Thursday, 15 August 2013

CCM Taifa yapinga madiwani Bukoba Mjini kutimuliwa



Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye 
Na Mwandishi Wetu  (email the author)

Posted  Jumatano,Agosti14  2013  saa 20:17 PM
Kwa ufupi
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye asema uamuzi huo unatakiwa kutolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kagera kuwatimua madiwani wanane, chama hicho ngazi ya Taifa kimetengua uamuzi huo.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi juzi alitangaza uamuzi wa kuwatimua madiwani hao kwa kile alichosema ni kwa ajili ya masilahi ya chama na wananchi wa Bukoba.
Madiwani waliotimuliwa ni; Yusuph Ngaiza ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba na Diwani wa Kashai wakati wengine ni; Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Robart Katunzi wa Hamugembe.
Wengine waliorushiwa virago ni; Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper (Miembeni), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda (Buhembe), ambaye pia alikuwa Naibu Meya na Dauda Kalumuna aliyekuwa Diwani wa Ijuganyondo.
Mushi alisema; kwa mujibu wa Ibara ya 93, kifungu cha 15, inakipa kikao hicho mamlaka ya kuwatimua uanachama na kwamba pamoja na kukaidi maelekezo mbalimbali ya chama hicho, pia wameendelea kushirikiana na upinzani kuhujumu chama.
Tamko la CCM Taifa
Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa chama chake kimetengua uamuzi uliotolewa na Halmashauri hiyo ya Kagera kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukaidi maelekezo mbalimbali ya chama hicho.
Nnauye alisema; kutokana na utaratibu wa CCM na hayo yaliyotokea, uamuzi ni kwamba; madiwani wote waliosimamishwa wanatakiwa kuendelea na kazi zao kama kawaida hadi hapo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama itakapokutana Agosti 23 mjini Dodoma. Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Nnauye alibainisha kuwa uamuzi uliotolewa na CCM Mkoa wa Kagera wa kuwasimamisha madiwani wa chama hicho kwa madai ya kukiuka taratibu za chama sio sahihi, kwani uamuzi huo unapaswa kutolewa na Halmashauri Kuu ya Chama Taifa.
Madiwani waliotimuliwa ni wale wa Manispaa ya Bukoba ambao wamekuwa wakitajwa kumuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye amekuwa akivutana vikali na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani.
Nnauye alisema: “Tunasema kuwa uamuzi uliotolewa na Halmashauri ya Mkoa wa Kagera, kuwafukuza madiwani nane sio sahihi kwani Kamati Kuu ya CCM ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwani hata mimi Nape siwezi kutoa uamuzi kama huo.
Alisema kuwa wanatambua kwamba kuna mgogoro mzito kati ya madiwani wa CCM na Meya wa Manispaa hiyo, lakini uamuzi uliotolewa wa kuwasimaimisha sio sahihi, kwani ni kwenda kinyume na taratibu za chama jambo ambalo wao wanalipinga.
Kagasheki atoa neno
 ziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Khamis Kagasheki amesema kuwa hafahamu lolote kuhusu kufukuzwa madiwani lakini anafahamu kuwapo kwa mgogoro huo.
“Ni kweli ninaufahamu mgogoro wa madiwani wangu, nilikuwa sipo wakati wanafukuzwa, lakini kwa sasa nimerudi, nitafuatilia na kulishughulikia kwa undani zaidi ili kupunguza mgogoro huo,” alisema Kagasheki.
Aliongeza, hatua zilizochukuliwa za kuwafukuza ni kinyume na taratibu,lakini atawasiliana na viongozi hao ili kujua namna ambavyo wanaweza kulitatua suala hilo kwa busara zaidi.
Alisema, mgogoro huo ni wa muda mrefu, lakini unahitaji busara wakati wa utatuzi wake, jambo ambalo linaweza kuleta umoja na mshikamano ndani ya chama.
Kinachoelezwa na Madiwani
Nnauye alisema pia kuwa wamepokea barua za madiwani hao ambao wamesimamishwa kwa madai kwamba chanzo cha kufukuzwa kwao ni kusema ukweli kuhusu utendaji kazi wa Meya huyo.
Alisema, “Kuna tuhuma za Meya kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ambayo ni kama ile ya Soko, maji, barabara na kituo cha daladala. CCM taifa tuna taarifa za kina kuhusu mgogoro huo kitu ambacho tutakijadili kwenye kikao cha Halmashauri kuu na kukitolea uamuzi sahihi,”alisema Nnauye.
Nnauye alibainisha kuwa kutokana na tuhuma mbalimbali zinazotolewa kwa Meya huyo CCM inafanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo na kwamba chama kitatoa uamuzi pindi watakapo baini kuwa tuhuma zinazoelezwa kwa Meya zinaukweli au laa.
“Meya amekuwa akituhumiwa kuwa ameshindwa kusimamia na kutekeleza masuala mbalimbali kwenye Halmashauri ya mji huo kitua ambacho kinadaiwa kuleta mgogoro na madiwani ambao wanapingana naye, sasa ifahamike kuwa CCM haitamfumbia macho mtu yoyote anakwenda kinyume na taratibu tutafanya uchunguzi na kutoa maamuzi.”
Aidha alisema kuwa hawana uhakika kama kusimamishwa kwa madiwani hao taratibu zilifuatwa au laa jambo ambalo wao kama uongozi wa juu wa chama lazima walifanyie kazi ili kupata ukweli zaidi.
“Hatuna uhakika kama madiwani waliosimamishwa taratibu zilifuatwa ikiwa pamoja na kuwaita na kuwahoji kila mmoja, sisi kama Kamati Kuu tutakachokifanya lazima tuwaite kila mmoja atoe malalamiko yake ili tujue ukweli zaidi upo wapi,”alisema.
Nnauye alitoa mifano ya Halmashauri ambazo nazo zilikuwa na mgogoro kama wa Bukoba, Moshi na Kibondo, lakini yote ilimalizika na bila kuwana mvutano wa aina yeyote baada ya kufanyika kwa mikutano ya ndani.

