Wednesday, 26 March 2014

MKANGANYIKO JUU YA NDEGE YA MH 370 AIR MALYASIA ILIYOPOTEA

Na.
Dezidery Kajuna
 
Neno mkanyinko utumika mara kwa mara, lakini je umewahi kuwa na mkanganyiko juu ya jambo lolote? Vipi kuhusu MH 370? Sasa ni dhahili kuwa kupotea Kwa ndege ya MH370 ya huko nchini Malyasia inazidi kulete mkanganyiko mbaya zaidi kuwahi kutokea katika ajali za ndege tokea huko nyuma.

 
Ni zaidi ya majuma matatu sasa ndege haijaonekana au walau kujulikana ilikopotelea. Si sayansi wala uchawi ambao umeweza kutuletea jibu la kitendawili hiki. Ni tukio kubwa na la kusikitisha pengine kutokana na aina ya ndege. Ijulikane kuwa MH370 si ndege ya kwanza kupotea, ziko taarifa na historia za ndege kupote katika mazingira ya aina mbali mbali.
 
Lakini MH370 mbali kuwa ndege tu, imetengenezwa tofauti, imesheheni mifumo ya kompyuta ambayo usaidia kutoa taarifa mbali mbali. Ni moja ya ndege za kisasa kuwahi kutengenzwa katika ulimwengu wa sasa. Hata hii nayo imekumbwa na balaa hili la ndege kupotea bila kujali mifumo ya kisasa iliyopo ndani yake. Ni ajabu na wengi tumebaki kwenye mkangayiko.
 
Tanzania, Kwa mfano kuna matukio zaidi ya kumi ndege kupotea tokea enzi za ukoloni mpaka enzi hizi za sayansi na teknolojia. Ni vigumu kuelewa Kwa kina nini haswa upelekea ndege hizi kupotea. Lakini bila shaka wataalamu wa anga na wale mainjinia wa ndege wanayo majibu ya kutosha juu ya dhoruba za namna hii.
 
Wahenga husema " Msema kweli ni mpenzi wa Mungu" ngoja niliseme hili kutoka moyoni mwangu, sikuwahi kudhani kuwa usafiri wa anga unaweza kuwa ana ajali za kutisha. Pengine ilifika mahala nikajisemea maisha bora ni yale ya kupanda ndege hata kama unatoka dar kwenda kibaha, nikiamini ndege hizi ni salama  salimi, yaani hazipati ajali.
 
Hata hivyo imani niliyokuwa nayo miaka mingi imepotea na inazidi kufifia kabisa. Hakika sina shaka hakuna usafiri ulio salama. Ni Mungu pekee awezaye kutulinda dhidi ya ajali hizi. Nachomaanisha hapa ni kwamba kuanzia, boda boda, bajaj, landcruise, mabasi, treni, mpaka ndege hakuna usalama tena. Hata wale wachawi wanao tumia ungo nao upata ajali, ungo zao udondoka na kupoteza mwelekeo wa safari zao na hawa ndio upata mkanyiko zaidi ya wale wa boda boda.
 
Kuna taarifa  kutoka Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania ambapo Mkaguzi mkuuu alitoa taarifa na historia ya ndege zilizo wahi kupotea Tanzania. Habari hizi  zilichapishwa kwenye gazeti la tarehe 25 mwezi wa tatu. Nina nukuu kutoka kwenye gazeti hilo
 
"Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, , David Nyamwihura alisema katika mahojiano maalumu kuwa ripoti hiyo inaonyesha kuwa idadi kubwa ya ajali hizo hutokea maeneo ya milimani. sababu kubwa ni hali mbaya ya hewa na ukosekanaji wa vyombo vya kuangalia hali ya hewa,” alisema Nyamwihura"
 
Lakini Je ndege hizi zilipatikana?
Ifuatayo ni idadi ya  ajali za ndege 10 zilizowahi kutokea Tanzania na idadi ya vifo vilivyotokea.
 
1. DC -3- Machi 18, 1955
Hii ndiyo ajali mbaya zaidi ya ndege kuwahi kutokea katika anga la Tanzania, ikihusisha ndege DC-3 ya Shirika la Ndege ya Afrika Mashariki. Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Kilimanjaro na kuua watu 20.
2. Vickers Viking-Machi 29, 1953
Ajali ya pili ni ile iliyohusisha ndege aina ya Vickers Viking mali ya Shirika la Ndege la Afrika ya Kati iliyotokea eneo la Mkuyuni, Handeni ambapo watu 13 walifariki dunia.
3. Cessna 404-Septemba 9, 1999
Hii ni ya tatu ambayo ilihusisha ndege ya Shirika la Northern Air, aina ya Cessna 404. Ajali hiyo iliyotokea eneo la Mlima Meru, Arusha, ilisababisha vifo vya watu 12.
4. Cessna 402b-Agosti 12, 1976
 Cessna 402B ya Shirika la Safari la Air Nairobi. Ajali hiyo iliyotokea katika Ziwa Victoria, Mwanza, watu 10 walipoteza maisha.
 
