Friday 2 March 2007

Salamu na Hoja za Wana - TASAO kwa Mh. Rais J.M. Kikwete, 28.02.2007

Mheshimiwa Rais,

Hapa Norway na hususani Oslo, kuna wanafunzi watanzania wanaosoma katika vyuo mbalimbali. Wanafunzi hawa wanaunganishwa kwa pamoja katika Umoja wao unaojulikana kama TASAO – Tanzanian Students Association – Oslo. Umoja huu umeanzishwa january, 6 mwaka huu, kwa malengo ya kuwaunganisha, kusaidiana kwa hali na mali pia kuhamasishana katika kutimiza na kufikia malengo ya kishule yaliyotuleta huku kama wanafunzi.

Baada ya hayo mheshimiwa Rais, wanafunzi walikuwa na haya ya kusema kuhusu yanayojiri kwa ndugu zetu, wadogo zetu, kaka na dada zetu huko nyumbani Tanzania:


1. Suala la kuchangia elimu ya juu:
Kwa pamoja tunaungana na serikali katika suala hili. Tunaomba serikali iwe makini haswa katika suala la nani anastahili kupata mkopo.. Hata hivyo tuna mapendekezo yafuatayo;
i. Twaiomba serikali itoe mkopo kwa 100% kwa kila mwanafunzi aliyefaulu na ana sifa za kujiunga na chuo.
ii. Wazazi na wanafunzi waelimishwe juu ya suala hili ili kuepusha migongano
iii. Iwekwe mikakati thabiti ya kufuatilia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa ili iweze kuwasaidia na wengine
iv. Kuna haja ya kupitia mara kwa mara viwango vya posho na mikopo ili kukidhi tatizo la viwango vidogo vya bei za soko.

2. Kuhusu mazingira ya kusomea:
Pamoja na nia nzuri ya serikali katika kuongeza idadi ya vyuo na wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu, serikali pia izingatie;
i. Uwiano wa miundombinu na idadi ya wanafunzi
ii. Ihamasishe wawekezaji kuwekeza kwa kujenga hosteli kwa ajili ya malazi ya wanafunzi ndani ya maeneno ya vyuo.
iii. Ukubwa wa darasa (number of student) iendane na idadi ya walimu kwa baadhi ya vitivo
iv. Uboreshaji wa usafiri kwa wanafunzi wanaoshi nje ya vyuo (kampasi)
v. Uwezo wa vyuo kumudu mahitaji ya ufundishaji yanayohusiana na programu zilizoongezwa

3. Elimu kazini
Sambamba na nia nzuri ya serikali kuendeleza viwango vya elimu kwa watumishi wake, yapo matatizo ambayo yanarudisha nyuma nia nzuri ya serikali yetu. Kama yafuatayo:
i. Baadhi ya watumishi kuzuiwa kwenda masomoni hata pale wanapokuwa na ufadhili binafsi
ii. Kutotambulika kazini pindi wamalizapo masomo yao na kutakiwa kuomba kazi hizo upya
iii. Kutokuinuliwa kwa vyeo ama kupandishwa kwa madaraja ya utumishi ya watumishi kulingana na viwango vyao vya elimu walivyojiendeleza


4. Utafiti
Ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia tunapendekeza serikali kuzingatia yafuatayo;
i. Iwekeze kwenye tafiti za msingi kwa maendeleo ya nchi
ii. Ithamini na kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali zilizokwisha fanyika kwa ajili ya nchi yetu

Mwisho twasema ahsante kwa kututembelea na twakuomba kama wanafunzi tufikishie salamu zetu kwa mfalme na serikali ya Norway kwa ufadhili wao kwetu katika masomo. Twawaomba wasichoke kutusaidia. Pia tusalimie wa-Tanzania wenzetu walioko huko nyumbani pindi utakapo rejea. Karibu tena - Norway.

Ni sisi wanafunzi wa Tanzania hapa Oslo - Norway

Imesomwa na Rais wa TASAO,

JOHN, Chalukulu