Picha na Maktaba
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 9:53 AM
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 9:53 AM
Kwa ufupi
Pia wanadai kwamba wabunge wa CCM waliongeza
baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa
serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa rais kuwa na mamlaka
zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF
vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi
umma kupinga kile walichokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba
Mpya.
Jumapili, Septemba 15, vyama vikuu vitatu vya
upinzani viliandika historia nyingine mpya katika tasnia ya siasa za
Tanzania baada ya kuamua kushikamana kupinga Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Kauli za kupinga muswada huo ulianzia bungeni
mjini Dodoma, lakini sasa umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo
vimetangaza azma ya kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano
kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)
wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo kuwa sheria, hadi
pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Wanasema mapendekezo mengi yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalipendekezwa na
vyama hivyo, hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja na ya
Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha
umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na
mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Vyama hivyo, pia vilitangaza kuanza rasmi mikutano
nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa
ni ‘hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya’.
Mikutano hiyo itaanza Septemba 21 mwaka huu,
kwenye Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao
watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za
dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya
wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu
wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Tamko na madai yao
Tamko hilo la pamoja lilisomwa na Profesa Lipumba
ambapo anasema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya
mikononi mwa umma, anaongeza kuwa suala hilo kwa sasa limehodhiwa na
CCM.
“Tunamshauri Rais Kikwete asisaini muswada huu,
aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na
mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda
kumwona, ila aurejeshe bungeni,” anasema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na
usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka
kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza
taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Anasema muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho
ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na
makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza
baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa
Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka
zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika. Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa
CCM, Septemba 6 mwaka huu, ambao walitumia wingi wao kuupitisha
muswada huo katika mkutano wa 12 wa bunge ambao ulisababisha tafrani
kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje
ya ukumb wa Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani
walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani,
isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Mbowe
Yeye anasema wameamua kuweka pembeni tofauti zao
kwa ajili ya kudai Katiba Mpya ya Watanzania wote, kwamba hata
wanahabari wanatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyombo vyao vya habari
vinavyomilikiwa na vyama vya siasa, kuwa wakweli katika kudai Katiba
Mpya.
“Waandishi wa habari msiwe vipaza sauti vya
watawala bila kutafakari kwa kina Tanzania ya miaka 100 ijayo itakuwaje,
wanahabari mnaweza kutunyima Katiba Mpya au mkatunyima kama ikitumika
vibaya,” anasema.
Anaongeza kuwa amani ya nchi inaweza kuvurugwa
kama mchakato wa katiba utahodhiwa na chama kimoja cha siasa (CCM),
“Ikiwa hivyo, sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue
kuwa kuna misingi ya kuipata amani hiyo, amani inapatikana kunapokuwepo
na haki.”
Huku akinukuu kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere
cha ‘Freedom and Unity’, anasema, “Ni rahisi mno kuliwasha taifa la watu
ambao wamekwazika, taifa hili watu wamekwazika sana. Mchakato wa katiba
unaweza kutibu majeraha makubwa ambayo yanalikabili taifa.”
Anasema fursa adimu ya kupata Katiba Mpya
inapotezwa na bunge na CCM na anasisitiza kwamba wapinzani watatumia
kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea ili washiriki
katika kuidai katiba iliyotokana na mawazo yao.
“Wapinzani hatutarudi nyuma na hatutakubali nchi
kurejeshwa chini ya uongozi wa katiba ya sasa. Hilo wenzangu (wenyeviti
wenzangu) naomba mnielewe, Chadema hatukubali na naomba na nyinyi
msikubali, maana ndani ya CCM kuna kundi linataka kurudi katika katiba
hii tunayoilalamikia,” alisema.
Anasema katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere
alisema, ‘Kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa
makini’, kwamba hoja ya kutaka Amani itaharibiwa na wale wenye dola,
siyo vyama vya upinzani.
Mbatia
Kwa upande wake, Mbatia anasema historia ya nchi
inaonyesha kuwa waasisi wa kutaka sauti, kauli na mawazo ya umma
isikike katika kudai Katiba Mpya ni vyama vya upinzani. Anasema mwaka
1991 vikundi na wadau mbalimbali walikaa na kuanzisha mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba, kwamba ripoti ya tume ya Jaji Francis Nyalali
iliyoundwa mwaka 1991 na ripoti ya tume ya Jaji Kisanga ya 1998 (white
paper) zote zilikuja na mapendekezo ya kutaka Katiba Mpya, kupendekeza
muundo wa serikali tatu na kwamba tume hizo hazikuundwa kwa matakwa ya
Serikali.
“CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania
kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini
Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa,
lakini Tanzania itaendelea kubakia” anasema na kuongeza;
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu
wanakosea, hatuwezi kuangamiza wazo letu la kutaka Katiba Mpya, katika
taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo
yao.”
Anasema Katiba ni tamko la umma linalotokana na
umma unataka ujiongoze namna gani, “Katiba Mpya ni tendo la maridhiano
na kisiasa siyo tendo la kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka
pembeni, tupo juu ya itikadi za vyama vya siasa.” Anasema maridhiano ya
kisiasa ndio yalizaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1994 na
pia yamezaa serikali ya kitaifa Zanzibar mwaka 2009 baada ya Katibu Mkuu
wa CUF na Makamu wa rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad na aliyekuwa
rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume kuweka tofauti zao pembeni.
Anasema mawazo ya kutaka Katiba Mpya
wanayoyasimamia sasa yapo katika rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, hivyo ni lazima wayasimamie.
“Chama cha KANU hakipo Kenya lakini Kenya ipo, UPC
ya Uganda haipo lakini Uganda. CCM inaweza kuondoka na kufutika kabisa
katika historia ya nchi yetu lakini Tanzania itaendelea kuwepo” anasema.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI