Posted Alhamisi,Agosti29 2013 saa 20:56 PM
Kwa ufupi
Askofu Kulola ameacha mke wake aitwaye
Elizabeth, ambaye alibarikiwa kupata naye watoto 10 na wengine wawili wa
kuasili. Hata hivyo, watoto watatu walishafariki dunia. Ameacha wajukuu
44 na vitukuu 10.
Dar es Salaam. Vilio, simanzi na maombi ya
kunena kwa lugha vilitawala jana katika Kanisa la Evangelistic
Assemblies of God Tanzania (EAGT), Temeke Dar es Salaam wakati waumini
na ndugu wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Moses Kulola (83) walipopata
taarifa za kifo cha kiongozi huyo.
Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile alisema
kuwa Askofu Kulola alifariki dunia jana saa tano asubuhi kwenye
Hospitali ya Africa Medical Invesment (AMI), Dar es Salaam.
Mwakipesile alisema afya ya Askofu Kulola ilianza
kubadilika Mei mwaka huu akiwa mkoani Mwanza ambako alipelekwa Hospitali
ya Rufaa Bugando ambako alibainika kuwa na matatizo ya moyo.
“Kanisa liliamua kuchukua jukumu la kumpeleka
Hospitali ya Apollo, India kwa matibabu zaidi na baada ya kuona afya
yake inatengemaa aliruhusiwa kurejea nchini, lakini Agosti 16, mwaka huu
hali ilibadilika ndipo tukampeleka AMI alikofikwa na mauti,” alisema
Mwakipesile.
Alisema kifo hicho kimeacha pengo kubwa ambalo
haliwezi kuzibwa kwa sasa. Hata hivyo, wanafarijika kwa upande mwingine
wakiamini kwamba Mungu amemchukua mtumishi wake kwa wakati alioukusudia.
Alisema mwili wa Askofu Kulola utasafirishwa
kwenda Mwanza Jumamosi jioni kwa ndege baada ya kuagwa kanisani hapo.
Atazikwa kwenye Uwanja wa Kanisa la EAGT Bugando.
Askofu Kulola ni mmoja wa viongozi wa dini
waliokuwa na jina kubwa nchini na alifanya kazi za utumishi wa kanisa
kwa miaka 53 kwa kuhubiri na kuwaombea wenye matatizo mbalimbali.
Mtoto wa kwanza wa askofu huyo, Goodluck Kulola
alisema wamejifunza mambo mengi katika maisha ya baba yao, ikiwamo
upendo na unyenyekevu ulioongozwa na uchaji Mungu.
“Baba alikuwa ni asiyependa kabisa migogoro ya
kidini, kisiasa yaani ikitokea hali ya uvunjifu wa amani wa namna yoyote
ile alikuwa anaumia sana. Alipenda watu kwa ujumla ametufundisha
upendo.”
Askofu Kulola ameacha mke wake aitwaye Elizabeth,
ambaye alibarikiwa kupata naye watoto 10 na wengine wawili wa kuasili.
Hata hivyo, watoto watatu walishafariki dunia. Ameacha wajukuu 44 na
vitukuu 10.
Askofu Kulola, ambaye alizaliwa 1928, alianza
Shule ya Misheni ya Ligsha Sukuma mwaka 1939, baadaye alijiunga na Shule
ya Bwiru kabla ya kusomea Usanifu Majengo huko Israel kisha kuanza kazi
ya kumtumikia Mungu mwaka 1950.
Alifuzu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia katika Chuo Kikuu cha California State Christian Marekani.
Aliwahi kutumika kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God
(TAG) mwaka 1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la EAGT lenye
matawi katika nchi za Zambia, Malawi, Burundi na Msumbiji.
Rais Jakaya Kikwete jana alituma salamu za rambirambi kutonana na kifo cha Askofu Kulola.
source: Mwananchi
source: Mwananchi