Na Peter Saramba, Mwananchi
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 12:17 PM
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 12:17 PM
Kwa ufupi
Kamati za vyama vihusike kulinda
masilahi ya umma badala ya vyama. Vyama vya siasa vitakuja na kuondoka
lakini taifa na masilahi ya umma vitadumu milele.
Badala ya kutumika kulinda maslahi ya
umma, vikao vya kamati za vyama vimegeuka kichaka cha kulinda wezi,
mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma.
Arusha. Wakati Watanzania
wakitafakari hatima ya Bunge la Jamhuri la Muungano na jinsi
linaloyumbishwa na itikadi za vyama wakati wa uamuzi wa mambo muhimu na
yanayogusa masilahi ya umma, baadhi ya wabunge wanadai bunge hilo
limepoteza sifa.
Wabunge hao kutoka chama tawala, CCM na mpinzani
wake, Chadema wanadai Bunge limepoteza sifa muhimu ya kuwa moja ya
mihimili mikuu ya dola na badala yake limegeuka kamati ya chama.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini
Arusha, wabunge hao, Deo Fulikunjombe, Kangi Lugola, Ally Mohamed
Keissy, wote kutoka CCM na Zitto Kabwe (Chadema), wanakiri kuwa Bunge la
sasa limekosa msimamo wa pamoja katika kusimamia mambo ya msingi
yanayogusa maisha ya wananchi, badala yake mijadala mingi huegemea
itikadi za vyama.
Wakiwa jijini Arusha ambako walihudhuria mkutano
wa kumi wa Umoja wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali kutoka Nchi za
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC (SADCOPAC), wabunge hao
wanadai kuwa badala ya kutumika kulinda masilahi ya umma, vikao vya
kamati za vyama vimegeuka kichaka cha kulinda wezi, mafisadi na
wabadhirifu wa mali za umma.
Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara ameitupia lawama
za moja kwa moja kamati ya CCM inayoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kuwa inawaziba midomo wabunge wa chama hicho tawala kila
zinapoibuka hoja za msingi zenye faida na masilahi kwa umma.
“Wezi, wabadhirifu, mafisadi na watendaji wa
Serikali wanaokiukamaadili na kushindwa kutimiza wajibu wanalindwa
asishughulikiwe na Bunge kupitia kamati ya chama kwa kisingizio cha
kulinda masilahi ya chama na Serikali. Kamati ya chama imekuwa kichaka
cha kulinda wezi?” anasema na kuhoji Lugola.
Anasema Bunge sasa linatumia wingi wa wabunge wa
CCM kama kichaka cha kuridhia kila hoja ya Serikali bungeni bila kupima
faida na madhara yake kwa umma, jambo linalozidi kuwapa sifa wapinzani
ambao licha ya uchache wao, husimama kidete kupinga na hivyo kuungwa
mkono na umma huku CCM ikizidi kupoteza haiba.
“CCM ikitaka kutekeleza ilani yake ya uchaguzi,
basi ituache sisi wabunge wake tuikosoe na kuisimamia Serikali yake
badala ya kazi hiyo kuachiwa upinzani pekee,” anasema na kushauri
Lugola.
Bila kuonyesha mzaha, Lugola anataja mihimili ya
dola iliyosalia sasa baada ya Bunge kupoteza hadhi yake kuwa ni Kamati
za Vyama (Kamati ya Wabunge wa CCM), Mahakama (sheria) na Serikali
(utawala).
Vita dhidi ya ufisadi na dawa za kulevya
Lugola anasema wezi, mafisadi, wabadhirifu wa
fedha na mali za umma pamoja na wafanyabiashara wa dawa za kulevya
nchini wanajulikana kwa majina, sura na mavazi yao, lakini hawaguswi kwa
madai ya kukilinda chama kana kwamba CCM ndiyo inawatuma kutenda maovu
hayo.
“Watu binafsi wanaohusika na uhalifu washughulikiwe kwa maovu
yao wanayoyatenda kwa utashi wao baada ya kukabidhiwa madaraka na ofisi
za umma. Chama kisiwakingie kifua kwa kutuita kwenye kamati,” anasema
Lugola.