“Ninachoweza kusema Bukoba wamekosea kutoa taarifa kwa umma, kwani jambo kama hili lilitokea Moshi na Kibondo, lakini ilimalizika kimya kimya bila hata kusambaa kwa kama ilivyo kwa Bukoba kwani njia za mikutano zilitumika kuondoa tofauti zilizokuwepo,”alisema Nnauye.
Madiwani wakwepa kuzungumza
Baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Bukoba waliotimuliwa, wamekwepa kuzungumzia hatima yao wakidai madai ya kufukuzwa wameyasikia kwenye vyombo vya habari na wanasubiri barua.
Madiwani hao Gasper Richard (Miembeni),Robart Katunzi(Hamugembe)walisema wanasubiri kupewa taarifa rasmi huku Deus Mtakyahwa(Nyanga)akidai alikuwa safarini.Madiwani wengine waliopigiwa simu hawakuwa tayari kupokea wala kuzungumzia lolote kuhusu kufukuzwa kwao.
Taarifa za kutimuliwa kwa madiwani hao zilileta mshtuko mkubwa mjini hapa huku wengine wakionyesha hofu ya CCM kutetea Kata kata zote nane endapo uchaguzi utafanyika kujaza nafasi hizo.
Chadema Bukoba
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Bukoba, Victor Sherejei alidai umauzi huo ulikuwa umecheleweshwa kutokana na kuendelea kwa mgogoro baina ya madiwani hao.
Mbali na kusema kuwa mgogoro huo ulikuwa unakwamisha maendeleo ya wananchi, pia alisema chama chake kina nafasi kubwa ya kuchukua kata zote za madiwani waliokuwa wa CCM endapo uchaguzi ungerudiwa.
Imeandaliwa na Phinias Bashaya, Bukoba, Patricia Kimelemeta, Aidan Mhando na Irene Moss
source: Mwananchi news paper.