Thursday, 2 January 2014

Lowassa atangaza nia kimtindo

Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa akiwasalimia wananchi waliohudhuria sherehe za Mwaka Mpya nyumbani kwake jana. Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godluck ole Medeye na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole. Picha na Mussa Juma. 


Posted  Alhamisi,Januari2  2014  saa 8:46 AM
Kwa ufupi
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza katika ibada hiyo.


Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza katika ibada hiyo.
Lowassa alisema anaamini watu hao waliofika, wana uhakika wa ushindi katika safari hiyo kwa kumtegemea Mungu.
“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu,’’ alisema Lowassa na kupokelewa na sauti za shangwe kanisani.
Licha ya kutoweka bayana, Lowassa amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa wanasiasa wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwakani.
Azungumzia Katiba Mpya.
Akizungumzia Katiba Mpya, ambayo mchakato wake sasa unaelekea katika Bunge Maalumu, licha ya kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba alisema ana wasiwasi juu ya muundo wa Serikali Tatu.
“Nina wasiwasi na huu muundo, ni vyema viongozi wa dini, kuliombea taifa tupate Katiba bora kwani maoni ya watu asilimia 40 ambao hawakutaka muundo wa Serikali Tatu lazima yatazamwe,” alisema Lowassa.
Ibada katika Kanisa hilo, ambayo iliendana na harambee ya kuchangia hosteli na zaidi ya Sh89 milioni kupatikana, iliongozwa na Kaimu Askofu wa KKKT, Usharika wa Kaskazini Kati, Solomon Masango.
Katika mahubiri yake, Kaimu Askofu Masango alimtakia kila la heri Lowassa katika safari yake hiyo akisema anamtambua kuwa ni kiongozi bora.
Hafla ya nyumbani
Akizungumza katika hafla aliyoandaa baadaye nyumbani kwake, Lowassa alirudia kauli yake ya kuanza safari.

SOMa zaidi: Lowassa