Tuesday, 19 November 2013

Askofu: Mtandao umemuua Mvungi

19th November 2013

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,Marehemu Dk. Sengondo Mvungi
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, alizikwa jana katika Kijiji cha Chanjale Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro huku Askofu Rogath Kimario wa Kanisa Katoliki Jimbo la Same, akiwaeleza waombolezaji kwamba marehemu amekufa kwa kifo cha fedheha kilichotokana na kile alichokiita mauaji ya kimtandao.

Akihubiri katika ibada ya mazishi ya Dk. Mvungi, Askofu Kimario akiwa mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,  Angela Kairuki na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kuwa kwa kifupi Dk. Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12 mwaka huu, mauti yake yametokana na mauaji ya kimtandao na kwamba jamii imechoka na maswali yasiyojibika.

Marehemu arifariki dumia Katika Hospitali ya Milpark iliyopo Johannesburg, Afrika ya Kusini baada ya kuhamishwa kutoka Kitengo cha Mifupa(MOI) cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Acheni kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu katika masuala mazito kama haya yanayoligusa taifa kwa kutoa kauli za kutuaminisha kwamba ndugu yetu (Mvungi) alivamiwa na watu wanaoitwa majambazi.
Hivi ni nani aliyefanya hiyo research (utafiti) kwamba hao walikuwa majambazi?” alihoji Askofu Kimario huku akisisitiza kwamba Watanzania hawawezi kuamini katika hewa ambayo haipo.

Askofu Kimario alisema msiba huo ni wa wasomi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa Dk. Mvungi ni nguzo iliyoanguka na mhimili uliopotea.

“Wanyonge tuna maswali, tunataka majibu ya kifo cha Dk. Mvungi na kwa kweli hakuwa mwizi, mbinafsi, jambazi wala tajiri ambaye hawa wanaoitwa majambazi wamengelimfuata na kumshambulia kwa mapanga,” alisema na kuongeza:

“Amekufa hana kitu na hata nyumbani kwao hakujenga kwa sababu ya kulihangaikia taifa hata akasahau kwao. Wenye huo mtandao wote ni wadhalimu na wauaji.”

Ibada ya mazishi hayo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, aliyeafuatana pia na Askofu wa Jimbo la Geita, Damian Ngulu na Mkuu wa Parokia ya Kisangara Juu, Padri Wilhad Mbombengwa.

Wakati Askofu Kimario akizungumza hayo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hakuwa amewasili katika kanisa hilo na badala yake aliwasili saa 7:30 mchana akitokea mkoani Arusha na kupata nafasi ya kutoa kauli ya serikali akisema:

“Ni dhahiri kwamba ndugu yetu huyu hatunaye, serikali inafanya jitihada za kuwakamata watu waliofanya tukio hili la ovu, bado hata tukiwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na wakahukumiwa kunyongwa hakuna mbadala wa Dk. Sengondo Mvungi, lakini kwa kuwa sheria zinataka hivyo, tutahakikisha haki inatendeka.”

Alisema sifa zote na wasifu wa Dk. Mvungi zilizoelezwa na Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, na wanazuoniwengine zinatosha kuueleza umma wa Watanzania kwamba Dk. Mvungi alikuwa mtu wa aina gani katika jamii.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kueleza mchango wa kifikra wa kile kilichokuwa kikifanywa na Dk. Mvungi ndani ya Tume kwa miezi 18 ya kusaka maoni ya wananchi, akisema kwamba mwanamageuzi huyo hakuwa mbaguzi wa rangi, itikadi wala rika katika kusimamia kile
alichokiamini.

“Sengondo hakuwa mwoga kutoa mawazo yake kwa kile alichokiamini, lakini wakati fulani nilipewa kazi inayohitaji wanazuoni waliobobea na nikawachagua yeye na Dk. Harrisson Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) kunisaidia mambo mazito yanayohitaji ushauri wa kitaaluma,” alisema jaji Warioba na kuongeza:

“Kwa hivyo ameondoka ninamwomba Mungu aniongoze katika kazi ya katiba kwa sababu pengo lake linaonekana wazi.”

Akisoma wasifu wa marehemu, Profesa Kabudi alisema kuwa Dk. Mvungi wakati wa uhai wake alikuwa mchukia rushwa, dhuluma na mtu aliyechukia majungu jambo ambalo liliwafanya wamwite “Nguto au Leopard” kutokana na umahiri wake katika kuamua mambo mazito yakitaaluma na yale yanayohusiana na mustakabali wa siasa za nchi.

“Alikuwa mzalendo, jasiri na mwanamapinduzi wa kifikra katika amali ya dunia, mwili wake ungali utabaki juu ya nchi, lakini nafsi yake itabakiikisadifu maono na karama za uongozi wa taifa hili.
Ni mtu asiyehesabu wala kujali mapato zaidi ya kutanguliza uzalendo wake mbele,” aliongeza
Profesa Kabudi.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na maofisa mbalimbali wa serikali.

Mwili wa Dk. Mvungi uliingizwa karubini saa 9:45 baada ya kukamilika kwa ibada ya mazishi iliyomalizika saa 9:20.

Mazishi hayo yalifanyika katika makaburi ya familia ya wazazi wake, Mzee Adrian Muganyo Mvungi yaliyopo katika kitongoji cha Chamakera.

Simanzi ilitawala katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Parokia ya Kisangara Juu, miongoni mwa mamia ya waombolezaji waliojitokeza kumzika.

Marehemu ameacha mjane, Anna Shayo na watoto watano.
CHANZO: NIPASHE