Na Kelvin Matandiko
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 12:40 PM
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 12:40 PM
Kwa ufupi
Naibu Spika, Job Ndugai alifikia hatua ya
kuagiza Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freemon Mbowe na Mbunge wa
Hai atolewe nje ya ukumbi wa Bunge kwa madai ya ukaidi.
Mpaka sasa kutolewa nje ya ukumbi wa
Bunge kwa wabunge wa upinzani, imeonyesha kuwa uwezo wa kiti cha Spika
umefikia mwisho katika kutafakari uamuzi wake
Tangu kuchaguliwa kwa Spika Anne Makinda na naibu
wake Job Ndugai kuongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiti
hicho kimeonekana kuwa na changamoto nyingi katika kila kikao cha Bunge
kinachofanyika Dodoma.
Takwimu zinaonyesha mpaka sasa kuna zaidi ya rufaa kumi za malalamiko dhidi ya uongozi na kiti cha Spika.
Rufaa hizo zimefikishwa kwenye uongozi wa kamati
ya kanuni na hadi sasa hakuna hata moja iliyowahi kujadiliwa na kutolewa
uamuzi.
Katika mwendelezo wa matukio ndani ya Bunge hilo,
Septemba 5, mwaka huu, mvutano mkali uliokuwa na dalili mbaya uliibuka
ndani ya Bunge.
Naibu Spika, Job Ndugai alifikia hatua ya kuagiza
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freemon Mbowe na Mbunge wa Hai
atolewe nje ya ukumbi wa Bunge kwa madai ya ukaidi.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya wabunge wote wa
vyama vya CUF, Chadema na NCCR- Mageuzi kusimama na kuendeleza msimamo
wao wa siku moja awali kupinga kuendelea kwa mjadala wa Muswada wa
Sheria wa Mabadiliko ya Katiba na badala wakitaka usitishwe baada ya
kubainika kuwa na udhaifu.
Katika muswada huo, mbali na hoja za Chadema, hoja
kuu nyingine iliyokuwa imeteka Bunge ni kukamilika kwa muswada huo bila
kuwashirikisha Wazanzibari.
Kutokana na mwendelezo wa mivutano hiyo, mitazamo
mbalimbali imekuwa ikijadiliwa huku baadhi wakidai kuwa ni afya na
ukomavu wa Bunge hilo.
Aidha, makundi mengine yamekuwa yakitoa lawama zake kwa viongozi wa kiti hicho, Spika Makinda na msaidizi wake, Ndugai.
Hata hivyo, Ndugai amekuwa akinukuliwa katika
vyombo vya habari akisema kuwa sababu kubwa ya kuwapo kwa vurugu hizo
bungeni ni utovu wa nidhanmu unaoonyeshwa zaidi na wabunge wa kambi ya
upinzani.
Kutokana na mazingira hayo ya Bunge, baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanaona sababu na mwelekeo wa
Bunge hilo kwa sasa unatupeleka pabaya.
Ukiukwaji wa kanuni
Moja kati ya sababu zinazodaiwa kuwepo kwa
mivutano hiyo ni pamoja na ukiukwaji wa kanuni. Hatua hiyo imekuwa ni
wimbo ndani ya Bunge hilo.
Akizungumza juu ya hilo, Julius Simbeye ambaye
ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es Salaam anasema Spika na
naibu wake wameshindwa kusimamia hata kanuni za Bunge kwa sababu ya
kuendekeza itikadi za vyama.
“Mfano mzuri unakumbuka wakati Bunge la Bajeti ,
mjadala wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Aprili 18 kulikuwa na matusi
yasiyostahili kusikika mbele ya watoto sebuleni, wabunge tusiotarajia
kutukana , mfano Juma Nkamia Peter Serukamba, Mchungaji Peter Msigwa ni
aibu sana,” anasema Simbeye.
Simbeye anasema kutokana na ukiukwaji wa kanuni
unaoruhusiwa na kiti cha Spika, udhaifu unaotokana na mivutano isiyokuwa
na tija imezidi kuongezeka.
“Spika anakosa nguvu, labda ni kwa sababu
ameonekana kutumwa, wanaotukana matusi ni wote, lakini anajikuta
anashindwa kusimamia kanuni na kutumia uamuzi ya kimabavu,”anasema
Simbeye.
