Thursday 29 August 2013

Makinda apigiwa debe urais


Na Boniface Luhanga, 29th August 2013
                                      
                                              Spika wa Bunge,Anne Makinda.
Mbio za kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza kuchukua sura mpya, baada ya baadhi ya vigogo kujitokeza hadharani kumpigia debe Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Vigogo hao ambao wana ushawishi ndani ya CCM walishindwa kujizuia na kulazimika kumpigia debe Makinda ndani ya ukumbi wa Bunge jana, huku wakimwagia sifa za kuwa Rais wa Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kikatiba.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, alimmiminia sifa Makinda  kuwa anafaa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) na waziri kwenye serikali ya awamu ya pili na ya tatu kwa miaka kadhaa, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akiunga mkono hoja ya Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Afrika (CPA) tawi la Tanzania Mussa Azzan Zungu, kumpongeza Spika Makinda kwa kuteuliwa kwake kuwa Rais wa chama hicho Afrika.

Akichangia hoja hiyo, Anna Abdallah, ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa katika utawala wa awamu ya kwanza, alisema uteuzi wa Spika Makinda, siyo heshima kwake tu bali ni kwa Watanzania wote, lakini hasa kwa wanawake.

Alisema haoni sababu ya kwa nini Spika Makinda sasa asigombee CPA ngazi ya kimataifa kwani yeye pamoja na Watanzania na wabunge kwa ujumla watamuunga mkono.

 Alisema kwa msingi huo, anamshauri Spika Makinda kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha ndani na nje ya nchi kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa upande Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, wa Rungwe Mashariki, alisema Spika Makinda amekuwa mfano mzuri wa kuigwa kutokana na uongozi wake tangu akiwa mkuu wa mkoa, mbunge, naibu waziri, waziri kamili, naibu spika na sasa spika.

Profesa Mwandosya ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki akiwa amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 na kuishia kwenye nafasi ya tatu bora kabla ya yeye na Dk. Salim Ahmed Salim kubwagwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye mkutano mkuu wa CCM, alimwelezea Spika Makinda kuwa ni mtu mwadilifu, mtenda haki, anayejiamini, mvulimivu, mnyenyekevu, msikivu na mwenye msimamo, hivyo hashangai kupitia yeye (Spika), Bunge lijalo hata bila ya Katiba mpya, wanawake watafikia asilimia 55 katika Bunge.

Profesa Mwandosya alisema hiyo inatokana na ukweli wa historia yake ya kiungozi wasichana wengi sasa wanataka kuwa viongozi, lakini pia wanawake wengi watajitokeza kugombea ubunge.

Hata hivyo, Profesa Mwandosya hakutaja moja kwa moja kama Spika Makinda anapaswa kugombea urais mwaka 2015, isipokuwa alisema kwa wale wanaofikiria 2015 watambue kwamba (Makinda) ni tishio kwao.

Kupigiwa debe kwa Makinda kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kunaongeza idadi ya makada wa CCM wanotajwa kuwania uteuzi wa chama hicho tawala.

Hadi sasa wanaotajwa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Makinda alichaguliwa kuwa Spika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Sitta tangu mwaka 2005.

Sitta alishindwa kutetea nafasi yake baada ya CCM kutoa maelezo kuwa ulikuwa wakati mwafaka kwa nafasi hiyo ya juu kushikwa na mwanamke.

Mwaka 1995 wakati kwa mara ya kwanza Kikwete na Lowassa walijitokeza hadharani kwa pamoja wakiendesha harakati za kuwania urais, Makinda naye akikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliokuwa pamoja nao na alifika uwanja wa ndege siku wawili hao (Kikwete na Lowassa) walipokodi ndege kutoka Dar es Salaam kwenda kuchukua fomu za kuwania urais kupitia CCM makao makuu Dodoma.

Ingawa haijawekwa wazi juu ya harakati za kisiasa za Makinda, wakati anawania nafasi ya uspika hakuna aliyejua kuwa ana mpango huo, hadi vyombo vya habari vilipofichua kwamba naye alikuwa amejitokeza kuchukua fomu kimya kimya.

Alipoulizwa juu ya kuchukua fomu hizo kuchuana na bosi wake (Sitta) alisema kuchukua fomu siyo hoja, ila hoja ni kama atairudisha.

Kwa mshangao wa wengi, Sitta ambaye alikuwa amejitwalia sifa kemkem alivyokuwa ameendesha Bunge la tisa, akitajwa kama spika wa kasi na viwango, jina lake halikurudi baada ya Kamati Kuu ya CCM chini ya Rais Kikwete kuamua kuwa nafasi ya uspika ilikuwa zamu ya mwanamke.
CHANZO: NIPASHE