Thursday 31 October 2013

Dk Shein aongoza mazishi ya Balozi Sepetu Unguja

Na Mwinyi Sadalla na Beatrice Moses, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mapema mwili wa Balozi Sepetu uliagwa na waombolezaji wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa shughuli ambayo ilifanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo eneo la Kikwajuni katika Manispaa ya Zanzibar kabla ya misa maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph katika Mtaa wa Shangani.

Zanzibar/Dar. Rais wa Zanzibar,Dk Ali Mohammed Shein, jana aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika maziko ya mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe Marehemu
Balozi Issack Abraham Sepetu (71),aliyezikwa katika Kijiji cha Mbuzini,Mkoa wa Kusini Unguja jana Alasiri.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mapema mwili wa Balozi Sepetu uliagwa na waombolezaji wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa shughuli ambayo ilifanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo eneo la Kikwajuni katika Manispaa ya Zanzibar kabla ya misa maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph katika Mtaa wa Shangani.
Watoto wa marehemu, Amani,Mkusa, Wema na wengineo walikuwapo katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na Balozi mstaafu, Ali Abeid Karume, ambaye alisema marehemu ameacha pengo kubwa katika jamii kwani alikuwa kiongozi makini na mzalendo aliyelipenda taifa lake.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,Vuai Ali Vuai,alimwelezea marehemu kama mwasisi wa mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar wakati juhudi hizo zilipoanza mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi visiwani mwaka 1995 kupitia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Chifu Emeka Anyaoku.

SOURCE: MWANANCHI