja na hivyo kupunguza idadi ya wingi wa simu na viambata vya kutupwa zinapomaliza muda wa matumizi.

Mbinu  hizi zitumike pia vijijini ambapo kuna watumiaji wengi wa simu na idadi kubwa ya simu za mitumba
Mwisho

 
CHANZO: NIPASHE