Kwa ufupi
Mbinu mbalimbali za kusafirisha dawa hizo hutumika ikiwemo kuwatumia watoto na wanawake kuficha katika rasta zao. sasa endelea
Uchunguzi wetu ulibaini kuwa unaweza kununua
kinyago cha kimakonde na kukitoboa katikati kisha kuhifadhi cocaine,
heroin au mandrax ndani kisha kukifunga vyema kama mzigo katika boksi na
kuutuma katika nchi unayoitaka.
Hata hivyo, mbinu maarufu inayotumiwa na
Watanzania wengi ni kumeza pakti za dawa za kulevya na kusafiri kwa njia
ya basi hadi Afrika Kusini kisha kuvitoa kwa njia ya haja kubwa baada
ya kufika.
Njia hii imekuwa na athari kiasi cha baadhi ya
wasafirishaji kupoteza maisha; Mfano ni Watanzania wawili, Hassan
Wanyama na Ali Mpili ambao walifariki mwaka jana kwa kumeza dawa hizo
kisha kupasukia tumboni.
Mpili alifia katika nyumba ya wageni ya Braeside,
Harare baada ya kukosa basi la moja kwa moja kwenda Afrika Kusini hivyo
dawa hizo kupasukia tumboni.
Mpili alikuwa amemeza kete zaidi ya 80 za
heroin.Watanzania wawili waliokuwa wakifanya mbinu za kuutorosha mwili
wa Mpili nao walikamatwa.
Watanzania kukithiri katika biashara ya dawa za
kulevya kumesababisha wengi hata wale waaminifu kuingia katika usumbufu
mkubwa na kubatizwa majina chekwa yanayohusiana na dawa za kulevya.
“Mipakani siku hizi sisi Watanzania tunapekuliwa
kivyetu, wakituona tu wanatuita ‘drugs’ tofauti na zamani tulijulikana
kama taifa lenye watu watakatifu,” kinasema chanzo hicho.
Msemaji wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya
nchini (TDCC) Florence Mlay alizungumza na Mwananchi na kueleza kuwa,
tume hiyo bado haina taarifa rasmi kuhusu ongezeko la watumiaji na
wafanyabiashara wa dawa za kulevya Afrika Kusini.
“Kwa sasa hatuna ripoti yoyote kuhusu Watanzania
Afrika Kusini, lakini kwa kuwa vyombo vya habari vinajitahidi kwa kasi
basi tutalifanyia kazi hilo,” alisema Mlay.
Mipaka ya Tanzania
Tanzania kutumika kama moja ya njia kuu za
kusafirisha mihadarati kunathibitishwa na tukio la Julai 2012 ambapo
Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini (SARS) ilikamata kiasi cha kilo 350
cha dawa haramu aina ya Mandrax zikitokea Tanzania, kisha zilipita
Botswan na baadaye kuingia Afrika Kusini.
Julai mwaka huu, wanawake wawili wa Kitanzania
Agnes Masogange na Melissa Edward walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oliver Tambo na mabegi sita yaliyosheheni dawa za kulevya
aina ya methamphetamine maarufu kama `Tik’ yenye thamani ya Sh7 bilioni.
Msemaji wa SARS, Marika Muller alizungumza na Mwananchi na
kueleza kuwa ‘hicho ni kiasi kikubwa cha dawa kukamatwa katika mpaka
wowote wa Afrika Kusini’ kuwahi kutokea.
Mmoja wa watu wanaoishi Afrika Kusini, ambaye
anafahamiana na Agness alisema kuwa, siku chache kabla ya kukamatwa
kwake Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Masogange alionekana nchini
Afrika Kusini akifanya ununuzi wa gharama kubwa katika maduka ya
Johannesburg.
Kadhalika hata baada ya watuhumiwa hao kukamatwa
Mwananchi lilibaini kuwa wamekuwa wakiwatuma baadhi ya watu kuwanunulia
vipodozi na mahitaji mengine kwa ajili ya kuwapelekea mahabusu
wanakoshikiliwa.
Ripoti ya UN
Ripoti ya mwaka 2013 kutoka Ofisi ya Umoja wa
Mataifa ya Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) inaitaja Tanzania kuwa
moja ya nchi kuu za Afrika zinazotumika kama njia ya kusafirisha dawa za
kulevya.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Afrika Mashariki ikiwemo
Kenya na Tanzania ni maeneo makuu yanayopitisha dawa za kulevya aina ya
Heroin kutoka Afghanistan, Mandrax kutoka India na China na Cocaine
kutoka Latin America.
UNODC inasema katika ripoti yake hiyo kuwa hivi
sasa ni kawaida dawa za kulevya kusafirishwa kwa kutumia ndege za mizigo
kutoka Afrika Kusini hadi Dar es Salaam au Zanzibar.
“Afrika Mashariki kwa sasa inawindwa zaidi na
wasafirishaji wa dawa za kulevya kutoka Afghanistan na Pakistan kwa
sababu ya udhaifu katika udhibiti wa bandari, fukwe, viwanja vya ndege
na mipakani,” inasema ripoti hiyo.
Inaelezwa kuwa kingine kinachowavutia
wafanyabiashara hao ni udhibiti dhaifu katika mamlaka za mapato na mfumo
dhaifu wa kudhibiti uhalifu.
Kadhalika UNODC inaweka bayana ramani kuwa Heroin
husafirishwa kutoka Afghanistan, kisha Pakistan na kuingizwa Tanzania,
kabla ya kupelekwa Afrika Kusini.
Pia, ramani hiyo inaonyesha kuwa heroin na cocaine
hupita zaidi katika mipaka ya Tunduma, Malawi na Musina, Limpopo.
Pamoja na Afrika Kusini, kiasi kikubwa cha cocaine na heroin hupelekwa
Marekani na Ulaya Magharibi.Ripoti hiyo pia inachambua kuwa, cocaine
huzalishwa zaidi Latin America na kusafirishwa moja kwa moja hadi
Tanzania, kisha Afrika Kusini.
Heroin nyingine hutoka Myanmar, kisha Thailand na
huingizwa nchini kwa njia ya meli na mara chache kwa ndege. Dawa aina ya
ethaloquone (mandrax) hutoka nchini India au China na kuja moja kwa
moja nchini.
Kwa sasa maeneo mengine yanayotumika kupitisha dawa za kulevya nchini ni maeneo ya visiwani hasa Tanga na Zanzibar ambapo wasafirishaji hutumia boti binafsi ndogo. Mzigo unaposhushwa hapa hupelekwa kama mizigo midogo Dar es Salaam.
source: Mwananchi
Kwa sasa maeneo mengine yanayotumika kupitisha dawa za kulevya nchini ni maeneo ya visiwani hasa Tanga na Zanzibar ambapo wasafirishaji hutumia boti binafsi ndogo. Mzigo unaposhushwa hapa hupelekwa kama mizigo midogo Dar es Salaam.
source: Mwananchi