Saturday 5 October 2013

Ghasia Mombasa zaacha wafu 4, wengine 7 taabani


Askari wa Kikosi cha Zimamoto wakipambana kulizima jengo la kanisa la Jeshi la Ukombozi lililotiwa kiberiti na waandamanaji mjini Mombasa leo mchana. PICHA | AFP 
Na AFP

Posted  Ijumaa,Oktoba4  2013  saa 17:56 PM
Kwa ufupi

- Hali ilianza kuonekana tete toka leo asubuhi, ambapo wanausalama wa Kenya walionekana wakijaribu kuboresha ulinzi katika mitaa mbali mbali ya mji wa Mombasa kufuatia mauaji ya Omar.


Mombasa. Watu 4 wameuawa na wengine 7 kujeruhiwa mjini Mombasa katika ghasia zilizoanza baada ya swala leo mchana kufuatia mauaji ya Shehe Ibrahim ‘Rogo’ Omar na wenzake watatu jana.
Shehe ‘Rogo’ Omar  na wenza walifariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kumiminiwa risasi likiwa njiani kwenye barabara ya Malindi-Mombasa, katika shambulizi linaloolekana lilikuwa limepangwa  ili kuwatoa roho.
Mkuu wa polisi katika eneo la Kisauni, Jolius Wanjohi alithibitisha mauaji hayo ya Shehe Omar, lakini akashindwa kutoa maelezo zaidi, hali iliyochochea hisia za wafuasi wa mhubiri huyo na kusababisha waingie mtaani mapema mchana wa leo.
Hali ilianza kuonekana tete toka leo asubuhi, ambapo wanausalama wa Kenya walionekana wakijaribu kuboresha ulinzi katika mitaa mbali mbali ya mji wa Mombasa kufuatia mauaji ya Omar.
Hata hivyo kufikia mchana, waandamanaji waliokuwa wakijikusanya katika vikundi vidogo vidogo waliingia barabarani kwa ghadhabu, wakirushia magari mawe na kuwasha moto huku wakipambana na polisi.
Angalau mmoja kati ya waliokufa katika vurugu hizo alipigwa risasi, kwa mujibu wa Red Cross Kenya, huku magari na kanisa la Jeshi la Ukombozi (Salvation Army) katika wilaya ya Majengo vikitiwa kiberiti.
Shirika la habari AFP linaripoti marehemu wengine yaonekana walikufa baada ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali katika vurumai hiyo, likimnukuu msemaji wa Kituo cha Kukabiliana na Matukio ya Hatari nchini Kenya.
Polisi wanadai walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika viunga vya Majengo – eneo ambalo wanaishi Wakenya wa kada ya kati, wengi wao wakiwa waumini wa dini ya Kiislamu.
Huku Maimamu na viongozi wa kijamii wakiomba utulivu, baadhi ya mashuhuda wameiambia AFP kuwa polisi walionekana wakipiga risasi za moto hewani wakati wakijaribu kudhibiti vurugu hizo.
Kamanda wa polisi mjini Mombasa, Kipkemoi Rop, amethibitisha wamewakamata watu 24 kufuatia ghasia za leo mchana, akisisitiza jeshi lake halitavumilia “vikundi vya vijana wahuni  kuukamata mji [wetu].”
Marehemu Omar alikuwa mhubiri katika msikiti wa Musa, na alikuwa mwandani wa mhubiri mwingine machachari wa Kenya, Shehe Aboud Rogo Mohammed ambaye pia aliuawa katika tukio lisiloeleweka Agosti, 2012.
Tukio hili la jana lilikuja katika kipindi kigumu kwa wakazi wa Kenya, wengi wao wakiwa wamejawa hofu kufuatia shambulizi la jumba la biashara la Westgate wiki mbili tu zilizopita – tukio hatari lililoacha vifo zaidi ya 67 na kusababisha hatihati jijini Nairobi.


Shehe Omar anashutumiwa kuwa na uswahiba wa karibu sana na wanamgambo wa Kisomali wa Al-Shabab ambao wamekiri kuhusika katika uvamizi wa Westgate.
Baadhi ya Waislamu mjini Mombasa wamevilaani vyombo vya dola, wakivituhumu kwa kuchukua ‘hatua za makusudi’ kumwinda Shehe Omar na wenzake kama sehemu ya vita yao dhidi ya ugaidi – kauli ambayo serikali ya Kenya imeikataa katakata.

SOURCE: MWANACHI