Saturday 9 November 2013

Polisi wafukuzwa kazi kwa kuhodhi jino la tembo


Na Anthony Mayunga, Mwananchi

Posted  Novemba9  2013  saa 8:23 AM
Kwa ufupi
Kwa sasa wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilayani Bunda kujibu mashtaka dhidi yao.


Serengeti. Askari polisi wa Idara ya Upelelezi waliokamatwa wakati wakijaribu kuuza jino la tembo, wilayani Serengeti, wamefukuzwa kazi.
Kwa sasa wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilayani Bunda kujibu mashtaka dhidi yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Fernandi Mtui alisema askari hao walikamatwa usiku wa Oktoba 25 mwaka huu wakiwa na raia mmoja mkazi wa Bomani, mjini Mugumu.
Kamanda Mtui alisema walikutwa wakiwa na jino la tembo wakiwa katika harakati za kutafuta soko na kwamba walikuwa wanatumia gari.
“Baada ya kukamatwa, washtakiwa walishtakiwa kijeshi na baadaye kufukuzwa kazi ili wafikishwe katika mahakama ya kiraia,” alisema Mtui.
Alitoa wito kwa askari na wananchi kuacha kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali na kwamba watakaokamatwa watashtakiwa.
Kamanda huyo alisema katu polisi watasita kuchukua hatua. 

SOURCE: MWANANCHI