Uamuzi ya kimabavu
Mpaka sasa kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge kwa
wabunge wa upinzani, imeonyesha kuwa uwezo wa kiti cha Spika umefikia
mwisho katika kutafakari uamuzi wake.
Naibu Spika (Ndugai) ndiye ambaye amekuwa akitumia adhabu hiyo mara kwa mara.
Mfano, katika Bunge la Bajeti alifukuza wabunge wa
Chadema kutohudhuria vikao kwa siku tano. Mbali na hilo wiki iliyopita
aliagiza askari kumtoa nje kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani, Freeman
Mbowe kwa madai ya kuongoza mgomo wa kuendelea na mjadala wa Bunge.
Akisisitiza juu ya hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Raia ya kufuatilia Utendaji wa Bunge (CPW),Marcossy Albanie anasema
matumizi ya adhabu hiyo mara nyingi yamekuwa yakitumika kibabe na
kinyume cha kanuni.
“Hakuna kipengele cha kanuni kinachobainisha
ukomo kwa mbunge kuomba taarifa pale anapoona mbunge mwingine
amezungumza jambo lisilokuwa na ukweli, lakini Lissu ametolewa nje
baada ya kuomba taarifa kwa madai ya kuomba mara nyingi, ” anasema
Albanie.
Uwezo wao
Mfanyabiashara wa Mwanza, Merick Masuke anaongeza
kuwa vurugu hizo zinasababishwa pengine na uwezo mdogo wa viongozi hao
katika kukabiliana na hoja za wabunge machachari.
Anasema Bunge la sasa ni tofauti na lile la miaka
10 iliyopita ambapo kuna idadi kubwa ya wabunge wenye uwezo mkubwa wa
kuchambua mambo na wazalendo.
“Ukiangalia uwezo wa wabunge vijana kama vile,
John Mnyika, January Makamba, Zitto Kabwe na wengine wanaonekana kuwa na
uwezo mkubwa wa kujenga hoja zinazomshinda Spika kuzikabili,” anasema
mfanyabiashara huyo.
Kulinda maslahi ya chama.
Sababu nyingine ya vurugu hizo inadaiwa kuwa ni
kutokana na propaganda za kisiasa zilizofanikiwa kuliteka Bunge hilo.
Hatua hiyo imesababisha kuwepo kwa ukandamizaji wa hoja binafsi za
wabunge.
Asasi za Kiraia zikiwamo Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu na The Citizens’ Parliament Watch(CPW), Februari 13 mwaka
huu zilitoa tathmini ya mwenendo wa Bunge hilo ambapo moja kati ya
sababu ilizotaja ni kuzimwa kwa hoja nyingi za wabunge.
Asasi hizo zilieleza kuwa Bunge limekuwa likivunja hoja mbalimbali za wabunge kwa kuangalia maslahi na mitazamo yake.
“Kuna baadhi ya wabunge waliotoa hoja binafsi
zenye maslahi kwa taifa lakini Bunge likazivunja, hiyo siyo haki na
utaratibu wa kibunge lenye kufuata misingi ya kidemokrasia,” ilinukuu
sehemu ya ripoti yake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Gaudence Mpangala anaongeza kuwa hatua hiyo ina mipango ya kujihami na
hatari ya kupoteza nguvu ya chama chake na uaminifu alionao ndani ya
chama na serikali.
“Hatupaswi kuwalaumu Spika na naibu wake wametumwa
tu, kwanza wanahofia yasiwatokee kama ya Samweli Sitta, wanaporuhusu
zaidi hoja za wapinzani ndivyo wanavyozidi kupoteza umaarufu wa CCM. Kwa
hiyo akifuata haki, lazima atakuwa kinyume na CCM, ” anasema Profesa
Mpangala.
Kutokubali mabadiliko
Profesa Mpangala anasema uamuzi wa kiti cha Spika umekuwa
ukidhihilisha wazi kutekwa na misimamo ya serikali. Aidha, anasema
kutokana na hoja mbalimbali za kambi ya upinzani, mwonekano huo ni
matokeo ya serikali iliyobakia na chembechembe za utamaduni wa chama
kimoja.
“Kuna sababu za kihistoria, kama kuna maovu na
uchafu utakaoendelea kuibuliwa na upinzani, hali hiyo inaweza kuiathiri
serikali, lakini upinzani wao watakuwa wananufaika. Kwa hivyo mambo haya
yanawajengea wapinzani umaarufu wa kisasa,” anasema .
source: MWANANCHI
source: MWANANCHI