Thursday, 14 November 2013

Mvungi, Ulimboka, Kibanda walipanga upya Jeshi la Polisi

Sura za Habari Hii
Mvungi, Ulimboka, Kibanda walipanga upya Jeshi la Polisi
Watuhumiwa wa Dk. Mvungi
Kova na watuhumiwa
Zana zilizotumika kujeruhi:
Kuumizwa kwa Kibanda na Ulimboka
Habari Yote
*Dk. Nchimbi atangaza kuundwa kwa divisheni mpy aya uhalifu
MATUKIO ya kutekwa na kujeruhiwa, Dk. Sengondo Mvungi, Absalom Kibanda naDk. Stephen Ulimboka, yamelazimisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuunda Divisheni mpya ya Kiitelejensia.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuwa divisheni hiyo inaundwa kwa lengo la kupambana na mbinu mpya za uhalifu zinazofanywa na majambazi ikiwamo kushambulia na kuteka watu.

Dk. Nchimbi alisema divisheni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa kabla ya Desemba 31, mwaka huu na itaongozwa na mkurugenzi wake, ‘Director of Criminal Intelligence’ ambaye atatangazwa na Rais.

Waziri alisema maandalizi ya kuundwa divisheni hiyo yamekamilika ikiwa ni pamoja na askari zaidi ya 200 kuhitimu mafunzo ya mbinu mpya za kupambana na uhalifu katika Chuo Cha Polisi (CCP), Moshi.

“Awali tulikuwa na kitengo tu, sasa itakuwa divisheni kamili na itakuwa na mkurugenzi wake na askari wetu tayari wamepata mafunzo na hawa watasambazwa katika kila tarafa nchi nzima.

“Hii itaondoa haya matukio yanayotokea sasa ya uhalifu yanayowapata raia wetu na tutapeleka kila tarafa askari wetu,” alisema.

Watuhumiwa wa Dk. Mvungi
Wakati huohuo, watu wengine watatu wametiwa mbaroni wakituhumiwa kuhusika katika tukio la ujambazi alilofanyiwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi na kufanya idadi ya watu waliokamatwa hadi sasa kufikia tisa.

Dk. Mvungi alivamiwa nyumbani kwa Mpiji Magohe, Novemba 3, mwaka huu ambako alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa kwa mapanga.

Dk. Nchimbi alisema kukamatwa kwa watu hao ni mafanikio makubwa ikizingatiwa kwa muda mrefu matukio ya watu kushambuliwa yamekuwa yakiongezeka huku watuhumiwa wakiwa hawapatikani.

Waziri alisema kutokana na kuimarishwa mfumo wa intelijensia wa jeshi la polisi, watuhumiwa hao walikamatwa na simu iliyokuwa inatumiwa na Dk. Mvungi pamoja na mapanga, kigoda ambavyo vinadaiwa kutimika katika tukio hilo.

Alisema watu hao waliweza kukamatwa kutokana na utambuzi wa upelelezi wa kiintelejensia uliofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na familia ya Dk. Mvungi

Akizungumzia namna walivyokamatwa watu hao, Dk. Nchimbi alisema baada ya baadhi yao kukamatwa waliwataja wenzao na sehemu walipoficha silaha zao zilizotumika katika tukio hilo.

“Bila msaada wa familia kazi ya upelelezi wa polisi ingekuwa ngumu, lakini pia ninavishukuru vyombo vya habari kwa kutulia kwao…. Hawakusumbuka na uvumi wa watu maana wangefanya kazi hii kuwa ngumu kweli,” alisema Dk. Nchimbi.

Kova na watuhumiwa
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwataja watuhumiwa wote tisa waliokamatwa kuwa Msigwa Opelle ‘Matonya’ (31) ambaye alikuwa kiongozi katika tukio hilo na Chibango Megozi, anayedaiwa kusaidiana na kiongozi huyo katika tukio hilo.

Wengine ni Ahmed Alli, Mkazi wa Mwananyamala, Zakaria Raphael (23) dereva wa bodaboda na mkazi wa Buguruni Malapa na Mongishiu Dosingo muuza ugolo mkazi wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Mbali na hao pia aliwataja Mange Sarwaa ‘Mr White’ (40), Paulo Jairos ‘Ndonondo’ (29), Juma Khamis Kanguwaa (29), ambao wote ni wakazi wa Vingunguti, Dar es Salaam na Mesunge Makenza Kimilanzoke (40), ambaye ni dereva wa bodaboda na mkazi wa Kitunda, Dar es Salaam.

Zana zilizotumika kujeruhi:
Kwa mujibu wa Kova, zana zilizotumiwa na watuhumiwa hao wa ujambazi ni mapanga matano na kigoda.

“Haya ndiyo mapanga watuhumiwa wenyewe walituonyesha, haya ni mafanikio makubwa tumekamata watuhumiwa wenyewe na kwa mara ya kwanza wenyewe wameonyesha vielelezo.

“Haya mapanga na simu tumehifadhi kwenye bahasha maalumu ili tusiingiliane vidole na wahalifu, haya ni maandalizi ya kulelekea kwenye jinai,” alisema Kamishna Kova.

Kwa mujibu wa Kova, upelelezi wa tukio hilo umekamilika na kinachosubiriwa ni Wakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuthibitisha ili hatua nyingine za sheria ziweze kuendelea.
  
 Kuumizwa kwa Kibanda na Ulimboka
Akizungumzia jeshi la polisi kushindwa kuwakamata watu waliohusika na matukio ya kushambuliwa kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, Kova alisema tukio la kujeruhiwa kwa Dk. Mvungi na matukio ya kushambuliwa kwa Kibanda naDk. Ulimboka haya yametofautiana.

Dk. Mvungi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi na pia Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alivamiwa nyumbani kwake Novemba 3, mwaka huu.

Hivi sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Millpark nchini Afrikan Kusini.

CHANZO: MWANANCHI