Wednesday, 11 September 2013

MADAWA YA KULEVYA: Matumla: Mkwanda ameifedhehesha familia

 Bondia Rashid ‘Snake man’ Matumla  

Na Imani Makongoro, Mwananchi

Posted  Jumatano,Septemba11  2013  saa 9:55 AM
Kwa ufupi
Mkwanda ambaye kwa mujibu wa Rashid alipumzika kucheza ngumi miaka kadhaa iliyopita kutokana na kusumbuliwa na  maradhi alikamatwa wiki iliyopita nchini Ethiopia akiwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki na leo watapandishwa kizimbani nchini humo kwa tuhuma hiyo.


Mkwanda amewahi kugombea ubingwa wa dunia wa IBF kwa vijana mara mbili.
Dar es Salaam: Bondia Rashid ‘Snake man’ Matumla amedai endapo itathibitika mdogo wake, Mkwanda anajihusisha kusafirisha dawa za kulevya atakuwa ameipa fedheha familia yao.
“Mkwanda ameipa fedhea familia yetu, hii ni aibu kubwa ukizingatia vitendo hivyo vinakatazwa si Tanzania tu bali na kwenye nchi nyingine,” alisema Matumla jana katika mahojiano na gazeti hili.
Mkwanda ambaye kwa mujibu wa Rashid alipumzika kucheza ngumi miaka kadhaa iliyopita kutokana na kusumbuliwa na  maradhi alikamatwa wiki iliyopita nchini Ethiopia akiwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki na leo watapandishwa kizimbani nchini humo kwa tuhuma hiyo.
“Mimi mwenyewe nashangaa ni lini amejiingiza kwenye kazi hiyo, hata wakati anaondoka hakuniaga, mimi kaka yao na familia hatuelewi chochote,” alisema Matumla.
Alisema mdogo wake huyo alikuwa amebadilisha uraia na kuchukua uraia wa Sweden na kuoa hukohuko Sweden licha ya kwamba hapa Tanzania alikuwa amepanga Mbagala, Dar es Salaam na alikuwa anakuja na kukaa kwa muda na kisha kuondoka.
“Ni mwezi sasa umepita sina taarifa naye na hata wakati anaondoka hakuniaga, nimesikia kupitia vyombo vya habari kitendo cha mdogo wangu kukamatwa kimenisikitisha mno, siyo siri nimekwazika na ninarudia kusema hii ni fedheha kwenye familia yetu,” alisema bingwa huyo wa zamani wa dunia wa WBU. Rekodi zinaonyesha kabla ya kupumzika kwa muda kucheza ngumi, Mkwanda alishinda mapambano manane (sita kwa KO) alipigwa mara tatu zote kwa KO alitoka sare mara moja tangu 2004.