Tuesday, 22 April 2014

UVCCM: Green Guard iwashughulikie Ukawa ikiwa...


 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumanne,Aprili22  2014  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Alisema viongozi wa Ukawa wamekuwa wakiwatukana waasisi wa Muungano; Mwalimu Julius Nyerere na Shekh Abeid Karume hata nje ya Bunge ambako hawana kinga.

Dodoma/Dar. Katibu wa Uhamashaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda amekiagiza kikundi cha Ulinzi cha CCM (Green Guard) ‘kuwashughulikia’ wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watakaowatukana waasisi wa Taifa.
Makonda alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM mkoani Dodoma, kuwa hatua hiyo ichukuliwe ikiwa vyombo vya dola vitaacha kuchukua hatua dhidi ya wajumbe hao.
CCM kimejitenga na kauli hiyo kikisema ni ya Umoja wa Vijana, taasisi ambayo inajitegemea ndani ya chama.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alisema jana kuwa hakuwa na taarifa zozote juu ya mipango hiyo ya vijana wa CCM.
Kauli ya Makonda
Katika mkutano huo, Makonda alisema, “Ukija kwenye chama sisi hatuna polisi, hatuna jeshi, tuna Green Guard, kazi yake ni kulinda viongozi. Huku tunakokwenda kama itafika watu hawa wanaendelea kuwatukana viongozi, unaenda kuripoti polisi hawachukui hatua, maana yake nini? Si utawala wa sheria haupo?” alihoji.
Alisema viongozi wa Ukawa wamekuwa wakiwatukana waasisi wa Muungano; Mwalimu Julius Nyerere na Shekh Abeid Karume hata nje ya Bunge ambako hawana kinga.
“Hatutakubali tena na ninawaomba vijana wote wa Green Guard popote pale watakaposhuhudia kiongozi wa nchi, Hayati Mwalimu Nyerere, Mzee Abeid Aman Karume na wakashuhudia kwamba sheria haichukui mkondo wake, tutachukua hatua sisi wenyewe, unyonge sasa basi,” alisema.
Makonda ambaye pia ni mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema (Ukawa) watakapotoka nje ya Viwanja vya Bunge na kuendelea kuwatukana waasisi hao, vijana wa Green Guard watashughulika nao kwa mujibu wa sheria za nchi.
Nape awaruka
Alipoulizwa kama kauli ni ya chama hicho tawala, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema UVCCM ni taasisi inayojitegemea na Makonda ni msemaji wake hivyo kama amesema ni halali kwa taasisi yao.
“Umoja wa vijana uko huru kutoa matamko yao,” alisema.

Akizungumzia agizo hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema inathibitisha kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwa wasiwe wanyonge tena na kusema: “Sasa tumeanza kuona viashiria vyake.”
Dk Slaa alisema suala la Katiba siyo vita, kama nao wana hoja za kuwaelimisha wananchi basi waende kufanya hivyo, si kufikiria kuua wananchi kwa sababu ya hofu ya endapo wananchi watajua ukweli.
“Mungu anawatia upofu hawa wenzetu. Chama kikongwe kama hiki hakitazamiwi kuwa chanzo cha fujo na mauaji,” alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa wakianzisha fujo vyama vingine pia vitachukua hatua, matokeo yake ni umwagaji damu.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Salim Bimani alisema bado wana imani na Jeshi la Polisi kwani ndilo liliopewa jukumu la kulinda amani na usalama wa nchi, hivyo hatarajii kuona vijana wa Green Guard wanapewa nafasi ya kufanya uhalifu wao.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Beatrice Moses (Dodoma), Peter Elias, Nuzulack Dausen (Dar).

SOURCE: MWANANCHI NEWS PAPER