Kwa ufupi
Ni wale wanaodaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Musa Tesha huko Igunga Tabora.
Dar es Salaam. Hatima ya makada
watano wa Chadema, wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Tabora, inatarajiwa kujulikana leo, wakati mahakama hiyo
itakapotoa uamuzi kuhusiana na kesi hiyopamoja na mambo mengine, uhalali
wa mashtaka yanayowakabili.
Makada hao wa Chadema, Henry
John Kilewo, ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Evodius
Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Daniel, Seif Magesa Kabuta,
walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mawili,
moja la ugaidi na lingine la jinai.
Katika shtaka la kwanza wanashtakiwa chini ya
Sheria ya Kuzuia Ugaidi, wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha
huko Igunga, Tabora, na la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni
za Adhabu wakidaiwa kumdhuru Tesha kwa kumwagia tindikali.
Walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati
wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.Baada ya kusomewa
mashtaka hayo, mawakili wao, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari
walipambana kuwanusuru na mashtaka hayo.
Mawakili hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo,wakidai kuwa hakuna
vigezo vya kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji
utaratibu wa kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule
walikokamatiwa.
Hivyo waliiomba Mahakama hiyo ama iwafutie
mashtaka hayo au iamuru kila mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika
mahakama za mahali walikokamatiwa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa
Serikali, Juma Masanja akisaidiana na Wakili wa Serikali, Idelfonce
Mukandara, walidai mashtaka hayo ni halali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu
Mkazi wa mahakama hiyo, Joctan Rushwera aliahirisha kesi hiyo na kupanga
kutoa uamuzi leo.
Hakimu Rushwera aliamuru washtakiwa wote wapelekwe
mahabusu wakisubiri uamuzi wa kesi yao leo, kwa kuwa mashtaka
yanayowakabili hayana dhamana.