Kwa ufupi
Tulifahamu kwamba alikuwa anapenda sana
uchapaji wetu wa kazi, mimi na Masoud. Na hapana shaka, alikuwa mmoja wa
wale ambao walichangia kuamua kwamba RTD iwakilishwe kwenye michezo
hiyo ya New Zealand, maana alipenda sana michezo, hasa soka. Alikuwa
“Yanga damu.”
Kwa zaidi ya miaka 40, Tido Mhando amekuwa
akifanya kazi ya utangazaji. Kazi ya mapenzi yake maishani. Akianzia
chini kabisa kama mtangazaji wa salamu hadi kufikia ngazi ya juu kabisa
ya ukurugenzi mkuu. Kwa kipindi chote hiki amefanya kazi hii hapa
Tanzania, Kenya na Uingereza. Kwa hiyo, anasimulia mengi aliyoyaona
wakati wote huo kwenye makala zake hizi za kila Jumapili. Wiki jana,
alihadithia vile mkurugenzi wa RTD siku hizo alipotangaza kwamba yeye
Tido ameteuliwa kufuatana na timu ya wanamichezo wa Tanzania ambao
walikuwa wakienda kushiriki kwenye michezo ya nchi za Jumuiya ya Madola
(Commonwealth) huko New Zealand, mnamo Januari 1974. SASA ENDELEA...
Aliyekuwa mkurugenzi wetu hapo Radio Tanzania Dar
es Salaam miaka hiyo, Paul Sozigwa, alitangaza uamuzi huo wa menejimenti
kwenye mkutano wa watangazaji wote uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1973.
Basi kwa kweli, niliuona mwaka huu kuwa kwa
hakika, ulikuwa mwaka wangu. Kwa maana ndiyo mwaka ambao pia kwa mara ya
kwanza, nilifanikiwa kusafiri nje ya Tanzania; yaani, baada tu ya
kurejea kutoka Uganda, naambiwa tena natakiwa nipae anga za juu zaidi
hadi Christchurch, New Zealand!
Kusema kweli nilifurahi kupindukia. Maana hata
siku moja sikuwa na ndoto ya mapema hivi ya kwenda kule wengine
wanakokuita mwisho kabisa wa dunia, bondeni kuliko bondeni kwenyewe.
Uvuke Bahari ya Hindi hadi kwenye kisiwa hicho kilichopo kwenye Bahari
ya Pacific.
Nilitoka kwenye mkutano huo nikiwa na tabasamu la
kukata na shoka. Marafiki zangu wa karibu wakinitupia vijembe,
wakinitania eti labda nimefanya kazi nzuri ya kufagilia makaburi ya
mababu na bibi kule kijijini Kilulu, Mkuzi, Muheza, ndiyo maana mambo
yananinyookea hivyo.
Nilicheka tu. Ama kwa kweli sikutarajia kwamba
mkutano ule ungetokea kuwa kikao cha kihistoria hivi kwenye maisha
yangu. Kikao cha mafanikio kwangu kuliko nilivyotarajia. Kikao
kilichonifanya nifurahi kuliko maelezo.
Kitu kimoja kizuri siku zile pale RTD ni kwamba,
mtu akifikwa na jambo zuri kama lile, kila mtu alikupongeza. Kulijengeka
siku zile utamaduni mzuri wa kupeana hongera za dhati kwa mwenzenu
aliyefanikiwa. Kwa hiyo, karibu wenzangu wote walinitakia kila la heri.
Tuliokuwa tumechaguliwa kwenda kwenye safari hii
tulikuwa wawili, mimi na mwenzangu Abdul Omar Masoud Jawewa. Hakuwa
rafiki yangu wa karibu hivyo, lakini tulielewana sana. Tulishirikiana na
kushauriana kila ilipowezekana. Tulikuwa tunachangia kutayarisha kwa
zamu kile kipindi maarufu cha saa mbili kasorobo, “Michezo”.
Masoud hakuwepo wakati mkurugenzi Sozigwa
alipotangaza habari zile njema. Kwa hiyo, nikawa namsubiri kwa hamu
afike ili nimpatie mchapo. Ulikuwa mchapo wa nguvu kwelikweli. Sikutaka
apatiwe mchapo huo na mtu mwingine bali mimi mwenyewe; ili tuanze mara
moja kupanga mambo mengine ambayo yangehusu safari yetu. Kwa sababu
hiyo, wakati mwingi nikawa naangalia sehemu za langoni.
Lakini kwa kuwa bado nilikuwa nawajibika kuendelea
na majukumu yangu mengine, nilijisahau na ghafla nikiwa niko maktaba ya
sahani za santuri, nikamsikia Masoud anaulizia jamaa iwapo nimeonekana
huko. Tayari alikuwa ameshapewa nyepesi nyepesi, akawa ananitafuta.
Tuliongea na Masoud kuhusu yapi ya kufanya haraka
haraka, maana siku zilikuwa zimebakia chache, kama mwezi mmoja tu hivi
na palikuwa na mambo mengi ya kufanya, ikiwa ni pamoja na kupata
pasipoti za uhakika maana sote wawili tulikuwa hatuna, ukiacha ile ya
muda tu ambayo mimi nilipewa kwa ajili ya safari ya Uganda.
Tuliamua kwenda wakati huo huo kumwona aliyekuwa
Naibu Mkurugenzi na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Matukio siku hizo,
Sammy Mdee, ili tushauriane naye kuhusu safari yetu.
Sammy
alikuwa mtu wa vitendo, mtu wa chapchap, aliyependa kuwasaidia na
kuwashauri kwa karibu wale wote aliowaongoza. Alipenda mafanikio na
matokeo mazuri. Na yeye, kama Paul Sozigwa, alikuwa mtu mwenye ushawishi
mkubwa serikalini.
Tulifahamu kwamba alikuwa anapenda sana uchapaji
wetu wa kazi, mimi na Masoud. Na hapana shaka, alikuwa mmoja wa wale
ambao walichangia kuamua kwamba RTD iwakilishwe kwenye michezo hiyo ya
New Zealand, maana alipenda sana michezo, hasa soka. Alikuwa “Yanga
damu.”
Kwa hiyo, kama tulivyotarajia, Sammy alitusaidia
sana. Alitupatia na barua ya kupeleka Idara ya Uhamiaji ili tupatiwe
pasipoti haraka haraka, pamoja na maelezo mengine ambayo yangetusaidia
kwenye matayarisho ya safari yetu. Tukaanza mara moja kuchakarika.
Lakini, wakati tukiwa mbioni hivyo, nami nilikuwa
na jambo jingine binafsi ambalo nilikuwa nimepanga kulitekeleza aghalabu
wakati huo huo. Nilikuwa nimeamua kuoa.
Kwa muda wa kutosha, nilikuwa tayari nimeanza
kuona napata pata ile ari ya kufunga pingu za maisha. Kwa kuwa nilikuwa
mtoto wa kwanza wa kiume kwenye familia yetu kubwa, niliona ni vyema
nikachukua heshima yangu hii haraka iwezekanavyo.
Kwa ujumla, suala la kupata mwenza huyo halikuwa
tatizo hivyo, ingawa hapana shaka umakini ulikuwa unahitajika, ingawaje
kutokana na umaarufu niliokuwa nimejijengea tayari pamoja na utundu
kiasi niliokuwa nao, sikuona kama kazi hii ingekuwa ngumu.
Labda ni pale mwanzoni tu nilipodhani kuwa
ingekuwa vyema iwapo ningepata mwenza wa kutoka nyumbani kwetu Bonde.
Hapa napo hapakuwa pagumu sana, ugumu ukatokea tu pale , kila ulipotaja
jina la mmoja wao kwa wazee, uliambiwa huyo ni ndugu yako kwa hivi, huyu
kwa vile na yule kwa lile. Ilimradi ikafikia mahali ambapo niliona kuwa
labda jamaa wote wa Bonde ni ndugu zangu! Nikaamua kuachana na wazo
hilo, sikutaka mambo ya kimila ya kuchinja mbuzi ama kondoo ili kuvunja
undugu.
Kwa bahati, nilikuwa tayari kwa muda mrefu kiasi
nimeshikana na binti mmoja wa mchanganyiko wa Kizaramo na Kinyakyusa.
Nilikuwa nimemfahamu kiasi binti huyo tangu nikiwa bado Shule ya
Sekondari ya Minaki, kule Kisarawe. Wakati huo yeye akisoma Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Wakati huo, pale Minaki tulikuwa na utaratibu wa
angalau mara moja kwa muhula, kuwa na “ball’, yaani tulikuwa tukiwaalika
wanafunzi wa shule mojawapo ya wasichana ya jirani na kuwa “mapatina”
wetu wa dansi. Hasa hasa, tulikuwa tumezoea kuwaalika hawa wasichana wa
Jangwani.
Kwa ajili hii, uhusiano wetu na kina dada wa shule
hii ulikuwa mkubwa sana, hata wakati mmoja mimi na marafiki zangu wa
karibu pale shuleni, akina Sangwa Mwandu, Robert Mandawa, Victor Mnguto,
Twaha Kizuguto, Robert Mwaimu na John Mhina, tulikuwa na kundi letu
lililokuwa likifahamika kama “Bongo Boys”.
Mojawapo ya sifa ya Bongo Boys ilikuwa ni kucheza
dansi na kwenye haya “maball”, tulikuwa tunashusha ngoma kali kweli
kweli! Ghafla, kwenye mojawapo na sherehe hizi, tukaja kukutana na kundi
jingine la wasichana wa hapo Jagwani ambao nao walikuwa wakali kama
sisi, tukawataka urafiki na kuwapachika jina la “Bongo Girls”.
Kutokana na urafiki huu, tukawa mara kwa mara
tunakwenda kuwatembelea dada zetu hawa pale shuleni pao. Tukatokea kuwa
maarufu sana pale Jangwani. Ni wakati huu ndipo nilipomwona Mwangaza.
Yeye hakuwa miongoni mwa Bongo Girls, lakini alikuwa maarufu
sana kwa kucheza mpira wa pete (netball). Ingawaje alikuwa mfupi, bado
alikuwa na uwezo wa kuruka sana na kucheza vizuri mno mchezo huu, hata
akafikia kiwango cha kuchaguliwa kwenye timu ya taifa.
Lakini cha zaidi, Mwangaza alikuwa na umbo la
kupendeza mno, kiasi cha baadhi ya watu kumpa jina la utani la
“Sunshine”. Sikuwahi kuwa karibu naye nilipokuwa Minaki, lakini mara
baada ya kuanza kazi RTD, yeye akiwa bado Jangwani, tulikuja kukutana na
kujenga urafiki mkubwa sana.
Haikuchukua muda, ikawa kwamba kila mtu aliyekuwa
karibu nami alimfahamu Mwangaza na kwa muda wa miaka kadhaa, yeye na
mimi tukawa karibu sana na ndiyo maana, mwishoni mwa mwaka huo wa 1973,
nikawa nimepata hamasa ya kutaka kumuoa.
Mnamo mwanzoni tu mwa mwezi Desemba, nikafanya
sherehe ndogo ya uchumba nyumbani kwao Tandika, nikiwa na baadhi ya
marafiki zangu. Tuliamua tufunge ndoa Februari 1974, mara tu baada ya
mimi kurejea kutoka New Zealand.
Wakati huohuo, mipango yetu ya safari, mimi na
mwenzangu Masoud, ilikuwa ikiendelea vizuri. Tulifanikiwa kupata
pasipoti haraka sana na mambo mengine yote yakawa yamenyooka. Lakini
ghafla, siku moja ikaingia dosari.
Kama kawaida tulikwenda kwa pamoja kwa Sammy Mdee
kupata maelekezo zaidi ya safari yetu hiyo. Sasa safari hii tulipofika,
Sammy akatuambia kuna jambo alilokuwa anataka kutufahamisha.
Pamoja na majukumu mengine, mheshimiwa huyu ambaye
alikuwa pia ni mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ndege la Afrika Mashariki,
East African Airways, alitueleza kuwa kwa muda amekuwa akijitahidi kuona
iwapo katika kupunguza gharama za safari angeweza kupata tiketi moja ya
bure ya ndege kwa ajili ya mmoja wetu, lakini kwa bahati mbaya
haikuwezekana.
Tukiwa mimi na Masoud tumesimama pamoja huku
tukiwa kimya sana, Sammy alituambia kwamba, baada ya kushindikana huko
bado jitihada nyingine ziliendelea kufanyika ili kuona kama bado sote
wawili tungeweza kwenda kwenye safari hiyo, lakini hilo nalo pia likawa
limeshindikana kabisa.
Kwa hiyo, naibu huyo wa mkurugenzi akavuta pumzi
na baada ya kunyamaza kwa muda, akatuambia ya kwamba kutokana na hali
hiyo, wameamua ya kuwa aende mmoja wetu pekee na kutaja jina langu.
Lilikuwa ni pigo kubwa kwetu. Ulikuwa ni mstuko
ambao hatukuutarajia hata kidogo. Ulikuwa ni uamuzi mgumu, lakini
hatukuwa na la kufanya. Tuliondoka ofisini mle kwa Sammy Mdee
kimyakimya.
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO...
source: Mwananchi
source: Mwananchi