Na Patricia Kimelemeta na Raymond Kaminyoge
(email the author)
Posted Jumatatu,Agosti19 2013 saa 20:11 PM
Posted Jumatatu,Agosti19 2013 saa 20:11 PM
Kwa ufupi
Agizo hilo limekuja baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu, kushtushwa na matumizi makubwa.
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Hesabu za
Serikali Kuu (PAC), imeiagiza ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya Sh13 bilioni,
katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) uliofanyika Mei mwaka
2012.
Uamuzi huo umekuja baada ya kubainika kwa matumizi
mabaya ya fedha hizo, yaliyofanywa na Hazina kwa ajili ya ununuzi wa
samani za ofisini na kompyuta ndogo 200.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema
mbali na vituo hivyo, Hazina pia imenunua, seti za televisheni za
ukutani, mashine za kuchapishia karatasi, viti na makochi ya sebuleni.
Alisema ingawa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa fedha
za Serikali, baadhi yake vimeachwa katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Arusha, bila ya kuwapo kwa makabidhiano ya kisheria.
“Kamati imepata mashaka kuhusu matumizi ya Sh13
bilioni katika mkutano wa ADB, jambo lililotufanya tumuombe CAG kufanya
ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha hizi za Serikali,” alisema Zitto.
Alisema fedha hizo zilitumika bila ya kupitishwa
kwenye bajeti ya Serikali kitengo kinachotia shaka kuhusu uhalali wa
matumizi yake. Alisema mkutano huo ulifanyika kwa siku chache, lakini
kiasi cha fedha kilichotumika ni kikubwa.
“Ili tuweze kujiridhisha na matumizi ya fedha za
walipa kodi, tunapaswa kufanya ukaguzi maalumu utakaobaini uhalali wa
matumizi yake na sababu za Hazina kuziacha samani hizo kwenye kituo
kile,” alisisitiza.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Hazina, Elizabeth
Nyambibo, alisema fedha hizo zilitolewa kutoka katika mafungu
mbalimbali ya bajeti ya wizara hiyo ili kufanikisha mkutano huo.
Alisema hata hivyo fedha hizo hazikuingizwa katika bajeti kuu.
Alisema, kutokana na hali hiyo, samani hizo
zilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa ili aweze kuzihifadhi na kuzisimamia.
“Kituo cha AICC kinasimamiwa na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ndio maana tutamkabidhi Katibu Mkuu wa
wizara hiyo ili aweze kusimamia samani hizo, licha ya nyingine
kuziondoa,” alisema Nyambibo.
Wakati huohuo, kampuni 900 zimeshindwa kurudisha
mkopo wa Sh391 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya
wajasiriamali wa Tanzania. Serikali ya Japan ilitoa Sh391 bilioni kwa
Serikali ya Tanzania ili ziweze kuwasaidia wajasiriamali nchini, lakini
fedha hizo zilikopwa na baadhi ya kampuni na zingine zimeshindwa
kurudisha.
Kwa mujibu wa Kabwe, fedha hizo zilikopwa katika kipindi cha mwaka 1987 hadi 2004.
source: Mwananchi
Kwa mujibu wa Kabwe, fedha hizo zilikopwa katika kipindi cha mwaka 1987 hadi 2004.
source: Mwananchi