Kwa ufupi
Alisema Waislamu wengi waliotoa maoni yao
kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitaka kuwapo kwa mahakama hiyo
lakini cha kushangaza tume hiyo iliyatupa.
Dar es Salaam. Wajumbe wa
Baraza la Katiba la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, wametaka
kipengele cha Mahakama ya Kadhi kiwekwe kwenye Katiba Mpya.
Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za
Kiislam, Sheikh Mussa Kundecha, alisema jana kuwa ingawa rasimu ya
Katiba haina kupengele hicho, lakini wao wanaona hiyo ni haki yao.
“Tunataka kipengele cha Mahakama ya Kadhi kiwekwe
Katiba Mpya na iendeshwe na kugharamiwa na Serikali,” alisema Sheikh
Kundecha wakati wajumbe hao walipokuwa wakijadili rasimu ya Katiba.
Alisema Waislamu wengi waliotoa maoni yao kwenye
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitaka kuwapo kwa mahakama hiyo lakini
cha kushangaza tume hiyo iliyatupa.
“Sasa licha ya kwamba kipengele hicho hakipo kwenye rasimu, bado tunaendelea na kilio chetu cha kutaka kiwekwe,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba, wiki iliyopita alisema kipengele ambacho
hakipo kwenye rasimu hakitawekwa kwenye Katiba Mpya.
Sheikh Kundecha alihoji iweje kuwe na Mahakama za
Biashara inazoendeshwa na Serikali, wakati kuna Watanzania wachache
ambao ni wafanyabiashara.
“Kuna wafanyabiashara wachache lakini wana
mahakama yao, kunakuwa na ugumu gani kuweka Mahakama ya Kadhi kwa ajili
ya Waislamu?” alihoji Kundecha. Mwaka jana, Serikali iliruhusu
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ambayo iko nje ya mfumo wa Serikali.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper