Kwa ufupi
Akizungumza na Kamati ya Bunge ya Uchumi,
Viwanda na Biashara iliyotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki
iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TPCC, Pascal Lesoinne,
alisema suala hilo kama halijapatiwa ufumbuzi litaathiri uhai wa kampuni
nyingi nchini, hatimaye uchumi wa nchi.
Saruji kutoka nje inadaiwa kusababisha Serikali kupoteza mapato ya Sh25 bilioni kwa mwezi.
Dar es Salaam. Kampuni ya
Uzalishaji Saruji Tanzania Portland Cement Company (TPCC), imeomba
Serikali kuanzisha juhudi za makusudi zitakazosaidia kukabiliana na
uingizaji bidhaa nchini zisizo na viwango ikiwamo saruji.
Akizungumza na Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda
na Biashara iliyotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki iliyopita,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TPCC, Pascal Lesoinne, alisema suala
hilo kama halijapatiwa ufumbuzi litaathiri uhai wa kampuni nyingi
nchini, hatimaye uchumi wa nchi.
“Kampuni nyingi za Kitanzania za saruji hivi sasa
zinakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa saruji itokayo nje hasa
Pakistan,” alisema Lesoinne na kuongeza:
“Waingizaji saruji kutoka nje wanatumia ipasavyo
mianya iliyopo kwenye mfumo wa forodha na uingiaji bidhaa kwa kulipa
kati ya asilimia tano mpaka 10, hali ambayo inasababishia nchi hasara
ya zaidi ya Sh25 bilioni.”
Aliongeza kuwa Tanzania haihitaji saruji kutoka
nje, kutokana na uwapo wa viwanda vingi vinavyoweza fikia mahitaji ya
nchi kikamilifu.
Pia, Lesoinne alisema kutokuwa na umeme wa
uhakika, kumeongeza gharama za uendeshaji kwa kampuni yake na kwamba,
inatumia zaidi ya Dola 2 milioni za Marekani kwa mwezi kwa ajili ya
umeme mbadala.
Naye Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila,
alionyesha wasiwasi wake kuhusu jitihada zinazochukuliwa na mamlaka
husika na kuzitaka kufanya uchunguzi sahihi kujua ukweli wa suala hilo.
“Hili ni suala nyeti. Kamati hatuwezi kulifumbia
macho kwa sababu lina athari kwenye maendeleo ya uchumi wa nchini yetu,”
alisema Kafulila.
Naye Mkurugenzi wa Viwanda Wizara ya Viwanda na
Biashara, Eliness Sikazwe, alisema Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, tayari ameteua kamati ya wanachama saba kuchunguza
suala hilo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi