Thursday 3 October 2013

Polisi wawajibike kudhibiti wahalifu wa tindikali nchini

3rd October 2013
Gazeti hili tangu wiki iliyopita limekuwa likiandika mfululizo wa  simulizi za watu waliojeruhiwa kwa tindikali hasa visiwani Zanzibar.


Mbali na kuzungumza na waathirika hao ambao wamebaki kuwa na makovu yasiyofutika katika maisha yao yote, pia tumezungumza na viongozi wa vyombo vya ulinzi, viongozi wa dini na hata wafanya biasharaya wa tindikali.

Katika taarifa hizo ambazo tumeziandika kwa mfululizo na kwa kina, kila mwenye moyo wa ubinadamu akizisoma damu itamwenda mbio kwa machungu yaliyowakumba wote waliojeruhiwa. Ni habari za kuhuzunisha sana.

Mlolongo wa watu ambao ama tuliwaona au kuzungumza nao ni pamoja na Sheikh Fadhil Saroga, Katibu wa Mufti wa Zanzibar; Sheha Mohamed Said Kidevu, Ali Mwinyi Msoko, wakiwa ni majeruhi wa kimiminika hicho.

Pia tulizungumza na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa, Mkemia Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Slim Rashid Juma, pamoja na viongozi kadhaa wa dini kisiwani huko, pia tulipata wasaa wa kuzungumza na wanaojihusisha na biashara halali ya tindikali kwa miaka kadhaa tena wakiuzia taasisi za umma kama shule; wote kwa ujumla wao hakuna mwenye jibu juu ya chanzo hasa cha wimbi la watu kudhuriwa kwa tindikali.

Pamoja na hisia zote zilizotolewa, kitu kimoja kilionekana dhahiri, kwamba kuna hofu kwamba wanaofanya uhalifu wa kujeruhi watu kwa tindikali wana nguvu kubwa (kisiasa), wanamtandao mapana na wana uwezo wa kifedha ndiyo maana hawakamatiki kirahisi.

Baadhi ya waathirika wa ukatili huu ambao ni vigumu kueleza na kupata hisia halisi jinsi walivyoumia, wanavyoendelea kutaabika na wengine wakiwa wamepoteza kabisa nguvu na uwezo wa kujitafutia kipato cha kukimu familia zao, wanasema kuwa pamoja na kuumizwa kiasi hicho wanamini kwamba watesi wao wapo wanawaangalia na huenda kuna siku watarejea kuwamalizia.

Hali hii imewajengea hofu tena hofu kubwa mno.

Kinachosumbua zaidi katika kadhia hii ambayo ni ya kikatili kuliko maelezo dhidi  ya ubinadamu, ni polisi kuonekana kutokuwajibika vilivyo. Hakuna mhalifu hata mmoja wa tindikali amekamatwa na kufikishwa mahakamani, hakuna juhudi za makusudi za kuwakamata wahusika ijapokuwa Zanzibar ni eneo dogo tu, kila mmoja akimfahamu mwenzake vilivyo.

Lakini cha kuhuzunisha zaidi, ni operesheni inayoendeshwa na polisi visiwani huko kukamata tindikali kufanyika kana kwamba waliokuwa wanauza bidhaa hiyo kihalali, wakiwa na leseni halali na kwa kweli wakiwa wamefanya kazi hiyo kwa miaka na miaka, kuonekana kama wahalifu. Uhalifu wao ni kuwa na maduka halali ya kuuza tindikali.

Inajulikana wazi kuwa tindikali ni moja ya mali ghafi ya kutengeneza bidhaa kadha wa kadha, miongoni mwake ni sabuni, dawa za kutumika katika vyoo na mabafu, na kila mwenye gari hawezi kusema kuwa hajui tindikali kwa sababu berti nyingi za magari zinatumia maji yanayoitwa ya betri. Maji haya yapo baridi na makali, aina hii ya pili ni tindikali.

Ukisikia operesheni ya polisi iliyofanywa kisiwani Zanzibar hivi karibuni na kuelezwa kuwa wamefanikiwa kukamata tindikali nyingi, ukweli ni kwamba wamekwenda kwenye maduka ya watu wanaoendesha shughuli ya uuzaji wa kemikali hiyo kihalali na kukamata, huku wakijigamba kwamba wamefanikiwa katika operesheni yao. Ukweli ni kwamba hakuna mhalifu anayeonyesha uhalifu wake hadharani.

Juzi akiwa nchini Marekani Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa, Ban Ki Moon, alimhakikishia kwamba serikali husasan Jeshi la Polisi wamejipanga kutokomeza wimbi la watu kushambuliwa kwa tindikali. Hii ni ahadi kubwa, na ni sahihi kabisa kwa kiongozi mkuu wa nchi kuwa na kauli ya namna hiyo.

Pamoja na kuamini katika kauli ya Rais na tukisubiri kuona hatua zikichukuliwa, tunajiwa na hofu kwamba ni kwa nini kama taifa tusubiri kwenda kuonana na Ban Ki Moon ndipo tuzungumze juu ya utayari wetu wa kutokomeza janga hili ambalo kwa sasa limechafua jina letu hata kwenye anga za kimataifa?

Tunajua Rais ana wasaidizi wake, amegawa dhamana kwa watu mbalimbali, suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao ameweka mikononi mwa Jeshi la Polisi, umma unakatwa kodi ili serikali itekeleze majukumu yake, moja ya majukumu hayo ni kuhakikishiwa ulinzi wa maisha na mali zao, sasa kama jukumu hili linatetereka wananchi wanakuwa na maswali yasiyokuwa na majibu, kwamba ni nani hasa mwenye nguvu nyingi kiasi kwamba polisi ama wanamgwaya au wanamlinda katika kukata mzizi wa uhalifu wa kushambulia watu wema kwa tindikali?

Mfululizo wote wa habari tulizoandika kwa wiki mbili sasa unaacha mzigo mzito mabegani mwa polisi, kwamba ni lazima iachwe siasa, iache ulegelege, iache maneno yasiyokuwa na tija, ikomeshe wahalifu wa tindikali ili nchi itulie na watu waishi kwa amani.
 
CHANZO: NIPASHE