Thursday, 14 November 2013

Mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na bastola ya Dk Mvungi

Kamanda wa Polisi Kanda ya Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akiwaonyesha waandishi wa habari bastola iliyodai ni ya Marehemu Dk Sengondo Mvungi, ambayo polisi wamedai wamemkamata nayo mkazi wa Kiwalani katika eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam. PICHA|PAMELA CHILONGOLA 
Na Pamela Chilongola, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Novemba14  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Huyo anakuwa mtuhumiwa wa 10 kukamatwa tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kulikosababisha kifo cha Mjumbe huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


Dar es Salaam.Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia mtu mmoja (jina tunalihifadhi), kwa tuhuma za kukutwa na bastola inayodaiwa kuwa ilikuwa inamilikiwa na marehemu Dk Sengondo Mvungi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alidai jana kuwa mkazi huyo wa Kiwalani, Dar es Salaam alikutwa na bastola aina ya Revolver yenye namba BDN 6111 ikiwa na risasi 21 na baada ya kufuatilia kumbukumbu zao na kuwasiliana na familia ya Dk Mvungi walibaini kwamba ilikuwa ni ya mwanasheria huyo nguli.
Huyo anakuwa mtuhumiwa wa 10 kukamatwa tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kulikosababisha kifo cha Mjumbe huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Dk Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Novemba 3, mwaka huu. Mbali ya kushambuliwa, wavamizi pia waliiba bastola, kompyuta mpakato (laptop) na simu tano za mkononi.
Kamishna Kova alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 12 jioni Mitaa ya Twiga na Jangwani alipokuwa akiangalia runinga na akifuatilia taarifa za matukio ya tukio hilo. Alisema kukamatwa kwake kulitokana na taarifa za msamaria mwema.
Alidai kwamba baada ya kukamatwa aliwaongoza polisi hadi nyumbani kwake Kiwalani ambako walikuta bastola moja na risasi hizo.

SOURCE: MWANANCHI