Posted Jumatatu,Agosti26 2013 saa 22:3 PM
Kwa ufupi
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba alizindua Rasimu ya
Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba
kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika Agosti
31, mwaka huu.
Dodoma. Historia inatarajia kuandikwa katika
Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaoanza leo, mjini Dodoma
wakati litakaposafisha njia kwa Watanzania kwa mara ya kwanza, kupiga
kura ya maoni ya Katiba.
Bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Kura ya
Maoni 2013, ambao ndiyo utakaotoa njia kwa Watanzania kuamua Katiba Mpya
baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania Bara kupiga kura ya
maoni ya aina yoyote ile tangu Uhuru mwaka 1961 na
ya pili kwa Zanzibar ambayo ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka
2010 kutoa nafasi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuelekea mchakato huo wa Katiba Mpya, Bunge pia
litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba wa mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na safari ndefu ya mchakato
wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi iliyoanza Aprili 13, mwaka jana kwa
Rais Jakaya Kikwete kuzindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji
Joseph Warioba.
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba alizindua Rasimu
ya Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa Mabaraza ya
Katiba kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika
Agosti 31, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, Bunge litapelekewa maboresho
ya mapendekezo ya rasimu hiyo na kuyajadili ikiwamo kupitisha sheria ya
mabadiliko hayo na baadaye kuweka muundo wa sheria na muundo wa kupigiwa
kura hatua itakayofuata katika Bunge la Katiba baadaye Novemba, mwaka
huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya
Bunge, hoja hizo mbili zimetengewa siku tano kuanzia Septemba 9 hadi 13,
mwaka huu na mjadala wa marekebisho hayo unatarajiwa kuchukua nafasi
hasa kwa wabunge wa pande mbili, CCM cha Chadema juu ya kutengeneza
muundo.
Chadema, kimeshatoa baadhi ya mapendekezo yake
katika muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kura
ya Maoni ikiwamo kupinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu
wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
source: Mwananchi
source: Mwananchi