Anasema kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuwa akitaja majina ya
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kutatokea mtafaruku
bungeni, inalenga kudhoofisha hoja na vita ya kupambana na madawa ya
kulevya miongoni mwa wabunge.
“Lukuvi (Waziri) anawatia hofu wabunge ili waogope
kuishinikiza Serikali kutimiza wajibu wake kwa kupambana na janga hili
la dawa za kulevya.
Hakuna shaka kuwa anajenga picha kuwa tunahusika
na tunahonga ili tusikamatwe sisi, ndugu au marafiki zetu wanauza unga.
Serikali haina nia ya dhati kushughulikia wauza unga,” anasema.
Keissy (Mbunge wa Sumbawanga Kaskazini) kwa upande
wake, yeye anakwenda mbele kwa kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho
ya sheria bungeni kuruhusu wezi, mafisadi na wabadhirifu wa fedha na
rasilimali za umma kunyongwa hadharani kama inavyofanyika nchini China
ili kutoa fundisho kwa wengine. “Viongozi wahojiwe utajiri wao wa fedha
na mali nyingi wanazomiliki wao na familia zao mara baada ya kukabidhiwa
ofisi za umma. Wakishindwa washtakiwe, wafungwe maisha na ikiwezekana
wanyongwe,” anasema Keissy
Kwa upande wake, Filikunjombe (Mbunge wa Ludewa)
yeye anawaasa wabunge wenzake bila kujali itikadi zao kuweka mbele
masilahi ya umma badala ya vyama vyao wakati wa kujadili na kuamua hoja
mbalimbali bungeni.
“Ndiyo… vyama vinatupa tiketi ya kugombea. Lakini
tukishakuwa wabunge, hatuongozi wanachama wa vyama vyetu pekee bali
Watanzania wote. Lazima maneno, matendo na uamuzi wetu uweke mbele
masilahi ya taifa badala ya vyama vyetu,” anasema Filikunjombe.
Filikunjombe anaongeza kuwa utashi wa kisiasa
miongoni mwa viongozi ndiyo njia pekee itakayotokomeza wizi, ufisadi,
matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma pamoja na utoroshaji nje
wa fedha na rasilimali za umma.
Hoja ya wabunge hawa kutoka Tanzania inaungwa
mkono na mwenzao kutoka Uganda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya PAC
nchini humo, Ssewungu Gonzaga (DP), anayesema vyama tawala barani Afrika
vinaweka mbele itikadi za kisiasa wakati wa kujadili na kuamua hoja
zinazohusiana na wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na
rasilimali za umma serikalini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali nchini
(PAC), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) licha ya kuunga mkono
uwepo na umuhimu wa kamati za vyama bungeni kwa nia ya kulinda nidhamu,
msimamo wa pamoja, itikadi na sera, lakini anasema masilahi ya umma
unapaswa kuwekwa mbele kwenye kila jambo.
“Kamati za vyama zihusike kulinda masilahi ya umma
badala ya vyama. Vyama vya siasa vitakuja na kuondoka lakini taifa na
masilahi ya umma vitadumu milele,” anasema Zitto.
Anawashauri wabunge wote kutumia kwa tahadhari
masilahi yao wakati wa kujadili na kupitisha uamuzi bungeni ili mwishowe
taifa na umma viwe vimenufaika.
Zitto anataja aina tatu za masilahi ya wabunge kuwa ni masilahi
ya taifa, masilahi ya jimbo (wapigakura) na masilahi binafsi (utashi) na
kusema masilahi ya umma yanastahili kuwa juu ya yote.
Mkutano huo wa SADCOPAC uliohudhuriwa na wajumbe
zaidi ya 300 kutoka nchi 28 ulilenga katika kuwajengea wabunge ambao ni
wajumbe wa kamati za hesabu za Serikali uwezo wa kufuatilia na kusimamia
matumizi sahihi ya fedha na rasilimali za umma.
source: Mwananchi
source: Mwananchi