Monday 8 July 2013

JK ataja sifa za viongozi waliofilisika kifikra

 
Rais Jakaya Kikwete akiweka saini juu ya mpira uliotumika katika pambano la kirafiki Wabunge mashabiki wa Yanga na Simba lililofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa katika Tamasha la Matumaini. Anayeangalia ni mwamuzi wa pambano hilo, Othman Kazi. Yanga ilishinda kwa penalti 4-3. Picha Michael Matemanga  


Na Matern Kayera, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai8  2013  saa 7:59 AM
Kwa ufupi
  • Kiongozi yeyote wa dini anayesisitiza waumini wake kuunga mkono chama chochote cha siasa amefilisika kifikra
Rais Jakaya Kikwete jana alipuliza kipenga kuzindua Tamasha la Matumaini Dar es Salaam na kuwanyooshea kidole viongozi wa dini wanaohubiri siasa katika maeneo ya ibada akisema kufanya hivyo ni kufilisika kifikra.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kupiga filimbi kuashiria ufunguzi wa tamasha hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema ni jambo la hatari kwa Watanzania kukubali kugawanywa kwa misingi ya udini, rangi au maeneo wanakotoka.
Alitaka dini zitumike kuwaunganisha wananchi na siyo kuwagawanya akisema Watanzania wanakwenda makanisani na misikitini kusali na siyo kufanya siasa. Alisema kiongozi yeyote wa dini anayesisitiza waumini wake kuunga mkono chama chochote cha siasa amefilisika kifikra.
 “Ni hatari tukigawanyika, ni lazima tuwaambie watu wanaotaka kutugawanya kwa misingi ya dini, rangi au maeneo tunakotoka kwamba hatutaki na wala hatukubali. Nchi hii wakoloni waliishindwa hivyo lazima tuendeleze utamaduni wa kukataa kugawanywa kwa msingi wowote ule,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wanasiasa kuepuka kauli zenye kuchochea vurugu miongoni mwa wananchi wanapokuwa kwenye harakati zao za kisiasa akisema madaraka ya kisiasa yatafutwe kwa njia ya amani na siyo kuingiza kauli za uchochezi zenye kuwagawa wananchi.
“Nawaasa wanasiasa wasipandikize chuki za kidini au maeneo wanakotoka wananchi, kama ni madaraka yatafutwe kwa njia ya amani kwenye sanduku la kura,” alisema Rais. Alisema Tamasha la Matumaini liwe mfano wa kuigwa wa kutumia michezo kuwaunganisha watu badala ya kuwagawanya.
Alisema timu zilizotumbuiza jana zilimebeba majina ya Simba na Yanga, zimejumuisha wabunge kutoka vyama vyote ikionyesha kuwa wote ni wamoja licha ya tofauti za kisiasa.
Alipongeza mkakati wa waandaaji wa tamasha hilo ambao wametangaza kwamba mapato yatakayopatikana yatatumika kusaidia shule za sekondari katika mikoa minane nchini.

Chanzo: Mwananchi.co.tz