Thursday, 14 November 2013

Waasi wa Uganda, Rwanda waonywa

MAJESHI ya Umoja wa Mataifa (UN) na brigedi maalumu ya majeshi ya Afrika yanasubiri amri ya kuanza kuvishambulia vikosi vya jeshi la msituni vya Allied Democratic Forces (ADF)) cha Uganda na kile cha Democratic Forces for the Liberation of (FDLR) cha Rwanda ambavyo vimekua vikifanya mashambulio kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).


Kutokana na hali hiyo majeshi ya UN na brigedi maalumu ya vikosi vya Afrika vimeanza mashambulio dhidi ya vikosi vya ADF, kinachoipinga Serikali ya Uganda na kile cha FDLR, kinachoipinga Serikali ya Rwanda.

Taarifa kutoka ndani ya mkutano wa nchi za Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Kimataifa ya nchi za Maziwa Makuu kilichofanyika Afrika Kusini mwishoni mwaka mwezi uliopita, zimethibitisha Uganda na Rwanda kufanya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Jeshi la UN na brigedi ya Afrika yenye askari kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi, zimepewa kibali cha kuondoa na kusafisha mabaki ya wapiganaji wote wa msituni kaskazini mwa Kongo.

Taarifa kutoka ndani ya mkutano huo zilieleza kuwa nchi ambazo zinawahifadhi wapiganaji hao wa msituni waliojisalimisha kutoka kundi la waasi la M23 zimetakiwa kuwakabidhi mikononi mwa Serikali ya Kongo ua katika nchi walizotoka.

Vikundi hivyo vinavyokadiriwa kufikia 10, ni pamoja na vile vya Lord’s Resistance Army (LRA), ADF na FDLR vinaelezwa vimejificha katika misitu ya Kongo.

Luteni Kanali Paddy Ankunda, Msemaji wa jeshi la Uganda (UPDF) alisema sasa umefika wakati wa kuwaondoa wanajeshi wote wa msituni kaskazini mwa DRC kuweza kuleta amani na utulivu katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati.

“Napenda kuvishukuru vikosi vya UN na vile vya Afrika kwa kusaidia kuleta amani ndani ya Kongo,” alisema Ankunda.

Msemaji wa jeshi la Kongo, Kanali Olivier Hamuli alisema kuwa jeshi la nchi yake na lile la UN na brigedi maalumu ya Afrika, watavisaka na kuvitimua vikundi vyote vya msituni mashariki ya Kongo.

“Tunawapa muda wa kati ya saa 48 au zaidi kujisalimisha na kama hawataki kufanya hivyo basi tutawanyang’anya silaha kwa nguvu ya jeshi,” alisema Hamuli.

Makundi hayo madogo yametofautiana na kundi la M23 na majeshi ya Umoja wa Mataifa na yale ya Afrika yatakuwa na wakati mgumu kuvisambaratisha vikundi vya ADF na FDLR ambavyo vimejiimarisha Kongo kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Zaidi ya askari 3,000 wa brigedi maalumu ya Afrika na askari zaidi ya 18,000 wa UN chini ya MONUSCO mapema mwaka huu walipewa kazi ya kuviondoa vikosi vyote vya wapiganaji wa msituni kutoka DRC.

Inaelezwa kuwa kukosekana kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda katika mkutano wa SADC kulitafsiriwa kuwa bado kuna msuguano miongoni mwa viongozi wa SADC.

Kutokana na hali hiyo SADC iliazimia kutumika nguvu za jeshi dhidi ya vikosi ya M23 wakati Uganda na Rwanda zilikuwa zikitaka mazungumzo kumaliza mzozo wa Kongo.

Kwa muda mrefu sasa Uganda na Rwanda zimekuwa zikishutumiwa kwa kulisaidia kwa kulipa mafunzo ya jeshi na fedha kundi la waasi wa M23.

Wakati viongozi wa Jumuiya za SADC na IGCLR wakianza kutafuta maelewano kwa kikosi cha wapiganaji wa M23, vikosi vya ADF na FDLR vimetangaziwa onyo la kutakiwa kujisalisha na kukabidhi silaha kwa majeshi la UN.

Katika mkutano huo wa Afrika Kusini viongozi kutoka nchi 20 walihudhuria. Hao ni Rais Yoweri Museveni wa (Uganda), Jacob Zuma (Afrika Kusini), Joseph Kabila (Kongo DRC), Jakaya Kikwete (Tanzania).

Wengine ni Uhuru Kenyatta (Kenya), Joyce Banda (Malawi), Hifikepunye Pohamba (Namibia), Robert Mugabe (Zimbabwe) na Motsoahae Thabane (Lesotho.

CHANZO: MTANZANIA