Saturday, 7 September 2013

Viongozi wa G20 washindwa kuafikiana kuhusu Syria


Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Septemba7  2013  saa 12:0 PM
Kwa ufupi
Marekani yahaha kutafuta kuungwa mkono kuhusu uamuzi wake wa kuivamia kijeshi. Urusi yashikilia msimamo wa kuzuia uvamizi wa kijeshi.


St Petersburg. Viongozi wa nchi zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani wameshindwa kuafikiana kuhusu mzozo wa Syria katika mkutano unaofanyika nchini Urusi, huku Marekani ikitafuta uungwaji mkono kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria.
Katika mkutano huo wa mataifa hayo makubwa kiviwanda (G20) uliofanyika huko Petersburg, Urusi, suala la namna ya kuchukua hatua katika mgogoro unaoendelea nchini Syria ndilo lililotawala agenda za mkutano huo, ambao ni maalumu kwa ajili ya masuala ya uchumi na biashara.
Kumekuwa na mikutano ya dharura miongoni mwa pande mbili zinazotofautiana kuhusu namna ya kuchukua hatua kwenye mgogoro huo, ambapo Rais Barack Obama wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi wamekuwa wakijaribu kutafuta ushawishi kwa ajili ya kuungwa mkono.
Hadi jana mchana, viongozi waliopata fursa ya kulizungumzia suala hilo la Syria walisema hakukuwa na maafikiano kuhusu hatua za kuchukuliwa, ambapo Waziri Mkuu wa Italia, Enricco Letta, alithibitisha kupitia mtandao wa Twitter kuwa hakukuwa na maafikiano kuhusu mzozo wa Syria.
Urusi imekuwa ikisimama kidete kuhusu kutochukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad kuhusiana na madai kuwa ulitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake Agosti 21.
Hadi jana mchana, Rais Barack Obama alikuwa akiendelea na jukumu lake la kutaka kuungwa mkono kuhusu kuichukulia Syria hatua za kijeshi, ambapo aliweza pia kukutana na Rais wa China pembezoni mwa mkutano huo na baadaye kukutana na mshirika wake, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande.
Mjumbe wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, Samantha Power, ameishutumu Urusi kwa kulishika mateka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kutumia kura yake ya turufu. Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, naye alisema nchi yake ina ushahidi mpya kuhusu shambulio hilo la kemikali.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-Moon, aliwaambia viongozi hao wa G20 kuwa kutoa silaha kwa upande wowote katika mzozo wa Syria sio suluhisho kwani hatua za kijeshi haziwezi kuwa suluhisho la mzozo huo.
Washirika wa Syria bado hawaonekani kushawishika na kampeni za Obama za kuchukuliwa hatua za kijeshi.
Papa Francis ataka suluhisho
Wakati mkutano huo ukiendelea, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, pia ameelezea hisia zake kuhusu mzozo huo na kutoa wito kutafutwe suluhisho la amani na wala si kwa kutumia nguvu za kijeshi akionya hatua za kijeshi zitaambulia patupu katika kuumaliza mzozo wa Syria.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, pia alisema mara kadhaa kuwa nchi yake haitashiriki katika shambulio la kijeshi litalaoongozwa na Marekani dhidi ya Syria na tayari Bunge la Uingereza lilipiga kura kupinga nchi hiyo pia kuhusika katika hatua hiyo.

Mkutano huo wa G20 uliofanyika kwa siku mbili ulimalizika jana ambapo Rais Putin aliyekuwa mwenyeji alipanga muda maalumu kujadili mzozo huo katika chakula cha usiku wa juzi, licha ya kuwa Syria haikuwa katika ajenda.
Utawala wa Syria umekuwa ukishutumiwa kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wakati wa mzozo huo uliodumu miezi 30 sasa.

source: Mwananchi