Kwa ufupi
- Kagame alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na RPF.Ufaransa ikimsaidia Habyrimana na Marekani ikiwasaidia RPF
Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton,
hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za
kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC.
Kwa muda wa miezi takriban minne kumekuwa na
maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika maneno hayo
yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi za juu katika
Serikali yake.
Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais Jakaya Kikwete
kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu waliokimbilia
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji
ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.
Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu 800,000 wenye
msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu hizo zina utata,
kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa na idadi ndogo ya
watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.
Pia, wapo wale ambao wanaweza kushangaa kwa nini
Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania, nchi ambayo imekuwa
mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya 1960 na kwa nini
Rais Kikwete alitoa ushauri huo.
Kagame hakupendezwa na ukweli huo kwani kila mara
amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano yanayoendeshwa na
vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila inapotokea hali
kutulia.
Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa muda mrefu
kwani amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka kumi na
amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila mafanikio kwa
sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na kudai kuwa
kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho kinaanzisha
mapambano dhidi ya serikali.
Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa
Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo kabla
hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea Rwanda
baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake
ulirushiwa nyanya.
Hiyo ilikuwa ni kama kumpa ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati ule Watutsi walipouawa na Wahutu mwaka 1994.
Masikini! Annan angefanya nini wakati alipokuwa
akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji kila moja
lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa uchelewashaji
wa makusudi.
Baadaye Annan alipokuwa akigombea Ukatibu Mkuu wa
UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo iliyopinga na hata
alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo iliyokuwa kinara wa
kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa yakifanyika wakati
huo Kagame alikuwa akiyajua.
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Meja Jenerali
Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza
(BBC) akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa vikundi vyote
vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha kuwa Wahutu na
jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa linaundwa na
waliokuwa vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.
Kwa maneno mengine, Kagame ameifanya ardhi ya DRC kama uwanja wa
mapambano kati yake na wapinzani wake ambao wako mashariki mwa nchi
hiyo.
Jenerali Nyamwasa, ambaye kabla ya kukimbilia
Afrika Kusini alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India anasema kuwa Kagame
ndiye aliyeamrisha kutunguliwa kwa ndege iliyokuwa imebeba ujumbe wa
nchi hiyo pamoja na Rais Juvenal Habyarimana na Cyprian Ntyaramira wa
Burundi ambao ulikuwa umetokea Tanzania kwenye mkutano wa kujadili amani
ya nchi hiyo.
Baada ya vita kumalizika na hatimaye RPF kuchukua
uongozi, Ufaransa, mtawala wa zamani wa Rwanda ilimtuhumu Kagame kwa
kusababisha mauaji ya kimbari kwani Wahutu wasingianzisha chinja chinja
ya Watutsi kwa wakati huo kwani mazungumzo yale yalikuwa yanaelekea
ukingoni na hatua ya mwisho ingekuwa kwa RPF kuwa chama cha kisiasa
ambacho kingeshiriki kwenye uchaguzi.
Nia ya Kagame ilikuwa ni kuchukua uongozi Rwanda
kwa nguvu kwa sababu kwa mizania ya siasa za nchi hiyo ambazo zimejikita
zaidi kwenye ukabila ingekuwa vigumu kwa Watutsi walio wachache
kushinda.
Sababu ya pili ambayo ndiyo iliyowafanya RPF
wakatae au watumie nguvu ilikuwa ni juhudi ya Marekani ambayo ilikuwa
mfadhili mkuu wa RPF kuhakikisha kuwa ushawishi wa Ufaransa katika eneo
la Maziwa Makuu unaondoshwa kwa gharama yoyote.
Hii inathibitishwa katika kitabu Global
Intelligence; the world’s secret services today ambacho kimeandikwa na
waliberali, Paul Todd na Jonathan Bloch.
Waandishi hao wanabainisha kuwa wakati huo
kulikuwa na vita vya kijasusi baina ya Marekakani na Ufaransa ambavyo
baadaye vilibadilika na kuwa ni vita vya kijeshi.
Kagame alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na RPF.
Ufaransa ikimsaidia Habyrimana na Marekani
ikiwasaidia RPF ambao tayari walikuwa wakisaidiwa na Uganda walijipatia
taarifa za kijasusi kutoka kwa Serikali ya Rwanda na wapiganaji wake.
Majasusi wa Marekani ambao walikuwa wakitumia njia
za kijasusi za siri za kunasa taarifa za mawasiliano katika eneo la
Afrika Mashariki walifanikisha mipango ya RPF katika uwanja wa
mapambano.
Marekani ilikiri kuwa kuanzia 1994 ilikuwa
ikiwasaidia RPF kwa kuwapatia silaha na Kagame alipewa simu ya satelaiti
aina ya Motorola INMARSAT ambayo licha ya kufungwa kitaalam
(encryption) ili mawasiliano yake yasinaswe na wapiganaji wa Serikali ya
Rwanda au yeyote yule, kwa bahati mbaya shirika la Ujasusi la Kimataifa
la Ufaransa, DGSE (Direction Generale de la Securite Exteriure)
lilifanikiwa kunasa mawasiliano yale na Ufaransa iliituhumu Marekani kwa
kutoa kombora lililoiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana.
Kwa maana nyingine, ni kuwa Kagame hawezi kukwepa
mkono wa sheria wakati utakapofika kwani taarifa muhimu za namna mambo
yalivyokuwa yakienda katika uwanja wa mapambano, mawasiliano yake
yamehifadhiwa na taasisi hiyo ya kijasusi ya Ufaransa.
Waandishi hao wamebainisha kuwa kwa kuwa Rais Mobutu Seseseko wa
Zaire (sasa DRC) alikuwa akimsaidia Jonas Savimbi ambaye Wamarekani
walikuwa wameishamchoka na walimtaka aache vita ili utulivu urejee
Angola, nao wavune madini na mafuta huko wakiwa na sababu ya kumwondoa
Mobutu madarakani ili kukata mizizi ya usaidizi aliokuwa akiupata
Savimbi, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa UNITA, iliyokuwa
ikipigana vita vya msituni dhidi ya Serikali ya Angola chini ya MPLA.
Sababu nyingine ilikuwa kwa Mobutu kuwasaidia
Wahutu ambao walikuwa kipenzi cha Ufaransa ilibidi aondolewe ili
kuhakikisha kuwa Wamarekani wanalishika na kulidhibiti eneo lote la
Maziwa Makuu.
Ikumbukwe kuwa wakati huo Rais Bill Clinton ambaye
hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za
kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC, ndiye aliyekuwamadarakani wakati
huo na alifanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa shughuli za kijasusi
zinaendeshwa katika mtindo ambao utakuwa na manufaa zaidi kiuchumi na
siyo kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa vita baridi.
DRC ilikuwa muhimu kwa majasusi wa Marekani, hasa
kwa uzarishaji wa madini ya coltan ambayo hutumika kutengenezea simu za
mkononi, madini hayo hayapo sehemu nyingine yoyote duniani zaidi ya
DRC.
Clinton alihakikisha kuwa anafanya kila awezalo
kuondoa ushawishi wa Ufaransa nchini Sudan kwa kuwataka viongozi wa SPLA
wakati huo, Kanali John Garang na wengine wadai uhuru kamili na siyo
utawala wa shirikisho kutoka Sudan ili mradi Ufaransa ikose mafuta
yaliyokuwa yakichimbwa kutoka Sudan Kusini.
Waandishi hao wamebainisha kuwa Marekani ilitoa
dola 100 milioni ili kumsaidia Laurent Kabila kuanzisha jeshi la watoto
waliokuwa wakijulikana kama Kadogoo wakiwa na malengo ya kumwondoa
Mobutu.
Kufikia mwaka 1997, Shirika la Kijasusi la
Marekani (NSA) lilikuwa imejenga vituo vya kuendesha shughuli za
kijasusi ili kunasa taarifa za mawasiliano kupitia simu, nukushi, redio
katika sehemu mbalimbali za eneo la Maziwa Makuu kama vile, Fort Portal
nchini Uganda, Kigali Rwanda na Kongo Brazaville.
Ufaransa ambayo ilikasirishwa na jinsi Marekani
ilivyofanikisha kuwaondoa vibaraka wake katika DRC na Rwanda
ilihakikisha kuwa inawaandaa wanajeshi ambao walimpindua Rais Pascal
Lissouba wa Congo Brazaville ambaye alikuwa ni kipenzi cha Marekani.
source: Mwananchi
source: Mwananchi