Saturday, 9 November 2013

Waambata wa kijeshi DRC watembelea uwanja wa mapambano


Maafisa wa kijeshi katika balozi mbali mbali mjini Kinshasa wametembelea mahali palipokuwa ngome za mwisho za waasi wa M23 katika milima ya Chanzu mashariki mwa nchi hiyo.
Mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa akiongoza msafara mashariki mwa DRC Mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa akiongoza msafara mashariki mwa DRC
Siku tatu baada ya majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo-FARDC, kuwatimua waasi wa M23 kutoka kwenye maeneo waliyokuwa wanayadhibiti katika wilaya za Rutshuru na Nyiragongo mashariki mwa Kongo, wajumbe wa balozi mbalimbali nchini humo walisafiri hadi katika makao makuu ya zamani ya M23, kwenye mlima wa Chanzu ambako walishangazwa kuona vifaa vingi vya kijeshi walivyokuwa navyo waasi wa M23 ambavyo waliviacha kwenye uwanja wa mapambano.
Jeshi la serikali liliwatimua waasi wote wa M23 kutoka ngome zao zote  
 
Jeshi la serikali liliwatimua waasi wote wa M23 kutoka ngome zao zote
Akizungumza na waandishi wa habari katika mlima huo, mwambata wa kijeshi katika ubalozi wa Ujerumani mjini Kinshasa Thomas Brillisauer aliyekuwa kwenye ujumbe uliokwenda huko aliwapongeza wanajeshi wa serikali ya Kongo, FARDC, kwa kazi kubwa waliyoifanya kuwatokomeza waasi wa M23Brillisauer alisema, "Hongera kwa FARDC, kundi la M23 limekwisha, nadhani kwamba kazi hii pia ni matunda ya uungwaji mkono wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa cha MONUSCO, ambacho kiliingilia kati. Na Ujerumani inaunga mkono jeshi la FARDC kupitia mafunzo ambayo wanafanyia Ujerumani."

Kwa upande wake ofisa wa kijeshi kwenye ubalozi wa Ubelgiji katika Jamhuri ya Kidempkrasia ya Kongo, Kanali Steve Lemer, alisema ameshangazwa kuona vifaa vya kijeshi walivyokuwa navyo waasi wa M23 katika eneo hilo.
Wengi wa wapiganaji wa M23 sasa wamekimbilia nchini Uganda  
 
Wengi wa wapiganaji wa M23 sasa wamekimbilia nchini Uganda
Afisa huyo alisema, "Sikufikiria kuona risasi nyingi kiasi hiki katika eneo hili. Nilijuwa kwamba M23 walipiga kambi katika mlima huu lakini kwa kuona risasi nyingi namna hii unatambua kwamba walikuwa na njama ya kubaki na kuchukua maeneo mengi katika kanda hii,'' alisema afisa huyo na kuongeza kuwa ingefaa uchunguzi ufanywe kujua msaada huo ulikuwa ukitoka wapi.

Wajumbe hao wa balozi za Ujerumani, Ubelgiji, Urusi na tume ya pamoja ya uchunguzi iliyowekwa na jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya kanda ya maziwa makuu, walikwenda Chanzu ambako walitimuliwa waasi wa M23 siku tatu zilizopita.

Ziara yao katika eneo hilo iliwapatia fursa ya kutambua mengi kuhusu nguvu waliyokuwa nayo waasi wa M23 katika vita baina yao na jeshi la serikali, FARDC.

Wapiganaji wa M23 wengi wao wamevuka mpaka na kukimbia, baadhi wakielekea nchini Uganda na wengine Rwanda. Kwa wakati huu hali ni tulivu katika wilaya za Rutshuru na Nyiragongo.
Mwandishi: John Kanyunyu
Mhariri: Josephat Charo

SOURCE: DW.DE