Kwa ufupi
Kumbe aliwahi kuwa kijakazi migodini Arusha,alisota Kijiweni Sinza.
Salim
ni Mtanzania anayetangaza vipindi mbalimbali katika Shirika la Habari
la Uingereza (BBC). Safari ya kufikia mafanikio hayo ilikuwa na milima
na mabonde, tabu na karaha.
Penye nia pana njia na mtafutaji makini huwa
hachoki, ndivyo anavyosema mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dk Wayne Dyer
wa Marekani katika kitabu chake cha ufanye nini kupata unachokiazimia.
Licha ya kauli hii ya Dk Dyneer, kuna vijana wengi
nchini wanaonekana wamekata tamaa; Wengine hufikiri kwamba kama
umezaliwa katika familia duni, maana yake utakuwa na maisha duni milele,
huku wale ambao wamezaliwa katika familia tajiri, wanafikiri
wataendelea kuwa tajiri.
Hata hivyo ukweli ni kwamba mtu yeyote anaweza
kuwa na maisha bora, kama anavyosema msomi Hope Clark katika kitabu
chake Fedha za Waandishi cha hivi karibuni nchini Ireland, kwamba siri
ya kufanikiwa katika maisha ni kuishi kwa malengo, kuishi vizuri na watu
na kupenda kuwa karibu na wasiokata tamaa.
Mwalimu Julius Nyerere wakati fulani amewahi
kunukuliwa akisema ‘Uchumi mnao, mmeukalia’. Kila mtu alitafsiri
alivyoweza, lakini ukweli hasa ni kwamba mtu yeyote akijipanga vizuri
kwa maana ya kutuliza akili yake, kukaa na watu wa kumshauri vizuri na
kufanyia kazi mambo au mipango anayoipanga, anaweza kufanikiwa
anachotaka...Ni ukweli kuwa kuna wengi wana maisha duni kwa sababu
pamoja na mambo mengine ya tabia zao za kukata tamaa, waoga wa
kuthubutu.
Wengi wanasubiri wengine, wanalalamikia wengine zaidi
Mwalimu alisisitiza, nitamnukuu; “Hatuwezi
kusubiri hadi watoto wetu walio shuleni wamalize elimu yao ndipo tupate
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”
Kwa hali yoyote ambayo mtu inamsumbua katika
maisha yake ni vizuri kuangalia namna ya kujitegemea, badala ya
kulalamikia wengine, anasema mshauri maarufu Marekani, David Kudler
katika chapisho lake alilolipa jina Namna ya Kufanikiwa katika maisha.
Huu ndiyo ukweli wenyewe
Vijana wengi hapa nchini wamekuwa wakitamani sana
kufikia mafanikio lakini wengi wanalalamikia kuwa wanakabiliwa na
changamoto ya kukosekana kwa mbinu sahihi za kuwafikisha kwenye kilele
cha mafanikio wanayotaka. Wachambuzi wa masuala ya uchumi akiwemo
Profesa Muhammad Yunus ambaye anasifika kwa kuinua maendeleo kwa watu wa
hali ya chini Bangladesh, wanasema ili kufikia mafanikio ni lazima
uchukue hatua kwa nafasi uliyonayo, bila kujali ikoje, hii itakusaidia
kupata chachu ya kuongeza kasi ya kutekeleza hatua moja baada ya
nyingine katika safari yako.
Kuna wengi wamekuwa wakiwaza makubwa, lakini
wanaishia kuona tu wengine wakipaa. Hata hivyo ni wazi kwamba ushindi
huja baada ya kufanya harakati za kuutaka huo ushindi, siyo kukaa tu na
kulalamika kama wafanyavyo baadhi ya watu.
Kati ya vijana ambao wanaonekana kupambana hadi
kuweza kujenga majina na heshima zao Duniani ni Salim Kikeke; Ni mtu
ambaye kama angekata tamaa hakika asingefika aliko sasa.
Sasa amekuwa ni mtu wa kujadiliwa na umaarufu wake
hauko tu Tanzania, bali maeneo mengi ya Dunia hasa kunakozungumzwa
Kiswahili. Huyu mtu ni kati ya watangazaji wakongwe na kivutio cha watu
wengi kutoka barani Afrika na duniani kote, lakini katokea wapi?
Salim ni Mtanzania anayetangaza vipindi mbalimbali katika
Shirika la Habari la Uingereza (BBC). Safari ya kufikia mafanikio hayo
ilikuwa na milima na mabonde, tabu na karaha.
Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika
Chuo cha Kilimo Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya
kukosa ajira kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya
Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa
kilimo,” anasema Kikeke.
Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira
zilikuwa ngumu.Kwa karibu mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo
ya Tanzanite ya Mererani Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha
kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi.
Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua
kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani
kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini.
Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es
Salaam.
Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa
akishinda kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake,
Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Mboya ndiye mmoja kati ya rafiki zangu ambao
tulibadilishana mawazo, tulifarijiana na kufikiria matarajio ya ndoto
zetu, mambo yalikuwa magumu mpaka nikafikia hatua ya kusema basi
imetosha,” anasema Kikeke.
Kuingia utangazaji
Mara baada ya kuona matumaini yakififia kupitia
taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa maisha
baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni Magic FM.
Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi huo,
haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa ameupata
kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Mama yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa
kuingia katika utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za
redioni na alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea
duniani, nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,”
anasema Kikeke.
Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika
katika ofisi za kituo cha kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa wanaita
Magic FM, walikuwa wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba
kufanya kazi bure, nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,”
anasema Kikeke.
source-. mwananchi news paper
Kurudi CTN
Baada ya kurudi katika kituo hicho, Kikeke
alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti
wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na
DTV. Baadae alihamia ITV.
Kuingia ITV/Radio One
Baada ya hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha Radio One.
“Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu
wa Kitengo cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi
chochote nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila
nikawa na ya TV”, anasema Kikeke.
Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya abadilishe
mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV. “Charles Hilary akaipeleka
ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce
Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,”
anasema.
Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi
vya taarifa za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo
mambo yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini.
Safari ya BBC
Radio One walikuwa ni Redio washirika wa BBC hivyo
walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja kila mwaka na
kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa.
Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC, ambako anaendelea hadi leo.
Familia yake
Kikeke ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu. Ni
baba wa mtoto mmoja ambaye anasoma darasa la saba nchini. “Huku London
ninaishi peke yangu,” anasema.