5. IL76-TD Machi 23-2005
Ajali ya tano kwa wingi wa vifo, iliua watu wanane katika Ziwa Victoria, mkoani Mwanza. Ilihusisha ndege aina ya IL76-TD, mali ya Shirika la Air Trans Inc, Moldova.
6. Piper PA 32-300 Agosti 26, 1972
Ajali ya sita ni ile ya ndege aina ya Piper PA 32-300 inayomilikiwa na Shirika la Ndege la K. Downey and Selby la Nairobi iliyoanguka katika anga la Dar es Salaam eneo la Kijiji cha Mkamba. Watu saba walipoteza maisha.
7. Piper PA 32-300 Agosti 15, 1978
Ajali namba saba ilihusisha ndege aina ya Piper PA 32-300 mali ya Shirika la Amphibian Mombasa. Katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Tarakea, Mlima Kilimanjaro, watu saba walipoteza maisha.
8. Piper PA 23-250 Machi 30, 1970
Mwaka 1970 nao ulishuhudia ajali ya nane kwa ukubwa ya ndege aina ya Piper PA 23-250 mali ya Shirika la Tim Air, Tanzania katika eneo la Mafi Hill, Mombo ambapo watu sita walipoteza maisha.
9. Piper PA 23-250 Juni 2, 1979
Ajali ya tisa iliyotokea Juni 2, 1979, ilisababisha vifo vya watu watano na ilitokea eneo la Kambi ya Jeshi la Mgambo, Tanga. Ajali ilihusisha ndege aina ya Piper PA 23-250 mali ya Shirika la Tanzanair, Dar es Salaam.
 
 
10. Cessna 185-Oktoba 10, 1986
Ajali ya 10 mbaya zaidi ni ya mwaka 1986 iliyotokea katika eneo la Hombolo, Dodoma, ambapo ndege ya Shirika la NORAD, aina ya Cessna 185 ilianguka na kusababisha vifo vya watu watano.
 
Zipo ajali nyingine nyingi zilizowahi kutoka baada ya hiyo ya mwaka 1986.
Taarifa hizi zimenukuliwa kutoka gazeti la Mwananchi.
 
 
Turudi kwenye mada, Kwa mtiririko huo ajali za ndege utokea na uwezekano wa ndege kutoonekana ni mkubwa kutokana na eneo ndege ilipoangukia au kupotelea.
 
MH370 ni jinamizi ambalo halitasaulika, shirika la utangazaji la BBC linasema mataifa makubwa kama marekani , Ufarance, Ujeruman, China,  na Australia sasa yamejikita katika kutafuta mabaki ya ndege hiyo. Lakini utafutaji huo upo kimashindano, ni juu ya nani atakuwa wakuanza kupata mabaki ya ndege hiyo au kujua wapi ilikotokomea.
 
Walianza wachina wakasema tumeona vitu mifano ya mabaki ya ndege hiyo lakini satelaiti zao nadhani ziliwadanganya, wakaja waaustralia nao naona wanasema hali ya hewa imekuwa mbaya wakasitisha na baadae hali imetengemana na sasa wanaendelea.
 
Ikiwa siku zinakwenda, hatimaye waziri wa uchukuzi wa Malaysia pamoja na Waziri Mkuu walitangaza kuwa ndege hiyo imepotea kabisa baada ya kugundua mahali ambako wanahisi ndege ilimalizia mwendo Wake. Taarifa Kwa ndugu wale 239 zilitolewa bila shaka wafanye matanga bila kuwepo Kwa miili ya jamaa zao.
 
Kule China kumekuwa na maandamano na vurugu nyingi juu ya watu 150 kutoka taifa hilo kuhofiwa kupoteza maisha. Waandamaji hawa wanataka majibu kutoka serikali ya Malysia juu ya taarifa za ndugu zao, ni mkanyiko huu.
 
Ikiwa hazijapita siku nyingi nchi ya Ufaransa inasema imeona vitu zaidi ya 122 ambavyo bila shaka ni mabaki ya ndege hiyo, huu ni mkanganyiko. Swali ni je wale ndugu waliopokea taarifa za ndege kupotea kabisa wasitishe shughuli za misiba?
 
Je ni nani wa kumwamini katika hili? Serikali ya Malysia au vyombo vya usalama vya nchi zinazosaidia kutafuta ndege hii, yaani ni mkanyiko! Nasema ni mkanganyiko kweli kweli.
 
Kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kubashiri kuwa ndege hii imetekwa na magaidi, labda wana fanya jaribio la kuteka ndege, na hili ni jaribio tu, likifanikiwa basi watakuwa wametengeneza njia mbadala wa kupambana na maadui wao. Ubashiri huu nao ni mkanganyiko kwangu!
 
Kuna bilionea mmoja wa kule nchini Uingereza ambaye anamiliki vyombo vya habari vikubwa duniani Rupert Murdoch, yeye anasema ndege ipo kati ya pakistani na afghanistani imetekwa na magaidi. huyu naye anatupa mkanganyiko, sasa tumwamini nani? Nasema ni mkanganyiko kweli kweli!
 
Lakini Je unaombolezaje msiba wa mfu asiyekuwepo? Yaani ni mkanganyiko kweli kweli!
 
Tukutane wiki ijayo katika makala nyingine!