Monday 5 August 2013

Wafuasi wa MDC wadai kushambuliwa ZIM


 5 Agosti, 2013 - Saa 07:53 GMT

                           
Ushindani ulikuwa mkali kati ya Morgan Tsvangirai na Mugabe katika uchaguzi mkuu
Siku moja baada ya Rais Robert Mugabe na Zanu PF kutangazwa kushinda uchaguzi Mkuu nchini humo, baadhi ya wafuasi wa upinzani kutoka chama cha MDC wanasema wameshambuliwa na wenzao wa ZANU PF.
Baadhi ya dola za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, zimetilia shaka iwapo uchaguzi huo ulifanyika kwa uwazi.
Madai hayo yanakuja siku moja baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi uliofanyika Jumatano kutolewa na kumpa ushindi rais Robert Mugabe. Chama chake Zanu-PF kilipata thuluthi tatu ya viti vya bunge.
Watu 11 mjini Harare na wengine 20 kutoka mkoa wa Mashonaland, wanasema kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF wanaojulikana sana baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Chama cha MDC kimesemna uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi wa kura.
Kiongozi wake Morgan Tsvangirai, ameahidi kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.
Pia alisema kuwa chama chake cha MDC, hakitashirikiana na kile cha Mugabe na kuwa kitasusia kushikilia nafasi zozote katika taasisi za serikali.
Vyama hivyo viwili, vimekuwa wanachama wa serikali ya Muungano tangu mwaka 2009,baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2008 kusababisha ghasia.
Watu 11 waliodai kushambuliwa katika mtaa mmoja mjini Harare waliomba hifadhi katika makao makuu ya chama cha MDC mnamo Jumapili, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Brian Hungwe.
Wanadai kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF waliokuwa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakiwaamuru wafuasi wa MDC kufunga virago vyao na kuondoka.
Kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai alisema uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi.
Msemaji wa MDC, Douglas Mwonzora, alisema kuwa mashambulizi hayo yalipangwa. Lakini msemaji wa chama cha Zanu PF, Psychology Maziwisa, alikanusha madai kuwa wafuasi wa chama walikuwa wanawashambulia wapinzani wao.
MDC kinaonya kuwa hakitaweza kuwadhibiti wafuasi wake ikiwa madai ya wao kushambuliwa yataendelea.
Chama hicho kimeomba muungano wa nchi za Kusini mwa Afrika , Sadc, kuingilia kati na kuzuia hali kuzorota zaidi kiasi cha kutoweza jkudhibitiwa.
Baadhi ya wakuu wa chama cha MDC, wametoa wito kwa wafuasi wao kutoitii serikali na kutenga chama cha Zanu-PF.

chanzo: BBC  Sawahili