Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba15 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Oktoba15 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwili wa Mushi ambaye alijiua kwa kujipiga risasi,
unatarajiwa kusafirishwa na kuzikwa Kijiji cha Ongoma kilichopo katika
Kata ya Uru, mkoani Kilimanjaro.
Dar es Salaam. Hali ya mwandishi wa habari wa
Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro aliyejeruhiwa vibaya baada ya
kupigwa risasi mbili juzi huko Kibamba, Dar es Salaam inazidi kuimarika
na jana alizungumza na gazeti hili na kusema; “Sijambo, naendelea
vizuri.”
Ufoo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, hata hivyo, anazungumza kwa shida kutokana na kukabiliwa na
maumivu baada ya kufanyiwa upasuaji juzi.
Mwandishi huyo amehamishiwa katika wodi ya
upasuaji wa moyo huku kiongozi wa wodi hiyo, ambaye alikataa jina lake
kuandikwa gazetini, akieleza kuwa walimhamishia huko ili apate muda
zaidi wa kupumzika.
“Watu wanakuja kwa wingi kumjulia hali, tuliona tumhamishe ili apumzike,” alisema kiongozi huyo.
Kabla ya kupelekwa katika wodi hiyo, Ufoo alikuwa
katika wodi ya Kibasila na baadaye alihamishiwa katika Chumba cha
Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Ufoo alipigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery
Mushi ambaye alijiua baadaye. Pia Mushi anatuhumiwa kumuua mama yake
Ufoo, Anastazia Saro wakati wa tukio hilo.
Mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa huko Machame mkoani Kilimanjaro.
Ufoo aongea kwa shida
Mara baada ya mwandishi wa gazeti hili jana kuingia
katika chumba alicholazwa Ufoo huku akisindikizwa
na wauguzi watatu, mwandishi huyo alitoa mkono wake na kusema; “Njoo
hapa unisalimie huku umenishika mkono.”
Huku akionyesha uchovu na kusikia maumivu, alizungumza kwa tabu na kusema; “Sijambo naendelea vizuri.”
Mara baada ya wauguzi hao kumweleza kuwa kati ya
waandishi zaidi ya 30 waliofika kumjulia hali ni watatu tu ndiyo
walioruhusiwa kumwona alitaka kujua ni kina nani waliobaki nje kwa
kuhoji; “Nani hao wako nje.”
SOURCE: MWANANCHI
Hata hivyo, wauguzi hao hawakutoa nafasi yoyote kwa Ufoo kuulizwa maswali.
Ufoo alipigwa risasi moja tumboni, iliyotokea
kwenye mbavu na nyingine ilipita kifuani hadi kwenye ziwa lake la kulia
hadi kwenye mkono wa kulia.
Baada ya tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.
Awali Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alifika katika hospitali hiyo kwa
lengo la kuzungumza na mwandishi huyo, lakini alizuiwa na kutakiwa
kwenda ofisi za utawala ili kupewa kibali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na
Redio One, Joyce Mhaville alisema kuwa Ufoo anahitaji muda wa kupumzika
ili apone.
“Ufoo ana kumbukumbu ya kila kitu kilichotokea
ingawa kutokana na upasuaji aliofanyiwa anahitaji kupumzika saa 72,”
alieleza Mhaville.
Mushi kuzikwa Uru
Mwili wa Mushi ambaye alijiua kwa kujipiga risasi,
unatarajiwa kusafirishwa na kuzikwa Kijiji cha Ongoma kilichopo katika
Kata ya Uru, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa kikao cha ndugu wa marehemu
kilichofanyika kwenye Ukumbi wa 92 jijini Dar es Salaam jana, kaka wa
marehemu, Silver Mushi alisema bado hawajaamua siku ya kusafirisha.
Alisema maandalizi ya mazishi yanaendelea na ndugu
na jamaa zake wameshtushwa na taarifa za tukio hilo la mauaji kwani
hawakuwa na taarifa zozote za mzozo baina yao na Julai mwaka huu
marehemu na mzazi mwenzake huyo walisafiri pamoja hadi Uru mkoani
Kilimanjaro.
Silver alisema kuwa wawili hao walikuwa wanapendana na kilichotokea kimewashangaza.
“Siwezi kusema kuwa walikuwa wachumba kwani katika
mazingira yetu ya Kiafrika kuwa na mwanamke kwa miaka 10 hadi kuzaa
mtoto mwenye umri mkubwa kama huo ni wazi kuwa nyie mna zaidi ya
uchumba,” alisema.
Mushi alisema pia kuwa marehemu alikuwa anakaribia kuhitimu
Shahada ya Kwanza ya Masuala ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu Huria
nchini India.
Mushi awashtua wafanyakazi wenzake Darfur Watu
waliokuwa wakifanya kazi na Mushi kwenye Operesheni ya Kulinda Amani ya
Umoja wa Kimataifa
(Unamid) huko Darfur, Sudan wameeleza kustushwa na vitendo vya mfanyakazi mwenzao, Mushi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu
jana, watu hao ambao waliwahi kuishi na Mushi wakiwa kwenye shughuli zao
huko Darfur, walisema marehemu alikuwa na tabia ya upole, mcheshi na
mchapa kazi.
Mfanyakazi mwenzake, ambaye ni raia wa Tanzania,
ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa sio msemaji rasmi wa Unamid,
alisema hakuwahi kusikia Mushi akinung’unika kuhusu masuala ya maisha
yake.
Alisema pia mara nyingi, Mushi alikuwa
akiwasiliana na mzazi mwenzake Ufoo nyakati za jioni. Walikuwa
wakiwasiliana zaidi kwa njia ya mtandao wa intaneti.
“Kwa jinsi nilivyowaona kwa kweli walikuwa
wanapendana sana. Kila mtu haamini kama kweli Mushi amefanya kitendo
hiki cha kumpiga risasi Ufoo na kumuua mama mkwe wake,” alisema
Mtanzania huyo kwa masikitiko makubwa.
Pia Mushi alikuwa anasifiwa kutokana na uwezo wake
wa kufanya vitu vingi kiasi cha kupewa jina la utani la ‘multi
talented’ (Mtu mwenye vitu vingi).
“Mushi akiwa hapa Unamid alikuwa kama mtaalamu wa
mawasiliano lakini kumbuka huko nyuma aliwahi kuwa mpigapicha wa vituo
vya televisheni vya ITV na TBC,” aliongeza raia huyo wa Tanzania, ambaye
waliishi nyumba
moja katika Mji wa El-Jeneina huko Darfur ambako ni Magharibi mwa nchi ya Chad.
Mushi pia alikuwa ana sifa ya kupenda kula vyakula aina ya mboga na alikuwa analima bustani.
Mfanyakazi mwingine wa Unamid, ambaye ni raia wa
Nigeria mwenye cheo cha Kanali, alisema Mushi alikuwa akilima mchicha,
kabichi, bamia na mboga za majani ya maboga kwenye eneo la nyumba yake
huko Darfur.
“Nani jamani ataangalia bustani ya Mushi?
“Siamini kama amefanya kitendo hiki,” alilalamika mtu huyo.
Polisi
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova amesema wanatarajia kutoa ripoti leo ya kupigwa
risasi kwa Ufoo na kuuliwa kwa mama yake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Kova alisema ripoti hiyo itatolewa na kamati waliounda kuchunguza suala hilo.
“Umma utaweza kuisoma, kuichambua na kutoa maoni
kuhusu hatua za kuchukua ili matukio ya aina hiyo yasitokee tena,”
alisema Kova.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Elizabeth Edward, Aidan Mhando na Joseph ZabloSOURCE: MWANANCHI