Kwa ufupi
Dar es Salaam.
Maofisa wawili wa Wizara ya Fedha wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Wanatuhumiwa kwa ufisadi wa fedha za utoaji wa matangazo na habari kwa
vyombo mbalimbali vya habari.
Maofisa waliopandishwa kizimbani ni pamoja na
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Ernest Simon Mwakitalu na Ofisa
Ununuzi, Liipu Neligwa ambao walisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Wakati maofisa hao wawili wakipandishwa kizimbani
na kusomewa mashtaka hayo, wengine wawili ambao walitakiwa kupandishwa
kizimbani, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Ingiahedi Mduma na Mkurugenzi wa
Kampuni ya And- Line (2000) International, Daniel Ukwaya hawakuwapo mahakamani hivyo, mashtaka dhidi yao hayakusomwa hadi watakapokamatwa.
Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanakabiliwa na
jumla ya mashtaka 19. Shtaka moja ni kula njama kutenda kosa, mashtaka
manane ya kutumia nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri.
Mengine ni shtaka moja la matumizi mabaya ya
madaraka, mashtaka manane ya kughushi, shtaka moja la ubadhirifu na
shtaka moja la kusababisha hasara ya Sh19.8 milioni, ambalo ni shtaka
mbadala kwa wote.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Swai alisema
washtakiwa hao walitenda makosa hayo kwa tarehe tofauti kati ya Juni na
Julai, 2009.
Wakili Swai alidai kuwa washtakiwa hao walisaini
hati za ununuzi zenye taarifa za uongo kwa lengo la kuonyesha kuwa
Kampuni ya And Line (2000) International ilipewa fedha kwa ajili ya
vipindi vinane vya matangazo katika vyombo vya habari vya redio,
magazeti na runinga.
Alidai kuwa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari
zilihusu maonyesho ya 33 ya Biashara ya Kimataifa yaliyofanyika Dar es
Salaam katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Kilwa Road, kuanzia Juni 28
hadi Julai 10, 2009, kwa thamani ya Sh19.8 milioni, jambo ambalo si
kweli.
Baada ya kuwasomea mashtaka, Wakili Swai alisema
upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba Mahakama ipange tarehe
nyingine ya kutajwa ambayo washtakiwe wengine watakuwa wamekamatwa ili
wasomewe maelezo ya awali kwa pamoja.
Washtakiwa waliokuwapo mahakamani jana walikana
tuhuma dhidi yao na waliachiwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti ya kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni, kuwa na
wadhamini wawili wanaotambulika, ambao pia walisaini hati ya dhamana ya
kiasi hichohicho.
Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba hadi Agosti 15, mwaka huu itakapotajwa tena.