Monday 28 October 2013

UVCCM wamwandamana Maalim

Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad. 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Oktoba28  2013  saa 10:38 AM
Kwa ufupi
Kiongozi huyo wa UVCCM, alisema watu wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
 

Wanasema Serikali inatumia fedha nyingi kugharimia matibabu ya kiongozi huyo nje ya nchini, kinyume na ahadi yake ya kutotibiwa nje.
Zanzibar. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis amesema baadhi ya viongozi ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wameshindwa kutekeleza wajibu wao.
Amesema wajibu huo  ni pamoja na  kushindwa kutatua kero za madaktari na kusababisha kuzorota kwa huduma za afya visiwani humo. Sadifa aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara  katika Uwanja wa Vuga katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
“Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kumhudumia kwa matibabu, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad, itakumbukwa aliwahi kuwaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa akiwa kiongozi atahakikisha anatibiwa hapa hapa badala ya kusafirishwa nje ya nchi,” alisema.
Wabara waishio Zanzibar
Kiongozi huyo wa UVCCM, alisema watu wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sadifa alisema wapinzani wanaohoji uhalali wa watu hao kuishi na kufanya kazi Zanzibar, hawafahamu haki ya  kila mtu kikatiba kwa maana ya kuwa huru kuishi na kufanya kazi katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema ibara ya 11 na 26 ya katiba imeweka wazi kwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu atakayo ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Huku akishangiliwa na wanachama wa CCM alisema sera za ubaguzi hazitasaidia kujenga amani na umoja wa kitaifa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alisema umoja huo umeamua kuchunguza kikundi cha watu wenye asili ya India ambao wamekuwa wakipinga misingi ya Mapinduzi na  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona watu hao wakiwa katika mstari wa mbele kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakati hakuna muafrika anayeweza kwenda kuhoji uhalali wa harakati za ukombozi wa India au Iran kama hali ilivyojitokeza visiwani Zanzibar.
Alisema kitendo hicho hakikubaliki.

SOURCE: MWANANCHI