Kwa ufupi
- Katika hatua nyingine mwekezaji huyo ametangaza kuwekeza ndege nane kwenye Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), mradi ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 100 milioni.
Dar es Salaam. Mwekezaji Sheikh Salim Abdullah
ametangaza kuwekeza kwenye Uwanja Wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere
Dar es Salaam (JNIA) kwa kufunga mashine za kisasa, ili kuimarisha
usalama katika eneo hilo. Sheikh Abdullah ambaye ni Mwenyekiti wa
Kampuni ya Maendeleo na Uwekezaji ya Al-Harathy ya Oman, alitangaza
hatua yake hiyo jana, baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uwanja
huo, ambapo alisisitiza mashine zilizopo uwanjani hapo kwa sasa uwezo
wake kiutendaji na kiusalama ni mdogo. “ Mashine hizi uwezo wake ni
mdogo, dunia tunayoishi sasa imetawaliwa na magaidi uwanja wa ndege ni
eneo muhimu ambalo linapaswa kulindwa kwa uhakika, mizigo inabidi
kukaguliwa kwa umakini zaidi kwani wanaweza kuweka mabomu au vitu
vingine vya hatari wakasababisha madhara makubwa alisema na kuongeza:
“Nimekuja kuwekeza hapa kwa kuitikia mwito wa Rais
Jakaya Kikwete, amechoka sana inabidi sisi tumsaidie, ana nia nzuri ya
kuhakikisha nchi hii inakuwa kiuchumi inabidi tumsaidie kuwekeza katika
maeneo kama haya” alisema. Katika hatua nyingine mwekezaji huyo
ametangaza kuwekeza ndege nane kwenye Shirika la Ndege la
Tanzania(ATCL), mradi ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 100
milioni.
“ Tunanunua ndege nane ambapo nne ni aina ya
Embraer ERJ-175 za Brazil na nyingine nne aina ya Mbombardier,kwa
kuanzia tunapeleka vijana 10 wa kitanzania kwenda kusomea jinsi ya
kuongoza ndege hizo” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton
Lazaro, alieleza kuwa hatua hiyo ni faraja kubwa kwao na wana tumaini
itatumiwa vyema kwa manufaa ya kukuza uchumi .
Kwa upande wake,, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alisema Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji hao,
ikiwa ni pamoja na kusafisha madeni yaliyokuwepo awali
source: Mwananchi